Moshi. Chama cha Sauti ya Umma (Sau), kimetangaza mchakato wa uchaguzi kwa ajili ya kupata viongozi wa chama hicho ngazi ya Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, huku kikiwataka wananchi na wanachama wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Nafasi zinazowaniwa ni pamoja na mwenyekiti wa chama hicho wilaya, makamu mwenyekiti, katibu, katibu msaidizi, mwenezi, mweka hazina na viongozi wa vitengo vya wanawake, vijana na wajumbe wa ngazi ya mkoa.
Akizungumza leo Jumanne, Februari 18,2025, Kaimu Katibu wa Sau Jimbo la Moshi Mjini, Mohamed Shemvaa amesema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umeanza Februari 13 na utakamilika Februari 22 na uchaguzi utafanyika Februari 28, mwaka huu.
Aidha, amesema mpaka leo Februari 18, watano kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali huku akisisitiza kuwa uchaguzi wao utazingatia demokrasia na utafuata taratibu na sheria za uchaguzi za chama hicho.
“Tutaufanya uchaguzi huu kuwa wa kidemokrasia zaidi, kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi kwa watia nia wote, na kwenye mkutano huo watakaoingia ni wale wanachama hai, waliolipa ada zao za uanachama”amesema Shemvaa
Aidha amesema maandalizi hayo ni kwa ajili ya kuunda timu ya ushindi ikiwemo bafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani.
“Lengo la chama chochote kile cha kisiasa ni kushika dola hivyo basi katika weledi wetu tunahakikisha kwamba tunakwenda kupata viongozi bora wa kukivusha chama chetu,” amesema.
Amesema baada kumalizika chaguzi za Wilaya, wataanza mchakato wa uchaguzi wa Mkoa ili kupata viongozi wa Mkoa huo watakao saidia chama wakati wa uchaguzi.
“Baada ya kumaliza chaguzi hizi za wilaya na Mkoa, tutaanza hamasa ya kutafuta wanachama wapya ili utakapofika wakati wa uchaguzi, tuweze kuwa katika nafasi nzuri ya ushindi,” amesema Shemvaa.
Mwenyekiti wa Sau, Mkoa wa Kilimanjaro, Isack Kireti amewataka wanachama wote wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu, ili kushirikiana kukijenga chama hicho na kukivusha katika uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, baadae mwaka huu.
Amesema utaratibu umepangwa kwa ajili ya kuhakikisha wale wote watakaochukua fomu kushiriki uchaguzi wamekidhi vigezo.
“Baada ya utaratibu wa kuchukua fomu kukamilika, wale wote waliojitokeza watachujwa na kufanyiwa usaili na hatimaye kuingia kwenye uchaguzi, na tutahakikisha wale wote watakaokidhi vigezo wanapata fursa ya kushiriki uchaguzi” amesema Kireti.