Wananchi Vunjo Kusini waondokana na adha ya kukosa mawasiliano

Moshi. Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kirua, Vunjo Kusini wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, wameondokana na adha ya kukosekana kwa mawasiliano baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara ya mawasiliano.

Awali, wananchi hao, wakiwemo wafanyabiashara, walikuwa wakikumbana na adha ya kutembea umbali mrefu au kupanda maeneo ya milimani kutafuta mtandao.

Wananchi hao wameeleza hayo leo Jumatatu, Februari 17, 2025 kijijini humo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipokagua mradi wa minara 758 ya mawasiliano inayojengwa nchini na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Mmoja wa wananchi hao, Tarsila Francis, amesema awali wao kama wafanyabiashara walikuwa wanakosa namna ya kuwasiliana na wafanyabiashara wenzao au kuagiza bidhaa.

“Wafanyabiashara tulikuwa tunapata shida sana kuwasiliana na wafanyabiashara wenzetu au kuagiza bidhaa. Kiuchumi, mnara huu umetunufaisha kwa sasa hata nikiwa ndani napata mawasiliano, naagiza bidhaa bila changamoto,” amesema.

Naye Litropia Ngowi amesema awali kabla ya kujengwa minara hiyo walikuwa wakilazimika kupanda maeneo ya mlimani kufuata mtandao.

“Hakukuwa na mawasiliano kabisa, wakati mwingine unalazimika kupanda maeneo ya mlimani au wengine wanapanda juu ya miti kufuata mtandao, ila kwa sasa tunashukuru Serikali, changamoto hii imeisha,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa UCSAF, Albert Richard, amesema katika kijiji hicho moja ya minara iliyojengwa inahudumia wananchi zaidi ya 27,000 ambapo Sh120 milioni zimetumika katika ujenzi wa mnara mmoja ambao Serikali imetoa ruzuku kwa kampuni ya simu ya Vodacom.

Amesema Mei 13, 2025 minara yote 758 itakuwa imekamilika, ambapo kati ya hiyo, hadi sasa minara 402 imekamilika na kuwashwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo wananchi zaidi ya milioni 8.5 watanufaika na huduma hiyo muhimu ya mawasiliano.

Naye Mbunge wa Kinondoni na mjumbe wa kamati hiyo, Abbas Tarimba, ameitaka Serikali kupitia UCSAF kuhakikisha inaweka mikakati ya kuhakikisha minara inajengwa kila mara ili maeneo yote yapate mawasiliano.

Aidha, amesema badala ya Serikali kuwapa ruzuku kampuni za simu, ni afadhali kuangalia namna bora ya kujenga minara hiyo wenyewe na kukodisha kwa watoa huduma.

“Ili nchi yetu iwe na mawasiliano kote, ni lazima tulipe hili jambo kipaumbele tusikae nyuma na kusubiri miaka iende tuanze ujenzi wa minara katika maeneo mengine. Matumizi ya mitandao yanaongezeka, hivyo tuangalie kila mara kuhusu utoshelevu na kuhakikisha kila mahali mawasiliano yanapatikana,” amesema.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustine Holle, amesema wanaipongeza Serikali kwa ujenzi wa minara hiyo ya mawasiliano na kuwa itaongeza mapinduzi kwenye mawasiliano na kiuchumi katika jamii.

Related Posts