Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi mbili za kumiliki mijusi 226 aina ya Coud Gecko yenye thamani ya Sh13.8milioni, inayomkabili mfanyabiashara, Hika Shabani Hika (48) maarufu Majoka na Shaban Salum Mzomoke (45) maarufu kama Kisukari, haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Frank Rimoy ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Februari 17, 2025 wakati kesi hizo zilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Rimoy ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Kutokana na hali hiyo, hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hadi Machi 17, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Katika kesi ya kwanza, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2997/2025.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025, eneo la Shekilango lililopo wilaya ya Ubungo.
Inadaiwa siku hiyo washtakiwa walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali ambazo ni mijusi 213 aina ya Coud Gecko yenye thamani ya Sh13, 051,575 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Shtaka la pili ni kujihusisha na nyara hizo tukio wanalodaiwa kulitenda Januari 10, 2025 eneo la Shekilango wilaya ya Ubungo, ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mijusi hao bila kuwa na kibali.
Shtaka la tatu ni kumiliki nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda Januari 10, 2025 eneo la Mwanagati, Wilaya ya Ilala na walikutwa na mijusi 213 aina ya Coud Gecko ya Sh15,051,575 mali ya Serikali.
Katika kesi ya pili, Wakili Mafuru alidai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2998/2025.
Aliwataja washtakiwa hao katika kesi hiyo kuwa ni Shaban Mzomoke na Hika Hika, wanaokabiliwa na mashtaka matatu.
Akiwasomewa mashtaka yao, wakili Mafuru alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025 eneo la Shekilango,
Siku hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya mijusi mikubwa 13, ambayo imekufa yenye thamani ya Sh765, 575.
Shtaka la pili ni kujihusisha na nyara hizo na shtaka la tatu ni kumiliki mijusi hiyo, bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Wakili Mafuru alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao, Februari 4, 2025.