Haya yafanyike kusukuma ushiriki wa wasichana kwenye sayansi

Dodoma. Takwimu za elimu na ajira duniani zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana katika elimu na ajira kwenye fani za sayansi ni mdogo ikilinganishwa na ushiriki wa wanaume.

Machi mwaka 2023, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Gema Modu alisema bado idadi ya wanawake wataalamu katika fani ya uhandisi ni wachache, jambo linalochagiza kuongeza ushawishi kwa wasichana kusoma masomo ya sayansi.

Alisema wahandisi waliosajiliwa nchini ni takribani 35,000 lakini kati ya hao wanawake ni 4,000 tu na kwamba jambo wanalolifanya ni kushirikiana na jamii kujenga ushawishi kwa wasichana kusoma masomo ya sayansi, ili kuongeza idadi ya wanawake kwenye fani hiyo.

Changamoto hiyo ndio iliyolisukuma Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, kuanzisha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi.

Baraza likaitangaza Februari 11 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika sayansi.

Lengo la maadhimisho haya ni kujadili na kutafakari kuhusiana na ushiriki mdogo wa kundi hilo na kutambua pia mchango wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, fani ambazo kwa kifupi hujulikana kwa jina la STEM.

 Ni wazi kwamba ili kushiriki katika ajira za sayansi ni lazima kujenga msingi bora wa watoto wa kike katika elimu tangu wakiwa katika ngazi ya awali, sekondari, vyuo na vyuo vikuu kwa kuhakikisha watoto hao wanapata ushawishi mkubwa wa kuyapenda na kujifunza kwa bidii.

 Akizungumza na Mwananchi, mwalimu wa masomo ya kemia na hesabu, Pascal Ibrahim anasema wazazi, jamii na Serikali, wanatakiwa kuhamasisha wasichana tangu wakiwa wadogo katika shule za msingi na sekondari kwamba wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi.

 Anasema uhamasishaji huo ulenge katika kuwatia moyo kuwa wanaweza kufanya mambo ambayo wengine wamekuwa hawaamini kuwa wasichana ama wanawake wanayaweza.

 Anatoa mfano wa mambo wanayotakiwa kuhamasishwa watoto wa kike kuwa wanaweza kusoma wakawa madaktari bingwa, wahandisi wabobevu, wanamahesabu mahiri bila kusahau wanatehama waliobobea .

“Wasichana na wanawake wao wenyewe wawe na imani kubwa juu ya uwezo, ambao wamejaliwa na Mwenyezi Mungu kwamba wanaweza kufanya vizuri katika kila jambo pamoja na masomo ya sayansi, ”anasema na kuongeza:

“Ninaamini juhudi ni mafanikio. Hata kama wataona wanashindwa ila wasikate tamaa, kwa kuwa wanachokikatia tamaa hata hakikatishi tamaa.”

 Anasema pia walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, hisabati na Tehama wahakikishe kuwa wanazingatia suala la usawa wa kijinsia, bila kuwabagua wasichana na wanawake maana jamii hasa ya walimu katika baadhi ya maeneo imekuwa ikiamini masomo hayo ni ya wanaume tu.

 Anasema wamekuwa wakiamini wasichana wanatakiwa kusoma masomo ya sayansi ya jamii tu, jambo ambalo siyo sawa na pengine hata kuwatoa wasichana katika madarasa ya sayansi kwamba hawataweza kwa kuwa ni magumu.

 Ibrahim anasema badala ya kufanya hivyo jamii na walimu wanatakiwa kuwa sababu ya wasichana kuongezeka kwa wingi kusoma masomo ya sayansi na teknolojia, kwa kuwashawishi kujifunza masomo hayo kwa sababu wanaweza.

“ Ninapendekeza yaandaliwe makala kuwafikia wanafunzi shuleni kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kwa ajili ya kuwahamasisha wanafunzi wote kwa ujumla wasichana kwa wavulana katika shule za msingi na sekondari ya chini za umma na binafsi,”anasema.

 Anasema wanafunzi hao wanatakiwa kuhamasishwa umuhimu wa masomo hayo kwa kuwa kuwa hivi sasa ndani ya zama za maendeleo ya sayansi , teknolojia, siyo rahisi kuwaajiri wahitimu wote.

 Ibrahim anasema wanafunzi wapatapo maarifa na ujuzi wa masomo haya watajipa fursa ya kuwa wagunduzi wa mambo mbalimbali yatakayowasaidia maishani mwao.

Mazingira ya shule yaboreshwe

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Mayamaya mkoani Dodoma, Rahma anasema ni muhimu kwa watoto kuhamasishwa kusoma masomo ya sayansi na teknolojia shuleni, pamoja na kuwa na vitendea kazi vya kutosha kwa ajili ya kufundisha masomo hayo.

“Kwa mfano, masomo ya Tehama ni muhimu kitakachokuwa kinafundishwa kiwe na vitendea kazi vyote kwa hiyo wanafunzi wanakaa hasa wakijua wanafundishwa Tehama. Siku ya somo la sayansi, mwalimu avae kabisa koti la udaktari ama sare za muuguzi ndio itasaidia kuhamasisha wanafunzi kujifunza masomo hayo,”anasema.

Aidha, anasisitiza uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia hasa kwa shule za vijijini kwa kuhakikisha zinakuwa na madarasa yenye zana za ufundishaji zikiwemo kompyuta, akisema hali hiyo itachangia wasichana na wanawake kuongezeka kwenye masomo hayo.

Anasema wazazi wamehamasika vizuri sana na watoto wa vijijini wana uelewa wa kutosha, ila mazingira yaliyopo yanachangia wanafunzi kutoyapenda masomo ya sayansi.

 Naye mwalimu na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo anasema ushiriki mdogo wa wanawake na wasichana katika masuala ya sayansi unatokana na fikra tu.

“Ukiangalia katika ubunge, mwanaume hajawekewa viti maalumu lakini kwa mwanamke vipo. Hii inamaanisha ushindani kati ya mwanamke na mwanaume katika mambo magumu sio sahihi. Na hata katika sayansi inaonekana kama ni somo gumu,madaktari bingwa wanawake ni wachache sana, “anasema.

 Anasema ukimkuta msichana aliyechagua masomo ya sayansi anakuwa vizuri kuliko mwanaume, hivyo kinachotakiwa ni kuongeza hamasa kwa wasichana na wanawake katika ushiriki wa sayansi, teknolojia na tehama.

 Mtembo anashauri kuwa kama kuna uwezekano wa kutoa ofa maalum kwa wasichana wanaosoma masomo ya sayansi, hilo lifanyike kwa ajili kuhamasisha ili wengi wakimbilie huko badala ya kuishi na dhana kuwa wanaume pekee ndio wanaofaa kuingia kwenye mambo magumu.

Serikali yataja mambo manne

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete anasema mambo manne yanaweza kusaidia ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi , ikiwemo kuanzisha mifumo rafiki ya kuwapa motisha wanaoshiriki na kufanya vizuri katika sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati.

Anataja mambo mengine ni kuendelea kubuni njia na mikakati ya kuimarisha, kuratibu na ufugamanishaji mipango, programu na juhudi nyingine zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati na nyanja nyingine za kisayansi.

 Jingine ni kufanyika kwa tafiti mahususi zinazolenga kubainisha hali halisi ya idadi ya wanawake na wasichana wanaojiunga kwenye fani hizo katika ngazi mbalimbali za elimu nchini katika kipindi kizichozidi miaka 10.

Ridhwan anataja jambo la nne ni kuanzisha mfumo rafiki wa utoaji wa motisha kwa wanawake na wasichana wanaoshiriki na kufanya vizuri katika sayansi, tafiti na ubunifu.

 Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia elimu msingi,Dk Charles Mahera, anasema Serikali itaendelea kuandaa walimu wazuri wa masomo ya sayansi, kwa lengo la kuwasaidia wanawake na wasichana wapende kusoma masomo hayo.

“Kwa kuzingatia wanawake na wasichana ni asilimia 51.7, tukihakikisha wanasoma masomo haya tutaongeza ubunifu katika teknolojia na katika masomo ya sayansi. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzidi kuwekeza katika elimu pamoja na kujenga shule za wasichana katika mikoa yote Tanzania,”anasema.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917

Related Posts