Lindi yaeleza inavyopambana na migogoro ya ardhi

Ruangwa. Wakati kero ya migogoro ya ardhi ikiendelea kusumbua maeneo mbalimbali nchini, Mkoa wa Lindi umeeleza namna unavyopambana nayo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 18, 2025 na Kaimu Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Lindi, Raimon Chobi katika kikao cha mafunzo ya wataalamu watakaoshiriki katika utoaji huduma ya msaada wa kisheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid kilichofanyika wilayani Ruangwa.

Chobi amesema Mkoa wa Lindi umepunguza migogoro mingi hasa ya wakulima na wafugaji kwa kuwajengea vitalu na kutoa elimu juu ya madhara ya migogoro.

“Tumeweza kupunguza migogoro mingi kwa kutoa elimu kwa wananchi hasa ile migogoro ya kata kwa kata na kijiji kwa kijiji kwa kuwapa elimu na kuweza kuwapangia vitalu ambapo kila mkulima na mfugaji anajua eneo lake,”amesema Chobi

Kuhusu msaada wa kisheria ambao utatolewa mkoani humo Chobi amesema utaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza migogoro yote iliyopo Mkoa wa Lindi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya msaada wa kisheria mkoani Lindi

Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Nathalis Linuma amesema kupitia  kampeni hiyo ya msaada wa kisheria amewataka maofisa ardhi kwenda kutoa  elimu ya kutosha ilikuweza kumaliza migogoro yote.

“Niwaombe maofisa ardhi pamoja na viongozi kutoka katika Wizara ya Sheria na Katiba kuhakikisha kuwa elimu inawafikia wananchi ya kutosha ilikuweza kumaliza migogoro hapa mkoani kwetu,”amesema Linuma

Akizungumza na mwananchi, Husna Halfan mkazi wa Kijiji cha Chimbila A, amesema kampeni hiyo itasaidia kuondoa changamoto ya migogoro kwani maeneo ya vijijini yana migogoro hiyo.

Ester Msambazi, msajili wa watoa huduma za msaada wa kisheria akizungumza na wataalamu watakaoshiriki katika utoaji huduma ya msaada wa kisheria katika mkoa wa Lindi. Picha na Bahati Mwatesa.

“Kwanza naipongeza Wizara ya katiba na Sheria kwa kuweza kutoa elimu na pia kama sisi huku ambao hatuna uwezo wa kumpa wakili asimamie shauri langu hii kampeni itanisaidia mimi kupata uelewa wa nini nifanye ilikuweza kupata haki zangu,”amesema Halfan

Bakari Abdu, mkazi wa kata ya Nandagala wilayani Ruangwa amesema Serikali imefanya jambo jema kwa kuanzisha kampeni hiyo kutokana na wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha.

“Kiukweli migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Ruangwa kidogo imepungua baada ya kupatiwa elimu ya matumizi bora ya ardhi, lakini hii kampeni ya msaada wa kisheria itaweza kuondoa au kumaliza changamoto za migogoro wilayani kwetu,”amesema Bakari

Related Posts