600 wafanyiwa upasuaji mtoto wa jicho

Unguja. Wagonjwa 15,115 wamepatiwa matibabu katika Hospitali ya Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), kati ya hao 600 wamefanyiwa upasuaji wa macho, ikiwamo utoaji wa mtoto wa jicho.

Matibabu hayo yalifanyika katika kambi ya wiki moja iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Dk Hussein Khamis Othman, amesema hayo leo Jumanne Februari 18, 2025 aliposoma risala ya hospitali hiyo katika ufunguzi wa kambi ya uchunguzi wa macho awamu ya pili inayoendeshwa na madaktari kutoka Taasisi ya Vision for Puma ya nchini Ujerumani.

“Katika awamu ya kwanza ya kambi hii jumla ya wagonjwa 15,115 wamepatiwa matibabu mbalimbali kati yao wagonjwa 600 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, hivi sasa kambi hii ni awamu ya pili,” amesema.

Wananchi mbalimbali waliofika katika kambi ya uchunguzi wa macho kwa awamu ya pili katika Hospitali ya Kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar(KMKM) iliyopo Kibweni,Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya, Dk Amour Suleiman Mohamed amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya imejipanga kuandaa mikakati ya utoaji elimu na huduma za matibabu ya macho mara kwa mara ili kupunguza matatizo hayo.

Amesema miongoni mwa sababu inayochangia matatizo ya macho ni mtoto wa jicho.

Amesema takwimu zinaonyesha jumla ya wagonjwa 14,500 wanasumbuliwa na matatizo ya macho katika hospitali mbalimbali, kati yao wagonjwa 9,000 wanasumbuliwa na mtoto wa jicho.

Amesema Wizara ya Afya imejipanga kufanya uchunguzi wa macho kugundua matatizo hayo mapema, kutoa elimu na matibabu kwa wananchi ili kuwasaidia kuanza matibabu mapema.

Amesema kwa kubaini ugonjwa wa macho ni tatizo, Wizara ya Afya imeandaa utaratibu wa kuwafundisha madaktari bingwa wa matatizo ya macho kila mwaka ili kuwa na idadi yao ya kutosha kuwahudumia wananchi.

“Natoa wito kwa madaktari wa kambi hii kuangalia uwezekano wa kuweka kambi za nje ya hospitali ili kutoa nafasi ya kuwafikia wananchi wengi watakaonufaika na vipimo hivi,” amesema.

Mkuu wa Kikosi cha KMKM, Azana Hassan Msingiri amesema kambi hiyo ipo kwa awamu ya pili sasa katika hospitali hiyo inayowapa unafuu wananchi kupata vipimo vya macho.

Amesema katika kambi hiyo wananchi hupatiwa vipimo na matibabu bure, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali za kutoa huduma za matibabu bure.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Vision for Puma, Dk Frank Klenmn amesema kwa kushirikiana na timu yake yenye zaidi ya madaktari bingwa watano wamejipanga kuhudumia wananchi wengi katika kambi hiyo.

Amesema wagonjwa wengi waliofika katika kambi hiyo wanasumbuliwa na mtoto wa jicho, hivyo ameshauri wananchi kuwa na tabia ya kupima afya kwa lengo la kupatiwa matibabu mapema.

Related Posts