Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imekiri kukabiliwa na changamoto zinazohitaji mtazamo wa sekta mtambuka za mazingira, uchumi, teknolojia na utawala wa kimataifa.
Waziri wa wizara hiyo, Shaaban Ali Othman amesema hayo leo Jumanne Februari 18, 2025 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Katika swali, mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir amesema fursa za uchumi wa buluu zilizopo nchini bado hazijatumika ipasavyo kutokana na changamoto mtambuka ambazo ni vigumu kutatuliwa na sekta moja.
Kutokana na hali hiyo, amehoji mtazamo na mipango mkakati ya Serikali kuhusu mtazamo huo.
Akijibu swali hilo, Waziri Shaaban amekiri kuwapo changamoto kadhaa na ili kuzitatua, ushirikiano wa sekta mbalimbali, mikakati madhubuti na teknolojia bunifu zinahitajika.
“Ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya uchumi wa buluu inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji mtazamo wa sekta mtambuka ili kuzitatua, ushirikiano wa sekta mbalimbali, mikakati madhubuti na teknolojia zinahitajika,” amesema.
Waziri amesema sekta ya uchumi wa buluu inahitaji uwekezaji mkubwa katika bandari, viwanda vya samaki, nishati mbadala na utafiti wa baharini.
Ameeleza wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji binafsi kupitia sera za kifedha zinazovutia wawekezaji, ikiwamo mikopo nafuu, motisha za kodi na kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) katika kuendeleza miundombinu, bandari, viwanda vya kuchakata samaki na nishati ya baharini.
Amesema wizara itaendelea kusimamia mfumo wa kisheria ulio imara kwa lengo la kulinda wawekezaji na kuondoa hatari ya kupoteza mitaji yao.