Hakimu agoma kujitoa kesi za uchaguzi anazozisikiliza

Kigoma. Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Ana Kahungu ametupilia mbali pingamizi na hoja za mawakili wa Serikali kuhusu uhalali wa kuendelea kusikiliza mashauri mawili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024.

Akizungumza leo Jumanne Februari 18, 2025 kuhusu mawakili hao kutaka ajitoe katika shauri hilo, hakimu Kahungu amesema uandishi wa hukumu ni mchakato na anachokiona katika hoja za tuhuma zao dhidi yake ni hisia tu, hivyo hawezi kujitoa.

Awali, mawakili hao walimkataa hakimu huyo wakimtaka ajitoe katika kesi hizo zilizofunguliwa na wanachama wawili  tofauti wa ACT- Wazalendo, Didas Baoleche na Khalfan Nyunya.

Baoleche aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi, kata za Kibirizi na Nyunya, aligombea nafasi hiyo katika Mtaa wa Busomero Kata ya Kasimbu, zote katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Wanachama hao walifungua mashauri hayo dhidi ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliotangazwa washindi ambao ni Mrisho Mwamba (Mtaa wa Kibirizi), Hassan Asanary ( Busomero), wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ngazi ya mitaa hiyo na msimamizi wa uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).

Wote wanapinga mchakato wa uchaguzi na uchaguzi wenyewe pamoja na  matokeo yaliyotangazwa kuwa haukuwa huru na wa haki.

Wanadai kuwa, uchaguzi huo ulikiuka kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi, kutokana na matokezo kutotangazwa, kubandikwa na kukamatwa kwa kura bandia.

Wakati mashauri hayo yote yakiendelea kusikilizwa na hakimu Kahungu, mawakili wa Serikali waliibua pingamizi dhidi ya hakimu huyo wakimuomba ajitoe kusikiliza mashauri hayo.

Mawakili  hao kwa niaba ya wajibu maombi wa pili na wa tatu, waliwasilisha tuhuma hizo baada ya uamuzi wa mapingamizi waliyokuwa wamewasilisha wakitaka yatupiliwe mbali bila kusikilizwa madai ya msingi, kwa hoja kwamba yana kasoro za kisheria.

Hakimu Kahungu katika uamuzi wake leo Jumanne Februari 18, 2025 amekataa mapingamizi hayo ya Serikali na kuruhusu mashauri kuendelea kusikilizwa kwa mujibu wa madai ya msingi, baada ya kubaini kuwa mapingamizi hayo hayakuwa na misingi thabiti ya kisheria.

Baada ya uamuzi huo, mawakili hao wa Serikali waliwasilisha pingamizi dhidi ya hakimu, wakimtaka ajiondoe kusikiliza mashauri hayo kwa madai ya upendeleo kwa mwombaji.

Katika hoja zao, wamedai wakati wa usikilizwaji wa mapingamizi yao dhidi ya mashauri hayo, waliibua hoja ambazo hazikuonyeshwa kwenye uamuzi wa hakimu.

Hata hivyo, Wakili wa ACT-Wazalendo, Prosper Maghaibuni amepinga madai hayo ya mawakili wa Serikali, akieleza uamuzi huo ni sahihi na madai ya kuachwa kwa baadhi ya hoja yanapaswa kuthibitishwa.

Amebainisha kuwa, maelezo yaliyotolewa kwenye uamuzi ni uchambuzi wa hoja zilizojitokeza kwenye mwenendo wa kesi, si kwamba yalichukuliwa moja kwa moja kama yalivyowasilishwa.

Wakili Maghaibuni amesisitiza kuwa, maelezo katika uamuzi wa pingamizi hilo ni sahihi na halisi na hakuna uthibitisho wa madai kwamba, maneno yaliongezwa au kuachwa.

Wakili Maghaibuni  wa ACT- Wazalendo,  ameeleza kuwa tuhuma za upendeleo dhidi ya hakimu ni nzito.

Akirejelea kanuni na msimamo wa Mahakama Kuu katika kesi mbalimbali, Wakili Maghaibuni amefafanua kuwa ili hakimu au jaji ajiondoe kwenye kesi, lazima kuwe na sababu kubwa na siyo kwa misingi ya hisia pekee.

Ameonya kuwa, ikiwa hisia kama hizo zitaruhusiwa, basi kila mtu mwenye malalamiko binafsi dhidi ya hakimu,  anaweza kuibua hoja ya kumkataa, jambo ambalo si sahihi.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Abdallah Makulilo amesisitiza kuwa wanatambua uzito wa tuhuma hizo, ndio sababu wanamwomba hakimu ajitoe, kwa kuwa hazitaathiri tu pande zinazohusika, bali pia hadhi ya Mahakama.

Hakimu Kahungu  katika uamuzi wake, ametupilia mbali mapingamizi hayo katika mashauri yote mawili, akianza na uamuzi wa shauri la Baoleche jana na kumalizia na uamuzi wa shauri la Nyunya leo, Jumanne, Februari 18, 2025.

Katika uamuzi wa shauri la Nyunya, hakimu Kahungu amesema baada ya kupitia hoja za pande zote, amebaini kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake ni nzito, zina lengo la kumkatisha tamaa ili ajitoe kwenye shauri hilo.

Amesema kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Maofisa wa Mahakama anayelalamikiwa, anatakiwa kujitoa kwenye kesi pale anapoona kuwa hawezi kuwa huru na kwamba kuna sababu za msingi.

Amebainisha kuwa, sababu hizo ni pamoja na kuwa na mgogoro wa masilahi kati yake na wadaawa au masilahi binafsi na  mazingira yanayoweza kuingilia utoaji haki.

“Kwangu tuhuma hizi ni kubwa zinawahitaji kuthibitisha tuhuma hizi kama kwa nia ovu niliharibu mwenendo na kuthibitisha upendeleo huo,” amesema hakimu Kahungu.

Amesema madai kuwa hoja zao hazikujumuishwa kwenye uamuzi wa pingamizi hilo si sahihi.

Hakimu Kahungu amesema anaona kila kitu kimejumuishwa, hivyo wao hilo wamelitafasiri vipi.

“Hivyo kwa maneno machache, malalamiko haya hayana uthibitisho, kwa maana ya kesi nilizorejea naona maelezo haya (tuhuma za mawakili)  hayaniridhishi mimi kujitoa maana hayakidhi maelekezo ya mambo ambayo yakitokea hakimu au jaji anaweza kujitoa,” amesema hakimu Kahungu.

Amesema uandishi wa hukumu ni mchakato na kusisitiza anachokiona katika hoja za tuhuma zao ni hisia tu, hivyo hawezi kujitoa kwa hoja za hisia.

Hakimu Kahungu  amesema kwa mazingira ya shauri hilo na kesi mbalimbali zilizotolewa na mawakili na alizozirejea, anaona tuhuma za mawakili hao dhidi yake hazina mashiko zinakusudia kumkatisha tamaa.

“Hivyo natupilia mbali pingamizi hili,”, amehitimisha hakimu Kahungu  na akapanga kuendelea na usikilizwaji wa mashauri hayo.

Jana, baada ya kumaliza uamuzi kwenye shauri la Baoleche, Wakili wa Serikali Pantaleo Urasa aliieleza Mahakama kuwa wanakusudia kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Alisema ameiomba Mahakama isimamishe kwanza mwenendo wa shauri hilo kusubiri uamuzi wa rufaa wanayokusudia kuikata.

Hata hivyo, hakimu Kahungu ametupilia mbali hoja na maombi hayo akisema hawezi kusimamisha, kwa sababu maelezo kuwa wanakusudia kukata rufaa,  hayatoshi kumfanya asimamishe usikilizwaji wa kesi hiyo.

Amesema ataendelea na usikilizwaji wa shauri hilo mpaka Mahakama Kuu itakapotoa maelekezo mengine.

Leo, hakimu Kahungu ameendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa shauri la Baoleche huku akipanga kuendelea kesi ya  Nyunya, Februari 20, 2025.

Mashauri haya ni kati ya 51  yaliyofunguliwa na  ACT- Wazalendo nchini katika Mahakama za wilaya mbalimbali zikiwamo za Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti, kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi huo.

Katika Mkoa wa Kigoma, chama hicho  kimefungua mashauri 13, huku  Manispaa ya Kigoma Ujiji yakiwa tisa.

Mashauri hayo yote yako katika hatua ya usikilizwaji wa hoja za msingi kwa mahakimu tofauti tofauti baada ya kuvuka kikwazo cha mapingamizi yaliyoibuliwa na mawakili wa Serikali, isipokuwa matatu tu yaliyoondolewa na ambayo yako kwenye mchakato kufunguliwa upya.

Related Posts