*Amshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuiwezesha TASAF, agusia safari yake kielimu akitoa familia ya kaya masikini…
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WAKATI leo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ikisherehekea miaka 20 ya kuanzishwa kwake wanafunzi wanaotoka kaya masikini wametoa shukrani kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF)kuwa daraja ambalo limewezesha wanafunzi wanaotoka katika kaya zinazonufaika na mfuko huo kupata mkopo kwa asilimia 100 wanapofika ngazi ya kusoma chuo kikuu.
Kwa kukumbusha tu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii( TASAF) wameingia makubaliano ya kuhakikisha wanafunzi ambao wanatoka katika kaya masikini ambazo zinanufaika na fedha za mfuko huo wapewe mkopo kwa asilimia 100 ili kukidhi mahitaji wawapo vyuoni.
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu ,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam((DUCE)Theresia Noel anayesomea masomo ya sayansi ya siasa anatumia nafasi hii kueleza namna ambavyo TASAF imekuwa msaada mkubwa katika kufanikisha ndoto yake ya safari ya kielimu katika chuo hicho.
Teresia ambaye ni mlemavu wa viungo tangu akiwa na umri wa miezi sita amekuwa akilelewa na bibi yake mzaa baba, Angelina Joseph anayeishi Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam , anasema pamoja na changamoto nyingi ambazo amezipitia katika maisha yake ya kielimu lakini TASAF wamekuwa sehemu ya wadau muhimu kwake na hata kuwa katika chuo hicho wamefanikisha TASAF.
“Nasoma education na nimechukua masomo ya political Sayansi mwaka wa pili.Mimi ni mnufaika wa TASAF na imenisaidia katika masomo yangu naweza kusema wakati nafanya uchaguzi wa Chuo sikubahatika kuchaguliwa katika hiki Chuo cha UDSM -DUCE ila kupitia TASAF imeweza kunisaidia kwasababu nilikuwa nimechaguliwa Chuo kingine ambacho hakikuwa na mazingira mazuri kwa ajili kiti mwendo changu kuzunguka nacho.
“Hivyo nilijaribu kuongea na watu wa TASAF ambao walilibeba hili suala hili kwa mikono miwilli na kwa upande mwingine wao ndio wamefanikisha mimi leo kuwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-DUCE) na hata mkopo mimi nimepata asilimia 100 na imeweza kunisaidia mpaka sasa ninasoma,”anasema Teresia.
Akielezea zaidi Teresia anasema kwa jinsi ambavyo TASAF imekuwa msaada mkubwa kwake na familia yake anatoa ombi kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuendelea kuiwezesha TASAF ili iweze kufikia watu wengi zaidi ambao wanatoka kaya masikini na hasa zenye watoto wenye mahitaji maalum.
“Namshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuwa TASAF ila natamani zaidi aendelee kuisaipoti TASAF kwasababu inawasaidia watu sana na hata mimi kufikia ndoto zangu imetokana na TASAF hivyo iko kwa ajili yetu.
“TASAF imeanza kunigusa mimi moja kwa
moja ni wakati nataka kuja hapa Chuo kwasababu awali waliokuwa wananufaika na TASAF ni walezi wangu ambao ni bibi na babu kwa maana familia yangu.Lakini kwa sasa nanufaika nayo moja kwa moja.
“Natamani niwe kiongozi au mtu
ambaye nitakuwa na ushawishi pamoja na uwezo wa kusaidia watu ambao wanahitaji kusaidiwa kwa mfano watu wenye ulemavu natamani kuona wanafanikiwa na naiona TASAF wakienda kuifanikisha ndoto yangu na ipo siku itatimia,”amesema na kutumia nafasi hiyo kuendelea pia kuwashukuru watu wote ambao wamemshika mkono katika maisha yake mbali na TASAF.
Kuhusu mazingira ya Chuo cha DUCE amesema
ni mazuri hata katika uchaguzi wake wa chuo baaada ya kuona amechaguliwa Chuo fulani na mazingira yake hayakuwa mazuri Chuo ambacho kilikuja kichwani kwake moja kwa moja ni DUCE na hata alipoanza masomo yake anasoma vizuri kwani hakuna changamoto.
Teresia ambaye ni mnufaika wa TASAF alizaliwa mwaka 2002 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Jeshi la Uokovu jijini Dar es Salaam na alifanikiwa kufaulu masomo ya elimu ya msingi ,hivyo alijiunga sekondari ya Jangwani na baadae akaendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.
Alipomaliza alienda mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) ambako nako alifanya vizuri na sasa anaendelea na masomo yake DUCE akiwa mwenye furaha na tabasamu muda wote licha ya kwamba mama yake mzazi alimkimbia akiwa na miezi sita tangu kuzaliwa kwake na hajawahi kumuona wala kuwasiliana naye ingawa anaweka wazi kwake ameshamsamehe mama yake na hana kinyongo naye.
Kwa upande wa Bibi yake na Teresia,Angelina Joseph anasema kuwa anaishukuru TASAF kwa kuwezesha mjukuu wake kupata mkopo wa asilimia 100 kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ,kwani kwa sasa anaweza kupata fedha za kujikimu kwa kununua vifaa vya shule.
“Teresia alikimbiwa na mama yake akiwa na miezi sita tu hivyo nimemlea mwenyewe tangu wakati huo hadi sasa.Alipozaliwa alikuwa na changamoto ya TB ya uti wa mgongi ambapo nililazwa Hospitali ya Muhimbili kwa miezi sita na nikiwa pale kuna daktari mmoja aliniambia huyu mtoto mpeleke shule nisimuache kwani anaakili sana.
“Kilichonisukuma ni daktari wa Muhimbili ambaye alikuwa ananihamasisha nimpeleke shule kwani tatizo lake ni miguu sio mikono na nashukuru Mungu kuna rafiki yangu alilijitolea kumnunulia baiskeli na kulipa Ada ya chekechekea miezi sita na huo ukawa mwanzo wa Teresia kwenda shuleni.
“Natamani kuona Mungu anamsaidia Teresia anatimiza ndoto zake ili naye aje anisaidie na namuona ndio msaada wangu wa baadae.Tunamshukuru Rais Samia kwa kuwa na Mfuko wa TASAF ambao unawasaidia watu wa kaya masikini kama sisi na ombi langu kwake aendelee kuipa nguvu ili iwasaidie wananchi wengi zaidi.”
Awali Madame Madame Mercy Hozza ambaye ni Mtalaam wa wenye ulemavu hasa wasioona amesema Chuo hicho kinatekeleza sera ya elimu jumuishi na inahudumia wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji Maalum
Teresia ni mlemavu wa viungo na sio mlemavu wa miguu na jinsi ambavyo anaishi hapa chuoni ni mwanafunzi anayeshiriki masoko kama wanafunzi wengine wasio na changamoto yoyote,anajifunza katika darasa moja na wanafunzi wenzake,anatumia miundombinu pamoja na wenzie pasipo changamoto yoyote.
“Ni binti ambaye anajitahidi katika masomo ,anashiriki masomo yake yote,semina na mafunzo kwa vitendo.Ni mwanafunzi ambaye pamoja na changamoto ya ulemavu haijaweza kumuathiri kutokufanya vizuri katika masomo yake. Mwito wangu kwa jamii na mtu yeyote mwenye mtoto mwenye ulemavu hakuna sababu ya kumficha ndani.
“Tunaona watu wenye ulemavu wengi tu wakifanya shughuli mbalimbali ,wapo walimu vyuo vikuu,Sekondari na msingi,lakini wako watu wenye ulemavu ambao ni watalaam wa fani mbalimbali.Kwahiyo hakuna sababu ya kuficha mtoto mwenye ulemavu ndani.
“Mtoto mwenye ulemavu anamchango mkubwa kwa jamii, hivyo tuwatoe ndani na tuhahamasishe jamii watoto wasikae ndani.Wakati mwingine wenye ulemavu wanafanya vizuri zaidi kuliko hata wasio na ulemavu na hapa tunaoushahidi mwanafunzi asiyeona amewahi kuwa mwanafunzi bora.” .