Pacha waliotenganishwa waruhusiwa kuondoka Muhimbili

Dar es Salaam. Pacha waliotenganishwa nchini Saudi Arabia, Hussein na Hassan Amir (3), wameruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakitarajiwa kurejea Igunga, mkoani Tabora kesho, Februari 19, 2025, baada ya kupata eneo la kuishi.

Watakwenda kuishi kwenye nyumba iliyotafutwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora, wakati wakisubiri nyumba inayojengwa kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumanne, Februari 18, 2025 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila, Dk Julieth Magandi, amesema watoto hao wanaruhusiwa baada ya matibabu ya miaka mitatu na miezi mitano.

“Leo tunawaruhusu na kuwarudisha nyumbani watoto wetu. Walifikishwa Muhimbili mwaka 2021 wakiwa na wiki mbili tangu kuzaliwa wakitokea Igunga, Tabora. Tulikaa nao kwa miaka miwili kwa sababu tulikuwa tunawajenga afya zao kama maandalizi ya upasuaji mkubwa kwani waliungana sehemu kubwa ya mwili,” amesema.

Amesema ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora inakwenda kusimamia maisha ya watoto hao na imeshatafuta nyumba ya kuishi kwa mwaka mmoja.

 “Watakwenda kuishi Igunga mjiini. Hospitali imendaa usafiri wa ambulensi itawatoa hapa kwenda Igunga,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezipata, watoto hao wameanza kujengewa nyumba mjini Igunga na msamaria mwema ambaye hajataka kutajwa jina.

Alipoulizwa kuhusu watoto hao kurejeshwa Saudi Arabia mwishoni mwa mwaka huu kwa matibabu, Dk Magandi amesema madaktari bingwa wataifahamisha hospitali muda ukifika na watawasiliana na mama yao.

Dk Magandi ametoa shukrani kwa Hospitali ya Saudi Arabia na serikali ya nchi hiyo iliyowezesha upasuaji wa saa 16 wa kuwatenganisha watoto hao. Walikaa nchini humo mwaka mzima wakipatiwa matibabu na tangu waliporejea nchini Desemba mwaka jana, walikuwa chini ya uangalizi wa MNH.

Mama wa pacha hao, Hadija Hassan (25), ambaye ataambatana na daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa watoto, Zaituni Bokhari, ameishukuru hospitali, uongozi wa Saudi Arabia, na wataalamu wote wa afya waliosaidia tangu kuzaliwa kwa watoto hao.

“Nashukuru watu wote kwa kuwa pamoja nami, wamenipokea tangu mwaka 2021 mpaka leo naruhusiwa. Napenda kuwashukuru kwa msaada mlionipatia; ni mkubwa,” amesema.

Dk Zaituni amesema wakati watoto hao wanaruhusiwa, ni muhimu kuendelea kufanya tiba mazoezi, hivyo watakwenda kutoa maelekezo kwa hospitali watakayokuwa wanaangaliwa.

 “Wanarejea kwenda nyumbani. Kama daktari mwenye dhamana, kuna umuhimu wa kupata taarifa kamili za matibabu yao yamekwenda vipi. Hivyo, lazima tuzungumze na madaktari watakaokuwa wanawaangalia. Waendelee kuwachezesha viungo ili mguu mmoja walio nao uwe na nguvu. Bado wana safari ya kuendelea mpaka watakapokamilika,” amesema.

Dk Zaituni amesema upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao ulifanyika kwa saa 16 Oktoba mwaka 2023.

“Upasuaji ulihusisha wataalamu wa mifupa, moyo, kibofu cha mkojo, na mishipa ya damu. Kibofu cha watoto hawa kiliungana. Walikuwa na miguu mitatu, ila mmoja haukuwa unafanya kazi, hivyo huo umetumika kutengeneza maeneo mengine,” amesema.

Amesema watoto hao wamekaa nchini humo kwa mwaka mmoja na miezi minane na matibabu waliyapata katika Hospitali ya King Abdullah bin Abdulaziz ya nchini Saudi Arabia.

Related Posts