Dar es Salaam. Maandalizi ya Kariakoo kuanza kufanya biashara saa 24 yamepamba moto ambapo Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), umesaini mkataba na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanza kufunga kamera 40 katika awamu ya kwanza.
Mkataba huo umeseainiwa leo Jumanne Februari 18, 2025 kati ya Meneja wa kikosi cha umeme Temesa, Pongeza Semakuwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo, Elihuruma Mabelya.
Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja tangu Mwananchi itoe habari ikieleza namna wafanyabiashara, bodaboda walivyojipanga na maboresho hayo ya ufanyaji biashara.
Ufanyaji biashara huo wa saa 24, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 22, 2025.
Pia, katika habari hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliiambia Mwananchi kuwa tayari Temesa ilishinda zabuni hiyo na kilichokuwa kinasubiriwa ni kumalizika kwa mchakato wa mwisho wa manunuzi ya kamera hizo.
Akizungumza leo na Mwananchi muda mfupi, baada ya kumaliza kusaini mkataba huo, Semakawa amesema wanatarajia kuanza kufunga kamera hizo wiki mbili zijazo.

Ametaja maeneo yatakayoanza kufungwa kamera hizo kuwa ni barabara zote zinazoingia katika katika soko Kuu la Kimataifa Kariakoo.
“Tunachokifanya sasa ni kuzipitia kwanza barabara zote ambazo kamera hizo zinatakiwa kufungwa, ambapo baada ya kumaliza kazi hiyo, wiki mbili kuanzia sasa tutaanza kuzifunga rasmi,”amesema Semakuwa.
Naye Mkurugenzi wa jiji, Mabelya amesema Sh514.3 millioni zitatumika katika shughuli hiyo, fedha ambazo zilitenwa na halmashauri katika bajeti yake ya mwaka 2024/2025 lengo likiwa kuimarisha ulinzi na usalama wa biashara katika eneo la Kariakoo na barabara kuu zinazoingia na kutoka katikati ya jiji.
Amesema Katika bajeti hiyo ambapo kwa mkataba huo awamu ya kwanza utahusisha ufungaji wa kamera 40 ambazo zitafanya kazi saa 24..
“Lengo la mpango huu ni kuimarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara, kuongeza ufanisi wa shughuli za kibiashara na kusaidia mamlaka husika katika udhibiti wa usalama wa jiji.
Pia, zitasaidia kurahisha utambuzi wa matukio , kuimarisha ufuatiliaji wa wahalifu na kutoa ushahidi wa haraka pale inapohitajika,” amesema.
Mabelya ameongeza kuwa katika kuhakikisha ufuatiliaji wa hali ya usalama na udhibiti wa matukio ya kihalifu, kitovu cha kamera hizo zitafungwa katika kituo cha Polisi Msimbazi na katika ukumbi wa Anatouglo,”amesema mkurugenzi huyo.