Fukuto lazidi Chadema, mchakato kuwaidhinisha kina Mnyika na Lema wapingwa

Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana kuendelea kwa mivutano ya makundi ndani ya Chadema, kada mmoja wa chama hicho, amepinga uteuzi wa viongozi watendaji wa juu wa sekretarieti na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho uliofanwa na Mwenyekiti Tundu Lissu Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.

Mmoja wa makada wa chama hicho, Lembrus Mchome amewasilisha pingamizi hilo kwa barua kwenda ofisi ya katibu mkuu leo, Jumanne Februari 18, 2025 akibainisha uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha Baraza Kuu kutimia.

Kwa mujibu wa Mchome vigogo waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (naibu katibu mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (naibu katibu mkuu – Zanzibar).

Mchombe katika barua hiyo ambayo Mwananchi limeiona, anawataka wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho kuwa ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala.

Kwenye kikao hicho cha Baraza Kuu kilichofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam Januari 22, 2025, Lissu aliwasilisha majina ya wateule hao kisha wakaidhinishwa na wajumbe wa baraza hilo kwa kunyoosha mikono.

Mwananchi ilipomtafuta Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuzungumzia uteuzi huo, amesema kwa nafasi yake hana mamlaka ya kupokea malalamiko, badala yake aulizwe katibu mkuu mwenye mamlaka hiyo.

“Nafikiri itakuwa vyema mtafute mtu aliyeandikiwa barua,” amesema Lissu aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa chama hicho.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Mnyika kupitia simu yake hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Golugwa amekiri barua hiyo kufika ofisini hapo, ingawa amesema bado hawajaisoma kujua kilichomo ndani yake.

Golugwa aliyewahi kuwa katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini), amesema alikuwa kwenye shughuli fulani za chama, na alipofika tu ofisini, maofisa wa mapokezi wamemtaarifu kuhusu kuwepo kwa barua hiyo.

“Mimi na viongozi wenzangu bado hatujaisoma hiyo barua kujua kilichomo ndani, lakini tutaisoma na tukijua maudhui yake ndipo tunaweza kusema chochote,” amesema.

Mchome kwenye barua hiyo iliyonakiliwa kwa msajili wa Vyama vya Siasa, amesema ili akidi ya kikao kilichowaidhinisha vigogo hao kamilike, kilipaswa kuwa na wajumbe 309, badala ya 85 waliokuwepo ambao ni sawa asilimia 20.6.

Mchome, mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, amesema kwa mujibu wa katiba ya Chadema tolea la mwaka 2019 jumla ya wajumbe wa Baraza Kuu ni 412 na ili kikao kiwe halali na kufanya uamuzi kinatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua 309.

“Kikao cha Januari 22, 2025 kilikuwa na wajumbe 85, sawa na asilimia 20.6 ambao ndiyo wajumbe halali na ndio waliofanya uamuzi wa kuthibitishwa kwa wateuliwe hao kinyume cha katiba na kanuni za chama ibara 6.2.2 (a) na (b) ya katiba ya chama mwaka 2006 toleo la 2019.

“Ukumbini kulikuwa na jumla ya watu 236, wakiwemo wajumbe halali 85 na wasio halali 151, ambapo baadhi yao wameonekana katika picha za video jongefu wakipiga kura za kufanya uamuzi wa kuwathibitisha viongozi wa chama na wajumbe wa sekretarieti,” amedai Mchome.

Mchome ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga Mwanga mkoani Kilimanjaro na Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa, anadai kwa hali hiyo ni uthibitisho kwamba viongozi wa kitaifa na wajumbe wa kamati kuu watano waliopendekezwa na mwenyekiti wa Chadema na kuthibitishwa ni batili.

Kutokana na hilo, kada huyo ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu amesema viongozi wote waliothibitishwa kinyume cha utaratibu watangazwe kuwa batili, wasitumikie nafasi zao hadi uthibitishaji halali utakapofanyika.

Mchome ameongeza kuwa uamuzi wote uliofanywa na kamati kuu ambayo wajumbe hao wameshiriki ubatilishwe na Baraza Kuu liitishwe tena kufanya upya mchakato utakaohakikisha akidi inatimia.

“Hatuna malalamiko na walioteuliwa, ni watu sahihi, wengine tumeshawahi kufanya nao kazi kwa ukaribu, lakini tunahitaji wapite katika njia sahihi. Tunataka Baraza Kuu lijalo liwe na akidi ya asilimia 75 au zaidi ili kuwathibitisha kuwa wajumbe halali.

“Narudia, hatuna mashaka na walioteuliwa ni watu wazuri, lakini kwa sababu Chadema inasimamia katika misingi ya katiba, basi tuisimamie na kuilinda katiba yetu, ili kupata wajumbe halali. Naamini demokrasia itafuatwa katika hili,” amesema Mchome.

Related Posts