Jeshi la Polisi Arusha lapigwa jeki pikipiki 20

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameahidi kwamba kabla ya kufikisha siku 100 za uongozi wake mkoani humo, atakuwa ametekeleza ahadi zake ikiwemo kuliwezesha Jeshi la Polisi mkoani humo kupata pikipiki 50, baisikeli 100 zinazotumia umeme  na magari 20.

Amesema ataendelea kukusanya michango kutoka kwa wadau mbalimbali kufanikisha vitendea kazi hivyo na kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakapokwenda mkoani humo, atavikabidhi kwa Jeshi la Polisi vikiwa vimekamilika vyote.

Amesema vitendea kazi hivyo ni kwa ajili ya kuimarisha usalama na kukuza utalii mkoani Arusha, ambapo amekaribisha wadau mbalimbali kuchangia katika suala hilo.

Makonda ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 16, 2024 jijini Arusha wakati akipokea msaada wa pikipiki 20 zenye thamani ya Sh50 milioni kutoka Benki ya CRDB, zitakazosaidai kuimarisha usalama.

Amesema alipokutana na askari mkoani hapa moja ya ahadi alizotoa ilikuwa ni kuwaongezea vitendea kazi ambavyo ni pikipiki 50, baisikeli 100 zinazotumia umeme na magari 20 ili waimarishe ulinzi katika jiji hilo la kitalii.

“Nilipokutana na makamanda wa mkoa wa Arusha, kichwani na moyoni mwangu nilitamani kuwaongezea nyenzo au mara nyingi tunapenda kuwalaumu watu bila kujua mazingira ya utendaji wao au rasilimali walizonazo, changamoto wanazopitia zinafanya wasifanikishe dhamira na nia njema waliyonayo,” amesema.

“Niliwaahidi kama kiongozi nakuwa champion wa kutafuta vitendea kazi ili tuwe na kila sababu ya kuanza kunyooshea mikono polisi kwamba tumewawezesha na tumewalipa mishahara kwa nini uhalifu unaendelea kuwepo,” amefafanua.

“Nashukuru CRDB mmekuwa wa kwanza kunijengea heshima ya safari niliyoahidi kwa makamanda wetu, haitakwenda zaidi ya miezi mitatu kwani nimelenga siku 100 zangu hapa niwe nimeshamalizana na kila ahadi niliyotoa kwenu, kabla ya siku hizo nitakuwa nimekamilisha,” ameongeza Makonda.

Amesema watahakikisha vitendo vya kihalifu ikiwemo biashara ya dawa za kulevya, uporaji na nyingine zinakoma ili kulinda usalama uliopo.

“Naomba kuwasihi wale wachache wanaojihusisha na uovu na biashara haramu iwe ya kupora au dawa za kulevya, niwasihi kwa unyenyekevu mkubwa tuachane nazo kwani polisi hawatakubali kufedheheshwa na kupoteza heshima zao,” ameongeza.

Makonda ameongeza kuwa mji wa Arusha unaendelea kufungwa taa na kamera na kuwa siku zinavyozidi kwenda itafika hatua mtu akiingia Arusha kutoka eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuelekea Mjini au akitoka uwanja wa mdogo wa ndege wa Kisongo kuelekea Mjini anaonekana ili kudhibiti uhalifu.

“Hatutaki Arusha iwe ya kisiasa bali tunataka uwe mkoa wa kiuchumi na tutaangalia mfano kwa wazawa wengi wanaolima mazao mbalimbali tutaangalia namna ya kuwawezesha ili wasafirishe nje ya nchi yakiwa yameongezwa thamani,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kutokana na Arusha kuwa mji wa kitalii, lengo lao kutoa pikipiki hizo ni kuimarisha usalama na kukuza utalii ili mtalii anapokuja awe salama.

Amesema utalii ni sekta muhimu nchini katika kukuza uchumi na kuwa wanaamini msaada huo utaongeza chachu ya kuunga mkono jitihada za mkoa na taifa kwa ujumla katika kusimamia usalama.

“Pikipiki hizi zitasaidia kuimarisha usalama katika mkoa wetu wa Arusha na huu siyo mwisho. Hata katika ile kampeni ya usafi wa mkoa, mtatuambia ni wapi mnataka kuweka dustbin na sisi tutatoa mchango na kushiriki katika hilo,” amesema.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo ameshukuru kwa msaada huo na kuwa utawasaidia katika kuimarisha usalama na hawatasita kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu.

“Hii si mara ya kwanza, mwaka jana walitupa pikipiki 15, na sisi kama polisi zitatusaidia kuimarisha usalama na tutazitumia vema kama nyenzo kuhakikisha usalama wa mkoa unaimarika na wale wachache ambao bado wanajihusisha na uhalifu tutachukua hatua kali dhidi yao,” amesema kamanda huyo.

Related Posts