JKT Tanzania yapata ushindi, KenGold yatakata

Ushindi wa mabao 2-0 ambao wameupata JKT Tanzania, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC umewafanya Maafande hao kupanda nafasi sita kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku KenGold ikiendeleza moto.

Awali JKT ambao hawakuonja ushindi katika michezo minane iliyopita sawa na dakika 720, walikuwa nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 20 sawa na Mashujaa ya Kigoma.

Katika dakika 720 za michezo minane iliyopita, JKT imetoa suluhu nne dhidi ya Pamba, Mashujaa, Namungo na Yanga huku wakipoteza pia minne dhidi ya Simba (1-0), Azam (3-1), Coastal Union (2-1) na Singida Black Stars kwa bao 1-0.

Hivyo bao la Hassan Nassoro Maulid dakika ya 10, alilofunga kwa kichwa kufuatia faulo iliyochongwa na Najim Magulu na lile la kujifunga la Wilbol Maseke dakika ya 68 yamewafanya vijana hao wa Ahmed Ally kusogea hadi nafasi ya sita ikifikisha pointi 23 ikiwa na michezo 20.

KMC walijikuta pungufu kufuatia  kipa wao Ismail Mpank kuonyeshwa kadi nyekundu na hivyo timu hiyo kumaliza na wachezaji pungufu.

Matokeo hayo yameifanya KMC kushuka kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya nane hadi tisa.
Kwa upande wa KenGold ikiwa nyumbani imeendelea kufanya maajabu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Bao pekee la KenGold liliwekwa kimiani na Mishamo Daudi katika dakika ya 82 ya mchezo akimalizia pasi ya Seleman Bwenzi.
Hata hivyo KenGold imeendelea kubaki mkiani baada ya kufikisha pointi 13 mbili nyuma ya Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 15 kwenye msimamo.

Related Posts