Mziki wa Samatta wamkuna kocha PAOK

KOCHA wa PAOK, Razvan Lucescu, ameonyesha kuridhishwa na kiwango cha sasa cha mshambuliaji wake na nahodha wa Taifa Stars,  Mbwana Samatta ambaye amefunga mabao manne na kutoa asisti moja katika michezo mitatu iliyopita na mashindano yote ikiwemo Europa League.

Samatta aliyeanza kuonyesha makali kuanzia Februari 8 katika mchezo wa Ligi Kuu Ugiriki ‘Super League’ dhidi ya OFI Crete kwa kufunga mabao mawili wakati PAOK ikishinda mabao 5-0, awali hakuwa na nafasi kabisa kwenye kikosi hicho cha Lucescu kiasi cha kuwekwa sokoni.

Mromania huyo alisema; “Samatta ana uwezo mkubwa, na nimefurahi kuona anachangia kwa namna nzuri kwenye mashindano yote. Kila mara anapokuwa uwanjani, anaonyesha jitihada kubwa na anapambana kwa nguvu zote. Kuwepo kwake kwenye kikosi changu ni faida kubwa kwa timu.”

Baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya OFI Crete, Samatta aliendeleza makali tena kwa kufunga bao moja wakati PAOK ikipoteza 2-1 mbele ya FC Steaua București na jana Jumapili katika mchezo wa Ligi, akafunga na kutoa asisti wakati chama lake likiibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Lamia.

Lucescu aliongeza: “Mbwana ni mchezaji ambaye ameonyesha kuwa na uwezo wa kufunga licha ya changamoto ambazo amepitia ameonyesha ukomavu, na hili limethibitishwa na mabao yake katika michezo ya hivi karibuni. Si tu kwamba anafunga, bali pia anachangia kwenye uchezaji wa timu. Hii ni sifa ya mchezaji anayejua umuhimu wa timu na anafanya kila linalowezekana kuleta mafanikio kwa klabu.”

Samatta, aliyejiunga na PAOK msimu uliopita, amekuwa akijitahidi kurejea kwenye kiwango cha juu baada ya msimu wa kwanza usio na mafanikio makubwa, ambapo alifunga mabao mawili na kutoa asisti nne katika michezo 29 ya Ligi Kuu ya Ugiriki. Hata hivyo, mwaka huu ameonesha mabadiliko makubwa katika uchezaji wake, na amekuwa sehemu ya mafanikio ya PAOK katika michezo ya hivi karibuni.

Lucescu alielezea pia kuwa, ingawa Samatta alikumbwa na changamoto za kuzoea ligi ya Ugiriki mwaka jana, ameweza kujua vizuri nini kinachohitajika ili kufanikiwa kwenye Ligi Kuu ya Ugiriki.

“Kila mchezaji anahitaji muda ili kujua ligi, na Samatta amethibitisha kuwa ni mchezaji mwenye akili ya mpira na uwezo wa kutatua changamoto za kila mechi,” aliongeza kocha huyo.

Kwa sasa, PAOK inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Super League ya Ugiriki, ikiwa na pointi 43, nyuma ya Olympiacos Piraeus, AEK Athens, na Panathinaikos, ambazo zote ziko kwenye mbio za kutafuta ubingwa.

Ingawa kuna changamoto kubwa mbele, Lucescu ana imani Samatta atakuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika juhudi za timu hiyo kutafuta mafanikio msimu huu. Alhamisi ijayo, PAOK itakuwa Bukarest, Romania kucheza mchezo wa marudiano ya Europa League dhidi ya Steaua București.

Related Posts