Aliyemchinja mtoto, kutenganisha kichwa na kiwiliwili kunyongwa hadi kufa

Babati. Mahakama Kuu masjala ndogo ya Babati, mkoani Manyara imemhukumu adhabu ya kifo, Paskal Saqware, baada ya kupatikana na hatia ya kumchinja mtoto aliyekuwa akisoma shule ya awali (chekechea) na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Katika hukumu, Jaji Frank Mirindo amesema ushahidi wa uwepo wa nia ovu ni mzito kwa kuwa mtoto huyo alichinjwa, damu kuzagaa kwenye majani na mimea ya maua katika korongo na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili.

Jaji Mirindo amesema matendo aliyofanya mshitakiwa yanathibitisha uwepo wa dhamira ovu yenye nia ya kusababisha kifo chini ya kifungu 200 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Hukumu imetolewa Februari 17, 2025 na nakala kupakiwa leo Februari 18 katika mtandao wa Mahakama wa TanzLll ambao huchapisha maamuzi, sheria na kanuni za Tanzania.

Februari 20, 2024, kundi la watoto wanaosoma darasa la awali walikuwa wakirejea nyumbani. Njiani walikutana na mtu aliyeshika panga katika daraja la Kinyume lililopo kwenye shamba la miwa la Odedra katika Kijiji cha Mapea, Babati.

Mtu huyo aliwataka watoto wamfuate ili akawachumie matunda ya mtende. Watoto wengine walikimbia mmoja alimfuata, akambeba mgongoni na kuondoka naye.

Watoto waliokimbia walikwenda kuwasimulia wazazi wao, hivyo kundi la wanakijiji lilikusanyika na kuanza kumtafuta mtoto huyo.

Kundi hilo lililokwenda uelekeo wa korongo kando mwa shamba la miwa la Odedra, liliona michirizi ya damu na mwili wa marehemu ndani ya maji korongoni.

Jirani na korongo hilo walikuta fulana ya bluu yenye mistari myeupe na jozi ya makobasi ya rangi ya kijani.

Taarifa ilifikishwa Kituo cha Polisi Magugu, hivyo askari walifika kukagua eneo, kisha kuopoa mwili majini.

Kichwa hakikuwepo. Polisi kwa kushirikiana na wanakijiji waliendelea kukitafuta na kilionekana umbali wa kama hatua tatu kutoka mahali mwili ulipokuwepo. Askari waliondoka na mwili na vitu vya marehemu.

Siku iliyofuata, Februari 21, 2024 mtu mmoja alionekana akichungulia na kujificha kwenye shamba la miwa karibu na korongo ambako mwili wa marehemu ulipatikana. Alikamatwa na wananchi na kukabidhiwa kwa polisi.

Mtu huyo alitambuliwa baadaye kuwa Paskal Saqware aliyeshtakiwa kwa kosa la mauaji ya mtoto huyo ambaye mahakama iliamua kuhifadhi jina lake.

Katika usikilizwaji wa kesi mshtakiwa alitetewa na wakili Kuwengwa Ndonjekwa.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na jopo la mawakili watatu, Rose Kayumbo, Bernadetha Mosha na Jackson Mayeka, ulikuwa na jukumu la kuishawishi mahakama kuwa ushahidi wao hauachi shaka kuwa mhusika wa mauaji ni Paskal.

Katika hukumu, jaji amesema hakuna mashaka kuwa mtoto huyo aliuawa kinyume cha sheria kwa kuwa ushahidi wa mashahidi watatu waliokwenda eneo la tukio waliona damu na kichwa kimetenganishwa na kiwiliwili ndani ya korongo.

Jaji amesema ushahidi wa baba mzazi wa mtoto huyo, Petro Muhozi alieleza katika korongo walishuhudia damu kwenye majani na majani ya matunda ya ndelule, ushahidi ambao uliungwa mkono na kachero wa polisi, Sajenti Masanja.

Kachero huyo alieleza namna walivyokuta damu kwenye majani na mwili wa mtoto ukiwa hauna kichwa ambao waliutoa na baadaye walipata kichwa kwenye korongo.

Uchunguzi wa mwili ulibaini alichinjwa na kitu chenye ncha kali.

Kulingana na ushahidi, jaji amesema Februari 28, 2024 shahidi wa sita, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Chisano Bigolame, alimchukua mshitakiwa na kumpeleka Hospitali ya Babati Mjini ambako alichukuliwa sampuli za damu kwa ajili ya DNA.

Machi 7, 2024, Konstebo wa Polisi Amos Ramadhan, alikabidhi sampuli hizo kwa Ally Kinanda wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Jaji amesema kifungu cha 33(1) cha Sheria ya DNA ya mwanadamu, inataka ofisa anayechukua sampuli, kuhakikisha zinasafirishwa kwa njia sahihi na salama, lakini hakuna ushahidi kuonyesha shahidi wa 11 aliidhinishwa kuzisafirisha.

“Usimamizi sahihi wa sampuli za DNA ni muhimu kuhakikisha uadilifu wa sampuli zinazowasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi wa kimaabara. Lakini kutokana na dosari hizi sina sababu ya kukipa uzito kielelezo cha DNA,” amesema.

Jaji amesema ukiacha ushahidi wa DNA, ushahidi wa mazingira wa kutambuliwa unaonyesha yeye ni mtu wa mwisho kuwa na marehemu akiwa hai na kisheria ndiye anawajibika isipokuwa tu kama atatoa maelezo ya kutosha.

“Kitendo cha mshtakiwa kushindwa kutoa maelezo ya kutosheleza inafanya aingie kwenye muunganiko wa mnyororo wa ushahidi wa mazingira dhidi yake,” amesema akirejea misimamo iliyotolewa na mahakama katika kesi mbalimbali.

Katika kuiga kanuni hiyo, katika kesi ya mauaji ya mtoto huyo, hoja ya msingi ya kuitafutia majibu ni kama kuna ushahidi unaoonyesha mshitakiwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu kabla ya mwili wake kupatikana amekufa.

Jaji amesema shahidi muhimu wa Jamhuri aliyemtambua mshitakiwa kuwa ndiye mtu wa mwisho kuwa na marehemu ni mtoto aliyekuwa na marehemu aliyepewa jina GR mwenye umri wa miaka saba, aliyetoa ushahidi kama shahidi wa 10.

Aliiambia mahakama wakati anarudi kutoka shule na watoto wengine walikutana na mtu aliyebeba panga ambaye aliwaambia wamfuate ili awachumie matunda.

Alieleza walikutana naye katika daraja la Kinyume kwenye shamba la miwa la Odedra.

Mtu huyo aliwataka akawachumie matunda, wao wakarudi nyumbani na alipofika nyumbani alimwelezea mama yake namna walivyokutana na mtu huyo na akataka kwenda kuwachumia matunda wao walikataa ila marehemu alikwenda naye.

Mtoto huyo akaeleza kwa wakati huo akitoa ushahidi hafamu mwenzao yuko wapi na kwa namna alivyotoa ushahidi wake akieleza kuwa alikuwa amevaa kaptura imepunguzwa na shati iliyopunguzwa, ushahidi wake ni wa kuaminika.

Ushahidi wake unaungwa mkono na ushahidi wa mashahidi wengine wa Jamhuri akiwamo mama wa marehemu aliyesema mtoto wake alivyotoka nyumbani kwenda shule alivaa sare za shule na ndizo zilizokutwa jirani na mwili wake.

Mbali na hilo, mshitakiwa alitambuliwa katika gwaride la utambulisho lililofanyika Februari 22, 2024 katika kituo cha polisi Babati na alitambuliwa na watoto wawili ambao walikuwa na marehemu. Katika maswali ya dodoso alikiri kutambuliwa.

GR ambaye alikuwa shahidi wa saba wa Jamhuri aliweza pia kumtambua mshitakiwa katika kizimba cha mahakama alipoulizwa kama yule mtu aliyemuona akiwa na marehemu yupo, alienda na kumuonyesha kwa kidole.

Katika utetezi, mshtakiwa alijitetea kuwa alikuwa ni mwizi wa miwa na alipita katika eneo la tukio saa nne asubuhi.

Alieleza alikuwa ndani ya shamba la miwa ili kuiba na wakati akikamatwa alikuwa akila miwa.

Jaji amesema maelezo hayo yanathibitisha kuwa hakuna ubishi mshitakiwa alikuwepo kwenye shamba la miwa wakati anakamatwa lakini alipotakiwa kueleza siku moja kabla ya kukamatwa alikuwa wapi, hakuwa na majibu.

“Ni wazi kuwa Februari 20, 2024 mshitakiwa akiwa na panga, alitembea kutoka Gichameda kwenda Magugu na kupitia njia ya Odedra, akamchukua marehemu na kuondoka naye kuelekea kwenye korongo lililopo shamba la miwa.

“Siku inayofuata kiwiliwili na kichwa cha mtoto huyo vinapatikana kwenye korongo karibu na shamba la miwa na wanavijiji wanamuona mshitakiwa amejificha kwenye shamba la miwa na kumkamata,” amesema Jaji Mirindo.

Amesema kwa ushahidi huo na mwingine, unajenga uzito wa kesi ukimnyooshea kidole mshitakiwa na si mtu mwingine kuwa ndiye aliyefanya mauaji hayo, hivyo naye atanyongwa hadi kufa.

Related Posts