Bodi ya mikopo yavuna faida Sh1.5 trilioni ndani ya miaka 20

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh1.5 trilioni imetengenezwa kama faida na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kupitia mikopo ya Sh8.2 trilioni iliyotolewa kwa wanafunzi.

Faida hiyo imepatikana kupitia mikopo iliyowanufaisha zaidi ya wanafunzi 830,000 waliosoma katika ngazi mbalimbali ndani ya miaka 20.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya bodi hiyo yaliyofanyika leo, Februari 17, 2025 katika Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

Majaliwa amesema mafanikio yanayosherehekewa ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na michango ya viongozi waliopo.

“Utashi huu ni wa viongozi wetu katika awamu zote waliotekeleza kazi kubwa ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri. Viongozi wetu waliona mbali na kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo,” amesema Majaliwa.

Amesema kupitia mikopo iliyotolewa, bodi imefanikiwa kukusanya Sh1.5 trilioni kama faida.

“Ninatambua marejesho haya yamepatikana kutokana na jitihada na ubunifu mkubwa unaosaidia kuwafikia wanufaika waliomaliza masomo yao na mikopo yao kuiva,” amesema.

Wakati ufanisi huo ukipatikana, Majaliwa amesema kuwa ili kuhakikisha mikopo ya elimu ya juu haiwi mzigo kwa wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo.

“Kwa sasa mnufaika anarejesha kiasi kilekile alichokopeshwa, kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha ongezeko la madeni ya mikopo hiyo,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuiagiza bodi ya mikopo kuendelea kuweka mikakati ya kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kufanya maboresho ili kujiunganisha na kuzungumza lugha moja na taasisi za fedha nchini.

Kuhusu tozo aliyoizungumzia Waziri Mkuu, Mei 4, 2021, Serikali iliagiza Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB kuondoa adhabu ya asilimia 10 ya mkopo iliyokuwa inatozwa kwa wanufaika waliochelewesha kulipa mikopo hiyo.

Agizo hilo lilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alipokuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete

Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza, kufuta tozo ya asilimia sita ya mikopo inayotolewa na bodi hiyo.

Katika utekelezaji wa agizo hilo, Profesa Ndalichako alisema kuwa Serikali itaondoa tozo ya asilimia sita ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo, kuanzia Julai mosi, 2021.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, fedha zilizokuwa zinatolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zilikuwa Sh464 bilioni.

“Lakini alipoingia, aliagiza fedha za mikopo ziongezwe. Tuliongeza hadi kufikia Sh570 bilioni, kisha Sh654 bilioni, na sasa ni Sh731 bilioni,” amesema.

Mbali na mikopo hiyo, Serikali pia ilianzisha ufadhili kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ili kuwavutia zaidi na kuchochea uzalishaji wa wataalamu wengi katika kada mbalimbali.

Kupitia Samia Scholarship, wakati wa kuanzishwa kwake, Sh3 bilioni zilitolewa kama majaribio. Baadaye, kiasi hicho kiliongezwa hadi Sh6 bilioni, na sasa kimefikia Sh8.9 bilioni.

Related Posts