Ni mara kadhaa nimekutana na wazazi wanaolalamika kwamba anatumia fedha nyingi kulipa ada lakini mtoto wake hafanyi vizuri na wengine wanapoteza kabisa uelekeo kwenye elimu.
Kilio cha wengi ni kwamba natafuta hela kwa jasho ila zinaishia kupotea maana huyu mtoto hana anachoingiza kichwani na walimu wake wameshindwa kabisa kumsaidia.
Malalamiko haya yamenifanya leo nizungumze na wazazi wenzagu, nimegundua kuna makosa tunayafanya na ndiyo yanaathiri ustawi wa watoto wetu.
Wengi tunatamani watoto wetu wapate elimu, kwa maana ya kufanya vizuri kwenye masomo yao ajabu ni kwamba hatutaki kuwa sehemu ya safari hiyo.
Nasema hivi kwasababu sijui ni kwa bahati mbaya au makusudi, wazazi wengi wanakwepa kushiriki kwenye elimu ya watoto wao.
Hii inaweza isionekane kuwa na maana lakini ukweli ni kwamba wengi huishia kulipa ada na kusubiri matokeo ya mtihani.
Labda niwafahamishe kwamba elimu ya mtoto ni mchakato ambao mzazi anapaswa kushiriki kwa namna moja au nyingine.
Mbali na kulipa ada na kuangalia matokeo ya mitihani ni muhimu kuwa na uangalizi na ufuatiliaji wa karibu.
Hapa kwenye ufuatiliaji ndiyo sehemu yenye umuhimu zaidi, mzazi ni lazima ufahamu kama kweli mtoto wako anakwenda shule na anaelewa kile anachofundishwa.
Ukifanya hivi hautashangazwa na matokeo atakayopata kwenye mitihani, kwa sababu utakuwa unaelewa kwa kina uelewa wake kwenye masomo.
Hili litawezekana endapo kutakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya mzazi na mwalimu, hapa mtaweza kumfuatilia mtoto na kumsaidia pale itakapoonekana anahitaji msaada ili aweze kuelewa kile anachofundishwa.
Ajabu ni kwamba kuna wazazi ambao hawafahamu hata walimu wa madarasa ya watoto wao, huu ni mwezi wa pili tangu watoto wapande madarasa au waanze shule kwa wale wanafunzi wapya lakini unakuta mzazi hamfahamu mwalimu wa darasa la mtoto wake.
Sasa unajiuliza huyu mzazi anapata vipi taarifa na maendeleo ya mtoto wake ikiwa hajawahi kukanyaga shule, hana mawasiliano na wala hamfahamu mwalimu wa darasa ukiuliza nini amelipa ada anaamini ameshamaliza kazi yake.
Wapo wazazi ambao tangu amemuandikisha mtoto darasa la kwanza au kidato cha kwanza hajawahi kukanyaga shule wala kushiriki vikao vya wazazi vinavyoitishwa kwa kisingizo kile kile hana muda.
Inawezekana usiende shule walau uwe na muda wa kufuatilia madaftari na kuzungumza na mtoto kujua alichojifunza kwa siku husika, hilo pia mtu anaona gumu akidai ametingwa na majukumu ya utafutaji ilia pate hayo mamilioni ya ada.
Labda niwakumbushe wazazi wenzangu kwamba kutafuta fedha kwa jasho, machungu na masimango haileti matokeo chanya kwenye elimu ya mtoto wako kama hufuatilii. Kutafuta hela na kulipa ada ni jambo moja na kusimamia na kufuatilia elimu ya mtoto wako ni jambo lingine.
Hata utafute kwa jasho kiasi gani kupata fedha ya kulipa ada hiyo haiwezi kuwa tiketi ya kumuwezesha mwanao asimame kwenye mstari, una nafasi yako muhimu katika elimu ya mtoto wako.Mungu hawezi kutuma malaika kutoka mbinguni afuatilie elimu ya mtoto wako kwa sababu wewe hauna muda.
Kulipa ada hakumfanyi mwalimu amfuatilie mtoto wako, jiulize darasa analosoma lina wanafunzi wangapi hadi mwalimu aweke nguvu kwa mwanafunzi mmoja bila msukumo wa mzazi wake.
Tunasahau kwamba elimu sio akili ya darasani pekee, inahusisha nidhamu, ushirikiano na stadi nyingine muhimu hivi vyote vinajengwa kwa ufuatiliaji na usimamizi.
Sasa kama wewe mzazi utakuwa unaridhishwa na matokeo ya mitihani pekee, ukajiona huna sababu ya kumfuatilia mtoto, isifike wakati ukatafuta wa kumlaumu kwa mwenendo wake mbaya katika nyanja nyingine.