Mapya Wapakistan wanaodaiwa kusafirisha dawa za kulevya

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na uchunguzi wa kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 447.3 inayowakabili raia nane wa Pakistan, washtakiwa hao wamedai kuwa hawana nguo za kubadilisha huko gerezani.

Pia, washtakiwa hao wamedai hawana mawasiliano na familia zao zilizopo Pakistan, tangu walipofikishwa mahakamani hapo.

Washtakiwa hao wametoa taarifa hiyo leo, Februari 17, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025 ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam(50) maarufu kama Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi(55).

Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).

Awali, Wakili wa Serikali Aron Titus aliieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya Mahakama yao na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai wakili Titus.

Titus baada ya kueleza hayo, mmoja wa washtakiwa hao kwa niaba ya wenzake mshtakiwa Hanif alidai kuwa tangu wapelekwe gerezani hawana nguo za kubadilisha na pia hawana mawasiliano na ndugu zao waliopo Pakistan.

“Unavyotuona hapa mahakamani, sisi hatuna nguo za kubadilisha kule gerezani, lakini pia hatuna mawasiliano na ndugu zetu tangu tulivyokamatwa, tunaomba tusaidiwe mawasiliano ili tuwasiliane na ndugu zetu walipo Pakistan,” amedai.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza hoja aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, 2025 kwa kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Januari 9, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 25, 2024 eneo la Navy lililopo Kigamboni Wilaya ya Kigamboni, kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine.

Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya aina heroini, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024 eneo la Navy Kigamboni na kukutwa na heroini zenye uzito wa kilo 22.53.

Related Posts