Buchosa. Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wanaotumia kivuko cha Kome II wamelazimika kulipia Sh500 kubebwa mgongoni ili kufikishwa kwenye kivuko hicho baada ya gati kujaa maji.
Kujaa kwa maji katika gati hilo ni matokeo ya kuongezeka kwa maji katika Ziwa Victoria kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti yanayozunguka ziwa hilo.
Baadhi ya abiria hao hawataki kukanyaga maji huku wengine wakiogopa kuliwa na mamba kutokana na kukanyaga maji ya Ziwa Victoria, hivyo kuamua kulipia kiasi hicho ili kufikishwa kwenye kivuko.
Kivuko cha Kome II kinachofanya safari zake kati ya Nyakaliro na Kome, kina tani 45 ambapo kina uwezo wa kubeba abiri 100 na magari madogo matano kwa wakati mmoja.
Mmoja wa wananchi, Asteli John amesema wanalazimika kulipia fedha hiyo ili kukwepa kukanyaga maji huku abiria wengine wakilazimika kukanyaga maji kwa sababu hawana fedha hiyo ili wabebwe.
“Tunapata mateso makubwa hasa tunapokuwa na watoto wakati wa kuvuka tunaiomba Serikali itusadie jambo hili kwa kuweka mawe ili abiria waondokane na usumbufu,” amesema John.
Wananchi wanaovuka kwa miguu wameiomba Serikali kuharakisha kutengeneza gati ili waepukane na athari zinazoweza kutokea ikiwemo ya kuliwa na mamba wanaozagaa baada ya kina cha maji kuongezeka ndani ya Ziwa Victoria
“Mamba nao ni hatari baada ya kina cha maji kujaa ndani ya ziwa Victoria wameanza kuzagaa kila mahari,” amesema Jonathani.
Tulubuza Amoni, mkazi wa Buhama kisiwani Kome, amesema umefika wakati sasa Serikali iangalie upya namna ya ujenzi wa magati hayo unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, lengo ni kuwaondolea adha wananchi wanaotumia vivuko.
“Wakati magati haya yanajengwa, kina cha maji kilikuwa hakijaongezeka hivyo muda wa kujengwa magati ni wakati huu baada ya maji kuongezeka,” amesema Amoni.
Baadhi ya wananchi wanaofanya shughuli za kubeba watu wasikanyage maji kwenda kwenye kivuko wamesema ongezeko la kina cha maji ndani ya ziwa wao limewapatia fursa ya kujipatia riziki ya kuendesha maisha yao na familia zao.
Kazimili Athumani ni mmoja wa vijana wanaofanya kazi hiyo, amesema kazi hiyo inamfanya apate kipato cha karibu Sh30,000 kwa siku.
Meneja wa vivuko vya ziwa magharibi, Vitalis Bilauli amesema wamefanya tathimini maeneo yote yaliyoathirika na mvua likiwemo la kivuko cha Nyakaliro – Kome ili waone namna ya kuwasaidia wananchi kuondokana na adha hiyo.
“Siyo Buchosa tu, ni maeneo mbalimbali ikiwemo Kigoma, Mwanza na Msoma, hivyo tumejipanga na tutahakisha tunarekebisha maeneo hayo ili wananchi waweze kuyatumia bila wasiwasi,” amesema Bilauli.
Akizunguza na Mwananchi kwa njia ya simu, mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amesema madhara yaliyosabibishwa na mvua hadi kuongezeka kwa kina cha maji ndani ya ziwa kumeathiri miundombinu mbalimbali yakiwemo magati, hivyo Serikali inafanya mchakato wa kuhakisha wanarudisha hali nzuri na kuwaondolea adha wananchi.
“Nawaomba wananchi wa Buchosa kuwa na subira wakati Serikali ikifanya tathmini juu ya madhara yaliyosabishwa na mvua, lengo ni kuhakikisha wanaondolea adha wananchi,” amesema Shigongo.
Mkuu wa Wilaya Sengerema, Senyi Ngaga amewatoa hofu wananchi kuwa Serikali itarekebisha maeno yote ambayo yameharibiwa na mvua na kuwaondolea usumbufu.