Mauaji harusini yamtupa jela miaka 12

Moshi. Mahakama Kuu kanda ya Moshi, imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 12 jela, mkazi wa Masama Nguni Wilaya ya Hai, Vicent Timoth (25), kwa kosa la kumuua mmoja wa wageni waliohudhuria harusi ya mdogo wake.

Awali, Timoth alishitakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia chini ya kifungu 196 na 197 cha kanuni ya adhabu, lakini kukiri kosa la kuua bila kukusudia, ombi ambalo lilikubaliwa na Jaji Adrian Kilimi baada ya Jamhuri kutokuwa na kipingamizi.

Kulingana na hati ya mashitaka, mshitakiwa huyo ambaye anafahamika pia kama Ng’unda, alidaiwa Oktoba 8, 2023 huko Masama Nguni wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro alimuua kwa kumchoma kwa kisu, Abdul Hussein bila kuwa na uhalali kisheria.

Ombi la kukiri kufanya mauaji hayo bila kukusudia, liliwasilishwa kwa niaba yake na wakili wake, Deusderius Hekwe ambapo mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo, Henry Daud aliyesaidiana na Wanda Msafiri, hawakupinga ombi hilo.

Akisoma maelezo ya namna kosa hilo lilivyotendeka, wakili Henry alieleza siku ya tukio, mshitakiwa pamoja na marehemu, walikuwa ni waalikwa katika sherehe ya harusi ya mdogo wa mshitakiwa, aitwaye Amani Ng’unda.

Wakati wakiendelea kufurahia sherehe hiyo kwa kunywa na kula, kulizuka ugomvi kati ya marehemu na mshitakiwa na katikati ya ugomvi huo, mshitakiwa alichomoa kisu kutoka katika mfuko wa suruali aliyevaa na kumchoma nacho chini ya kifua.

Marehemu aliwahishwa kituo cha Afya Masama kwa ajili ya kuokoa uhai wake na matibabu, lakini alifariki dunia siku iliyofuata akiendelea kupatiwa matibabu ambapo tukio hilo lilitolewa taarifa katika kituo cha Polisi Bomang’ombe.

Uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa ulionyesha kiini cha kifo kilitokana mshituko uliotokana kiasi kikubwa cha damu hupotea haraka, na kusababisha mtiririko wa damu usiofaa kwa tishu na viungo na utoaji oksejeni kuwa mdogo.

Hali hiyo ilisababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali ambapo baada ya mshitakiwa kukamatwa, alihojiwa na polisi na kukiri kutenda kosa hilo na hata aliposomewa maelezo hayo ya namna kosa hilo lilivyotendeka, aliyakubali.

Akiwasilisha adhabu anayostahili mshitakiwa huyo, wakili wa Serikali Henry Daud, alisema mshitakiwa hana kumbukumbu za makosa ya nyuma isipokuwa wanaomba mahakama itoe adhabu kali na kuainisha sababu kuu tatu.

Moja ni kutokana na aina ya silaha iliyotumika kumuua marehemu ambayo ni kisu, mbili ni sehemu ambayo kitu hicho kilipigwa katika mwili wa marehemu na tatu ni kutokana na tabia na mwenendo wa mshitakiwa kabla na baada ya tukio.

Akifafanua, wakili alisema mshitakiwa aliondoka katika eneo la mzozo na kwenda nyumbani na kurudi na kisu na kumchoma nacho marehemu na baada ya kufanya hivyo, alitoroka kutoka eneo la tukio na kumwacha marehemu bila msaada.

Hiyo kwa mujibu wa wakili huyo, ilionyesha alikuwa na nia ovu ya kumuua marehemu, lakini wakili Hekwe katika maombolezo ya mteja wake ili apewe adhabu ndogo, alirejea hoja ya Jamhuri kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Katika hoja ya pili, wakili Hekwe aliiomba mahakama kuzingatia mazingira ya tukio ambayo hayaonyeshi uwepo wa dhamira ovu kwa kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa manane katika eneo ambalo kulikuwa na watu wengi wakisherehekea harusi.

Lakini wakili huyo alisema marehemu na watu wengine waliohudhuria sherehe hiyo walikuwa wamekunywa pombe nyingi na pia kulikuwa na mzozo kati ya mtu aitwaye Ndea na bodaboda wengine na siyo marehemu na mshitakiwa.

Katika hoja nyingine, wakili huyo alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwa mdogo wa mshitakiwa aitwaye Amani ambaye alialika watu wengine kusherehekea harusi na silaha iliyotumika ilichukuliwa nyumbani kwa Amani na kuitumia kujilinda.

Wakili huyo aliiomba mahakama kuzingatia muda ambao mshitakiwa ameshakaa gerezani hadi anapohukumiwa na kwamba alipotenda kosa alikuwa na umri wa miaka 23, umri ambao hajakomaa kufanya maamuzi na alikuwa ni mlevi.Hoja ya mwisho ni kuwa mshitakiwa hakuvisumbua vyombo vya uchunguzi kwani alitoa ushirikiano kwani alijisalimisha mwenyewe polisi na akaomba apelekwe kwa mlinzi wa amani na huko alikiri kosa na kueleza kwa uwazi nini kilichotokea.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Akitoa uamuzi wa aina ya adhabu kwa mshitakiwa katika hukumu yake aliyoitoa Februari 17 na kupakiwa katika mtandao wa mahakama Februari 19,2025, Jaji Kilimi alisema, alisema ukubwa wa kosa huonekana kwenye hati ya mashitaka.

Jaji alisema kulingana na taarifa za kosa hilo, mshitakiwa alitumia kisu kumchoma nacho marehemu na ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu na maelezo yake kwa mlinzi wa amani, yanathibitisha kuwa mshitakiwa alimchoma kwa kisu.

“Kwa hiyo hakuna ubishi kuwa kisu ambayo ni silaha hatari ilitumika kuchoma mwili wa mwanadamu aliye hai. Kwa hiyo kulingana na mwongozo wa utoaji adhabu, adhabu inaangukia kati ya miaka 10 na kifungo cha maisha,”alisema.

“Sasa hoja ya pili ya kuishughulikia ni adhabu gani ni sahihi. Baada ya kuzingatia uzito wa kosa na maelezo yaliyotolewa na maombolezo kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, ninaona kifungo cha miaka 18 jela ndicho anachostahili”

Jaji aliendelea kueleza kuwa kwa kuwa mshitakiwa alikiri kosa, anaona kuwa hiyo imesaidia kuokoa muda adhimu wa mahakama na gharama na pia alikiri kosa mbele ya mlinzi wa amani, inaonyesha mshitakiwa anajutia kosa alilolitenda.

Kutokana na hilo, anastahili kupunguziwa moja ya tatu (1/3) ya kifungo cha miaka 10 hivyo mahakama inampunguzia miaka sita na kubakia kifungo cha miaka 12 lakini pia akasema muda aliokaa gerezani baada ya kukiri kosa utazingatiwa.

Related Posts