Dar es Salaam. Serikali imependekeza kufanya mabadiliko ya vifungu 20 vya Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Sura ya 295 ili kutatua changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Miongoni mwa maeneo yaliyoguswa ni kuongeza ruzuku kama chanzo cha mapato cha NHC, mwajiri kuondolewa uwezo wa kukata kiasi cha pesa kama kodi ya nyumba pamoja na faini ya kutolipa kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi ambaye ni mpangaji wa NHC.
Maeneo mengine yaliyoguswa ni kuongezwa faini inayotozwa na NHC, kupanua wigo wa nyaraka ambazo mkurugenzi mkuu anaweza kukasimisha mamlaka ya kuzisaini kwa maofisa waandamizi wa shirika.
Hayo yamebainishwa kupitia muswada wa mabadiliko ya sheria uliowasilishwa bungeni ukiakisi kufanya maboresho ya sheria
ya NHC iliyotungwa mwaka 1990 kwa madhumuni ya kuvunja Ofisi ya Msajili wa Majumba, kuunda upya Shirika la Nyumba la Taifa na kuweka masharti yatokanayo na yanayohusiana na hayo.
Muswada huu unaeleza kuwa tangu kutungwa kwake, sheria hii imefanyiwa marekebisho mara moja kwa lengo la kuboresha majukumu ya Shirika.
Kifungu cha 23 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza ruzuku kama chanzo cha mapato ya Shirika. Lengo la marekebisho haya ni kuboresha uwezo wa kifedha wa Shirika kwa lengo la utekelezaji bora wa majukumu yake.
Akizungumzia uongezaji wa ruzuku kama moja ya chanzo cha mapato, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Felix Nandonde amesema ni jambo zuri lakini ni vyema ielezwe ni kwa ajili ya kazi gani.
“Kama ambavyo inatolewa katika kilimo na kuelezwa kuwa ni kwa ajili ya pembejeo vivyo hivyo na hii ielezwe ni kwa ajili ya kazi gani kama ni kujenga nyumba za bei nafuu au la,” amesema Dk Nandonde.
Amesema mahitaji ya nyumba kwa mwaka Tanzania ni zaidi ya 200,000 hivyo kuipatia ruzuku inaweza kuwa moja ya njia ya kuchochea mabadiliko na upatikanaji wa nyumba za bei rahisi.
“Nakubaliana nayo lakini inapaswa kuwekezwa katika maeneo gani, ndiyo linapaswa kujadiliwa, kama ni ujenzi isiwe nyumba tu bali miundombinu wezeshi kwa jamii ikiwamo uwezeshaji kiuchumi kwani moja ya changamoto ya wenye viwanda vidogo ni kukosa maeneo ya kufanyia biashara, NHC wanaweza kuwekeza viwanda,” amesema.
Eneo lingine wanaloweza kulitumia ni kujenga maeneo ya uwezeshaji kilimo ikiwamo vyumba baridi (cold rooms) kwa ajili ya kusaidia wakulima wa mboga na matunda kuhifadhi mazao yao kabla ya kufikishwa sokoni.
“Kuangalia maeneo ambayo nchi inaangalia sana kama kilimo ambayo kwa sasa kinaleta fedha nyingi za kilimo,” amesema.
Mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi amesema kutoa ruzuku ni jambo jema lakini ni vyema kutofautisha kazi za ruzuku na zile za kibiashara zinazofanywa na NHC.
“Ningetamani hiyo kazi itenganishwe na kazi ya kibiashara, ukichanganua majukumu ya kusaidia jamii na majukumu ya kibiashara inaweza isiwe jambo ambalo linaloweza kuwapima na kutoa mwongozo sahihi wa uwekezaji. Ni lazima hiyo sheria iwekwe kwa umakini ambayo inatofautisha kazi ya kibiashara na ile inayopewa ruzuku, inaweza kuwa fursa ya matumizi mabaya ya rasilimali,” amesema Dk Olomi.
Kwa mtazamo wake ruzuku ingeelekezwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao wanajenga majengo ya Serikali kuliko NHC ambao wanapaswa kujiendesha kibiashara.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja amesema kutolewa kwa ruzuku kunaweza kusaidia wananchi kupata huduma kwa gharama nafuu zaidi.
Katika ukusanyaji wa kodi, muswada huu umegusa na kufanya marekebisho katika vifungu vya 12 na 13 ambayo sasa yanaondoa wajibu wa mwajiri kukata kiasi cha pesa kama kodi ya nyumba pamoja na faini ya kutolipa kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi ambaye ni mpangaji wa Shirika.
Kwa mujibu wa utaratibu unaopendekezwa waajiriwa watalipa kodi ya pango kama ambavyo wapangaji binafsi wanalipa.
“Lengo la marekebisho haya ni kuongeza uwajibikaji wa moja kwa moja kwa mpangaji katika kulipa kodi ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Shirika,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kifungu cha 24 kinapendekezwa kurekebishwa kwa kuondoa mamlaka ya bodi ya kudhamini mikopo ya shirika. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya kifungu hicho na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya Serikali, Sura ya 134, ambayo inabainisha taratibu za upatikanaji wa mikopo na dhamana ya Serikali.
Vifungu vya 25 na 26 vinapendekezwa kufutwa ili kuondoa masharti yanayohusu Mfuko wa Dhamana na Mfuko Mkuu wa Akiba ulioundwa chini ya Sheria hii. Lengo la marekebisho haya ni kuruhusu fedha za shirika kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348.
Kifungu cha 27 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuiwezesha bodi kuwekeza bila kuhitaji kupata idhini ya waziri. Lengo la marekebisho haya ni kuliwezesha shirika kuwekeza kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, Sura ya 370 kuhusu uwekezaji wa mashirika ya umma.
Kifungu cha 31 kinapendekezwa kurekebishwa na kifungu cha 31A kinapendekezwa kuongezwa kwa lengo la kuondoa rejea ya masharti yanayohusu mgongano wa maslahi yaliyo katika Sheria ya Ardhi, Sura ya 113.
“Lengo la marekebisho haya ni kuweka masharti bora ya utaratibu wa udhibiti wa masuala yanayohusiana na mgongano wa maslahi ili kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kifungu cha 32 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza adhabu ya jumla. Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha adhabu kutolewa kulingana na hali halisi ya thamani ya fedha na uzito wa kosa.
Jedwali la Sheria linapendekezwa kurekebishwa ili kuwianisha masharti yanayohusu bodi na taratibu zilizopo za usimamizi wa mashirika ya umma. Lengo la marekebisho haya ni kuboresha mfumo wa utawala wa bodi ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji wake.