Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewasilisha bungeni Muswada wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) 2025 ukiwa na lengo la kuufanyia marekebisho ikiwamo usajili wa wananchama wa sekta binafsi, sekta isiyo rasmi na watu wasio na uwezo.
Muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Bunge wa 18 uliomazika Februari 14, 2025, umependekeza marekebisho yatakayoruhusu usajili mpana wa wanachama zaidi ya watumishi wa umma.
Lengo la Serikali kuwasilisha muswada huo ni kuoanisha shughuli za mfuko huo na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI).
NHIF ilianzishwa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa mwaka 1999 ili kuwahudumia hasa watumishi wa umma.
Hata hivyo, marekebisho hayo mapya yanalenga kupanua wigo wa wanufaika kwa kujumuisha makundi mengine ya watu badala ya kusajili watumishi wa Serikali pekee.
Hatua hii mpya inakwenda sambamba na matakwa ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya mwaka 2023, inayolenga kuleta mageuzi katika mifumo ya afya ili kuongeza ulinzi wa kifedha na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wote wa Tanzania Bara.
“Muswada huu unalenga kurekebisha Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura ya 395, ili kuendana na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya mwaka 2023 na kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa sheria hiyo,” unaeleza muswada huo uliosainiwa na Waziri wa Afya, Jenister Mhagama.
Sheria ya NHIF ya mwaka 1999 imefanyiwa marekebisho mara tisa ili kuendana na mabadiliko ya sekta, teknolojia na viwango vya kikanda na kimataifa.
Baadhi ya mabadiliko yanayopendekezwa ni kifungu cha 8 kurekebishwa ili kujumuisha makundi mengine ya watu wanaopaswa kusajiliwa chini ya mfuko na siyo kwa watumishi wa umma pekee ili kupanua wigo wa wanachama kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Kifungu cha 11 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza wigo wa wanufaika, “kifungu kilivyo sasa hakijajumuisha makundi mengine ya wanachama kama vile watu wasio na uwezo, sekta isiyo rasmi na makundi mengine ya watu katika skimu ili kujumuisha wanufaika wengi na kuoanisha masharti ya sheria hii na ya Bima Afya kwa Wote.”
Wanachama wengine ni madiwani, wastaafu na watoto au wanafunzi ambao hawamo katika kundi la wategemezi. Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, umri wa mtoto anayestahili bima utaongezwa kutoka miaka 18 hadi 21.
Marekebisho mengine ni ya kifungu cha 14 kinachopendekezwa kurekebishwa ili kujumuisha baadhi ya watu na makundi ya watu ambao hawakuwa wamejumuishwa katika sheria.
Muswada pia, unataja viwango vya michango kwa wanachama wote waliosajiliwa, wakiwamo waajiriwa wa sekta binafsi rasmi na baadhi ya wachangiaji wa sekta ya umma, huku ukilinganisha michango ya sekta isiyo rasmi na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Marekebisho mengine ni kuondoa marejeo yaliyopitwa na wakati kuhusu Sheria ya Hifadhi ya Jamii, kupanua makundi ya wanachama na kutambua njia mbalimbali za utambulisho, zikiwamo za kielektroniki.
Katika mabadiliko ya uongozi, muswada unapendekeza kuwa Rais atamteua Mkurugenzi Mkuu wa NHIF badala ya bodi kufanya hivyo, ili kuboresha uwajibikaji.
Ili kuhakikisha unyumbufu katika kurekebisha viwango vya michango, muswada unampa waziri mamlaka ya kuchapisha mabadiliko yoyote katika gazeti la Serikali baada ya mapendekezo kutoka kwa bodi.
Baadhi ya vifungu vinapendekeza kuondoa jukumu la NHIF la kuthibitisha watoa huduma, badala yake mfuko huo utathibitisha watoa huduma waliothibitishwa na Wizara ya Afya.
Pia, bodi itakuwa na mamlaka ya kurekebisha vigezo vya uthibitisho bila kuzingatia mipaka ya kijiografia, hivyo kuongeza unyumbufu wa huduma kwa wanufaika.
Muswada pia, unalenga kuhakikisha utoaji wa fedha kwa watoa huduma za afya unafanyika kwa wakati kwa kuweka malipo moja kwa moja kwenye akaunti zao.
Zaidi ya hayo, muswada unapanua hatua za ufuatiliaji ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za mfuko.
Ili kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Utoaji Taarifa za Kifedha (IFRS), sheria mpya itaitaka NHIF kuwasilisha ‘taarifa ya nafasi ya kifedha’ badala ya ‘mizania.’
Kuongeza ulinzi wa kifedha umekuwa kiini cha mageuzi yanayolenga mfumo wa bima ya afya Tanzania kwa miongo miwili iliyopita.
Mbali na kupitisha sheria ya 1999 iliyoanzisha NHIF, Srikali pia ilianzisha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) mwaka 2000 kwa lengo la kusaidia kaya za vijijini katika sekta isiyo rasmi, mfuko ambao unasimamiwa na halmashauri za wilaya.
Mwaka 2005, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulianzisha fao la Bima ya Afya ya Jamii (SHIB), likifuatiwa na mpango wa Tiba kwa Kadi (TIKA) mwaka 2009.
Mnamo mwaka 2016/17, NHIF ilifanyiwa marekebisho ili kujumuisha watumishi wa umma zaidi, kuboresha uongozi na wigo wa wanufaika, pamoja na marekebisho ya CHF ili kuunda Mfuko wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa (iCHF).
Mwaka 2023, Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilipitishwa kwa lengo la kuanzisha bima ya afya ya lazima kwa wananchi wote na wakazi wa Tanzania.