Msemaji wa Jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulayigye amethibitisha kuwa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (UPDF) limeingia kwenye eneo la Bunia, ambalo ni makao makuu ya jimbo la Ituri, sehemu muhimu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
Jenerali Kulayigye amevieleza vyombo vya habari kuwa UPDF inalenga kuwadhibiti wanamgambo wa ADF ambao wana uhusiano na kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) na ambao wanaendeleza mauaji ya watu katika kanda hiyo.
Jeshi la Uganda, kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC), limeendelea kukisaka kikundi cha waasi hao ambao wametokea Uganda na kupiga kambi katika misitu ya Kongo DR.
Itakumbukwa kuwa, Mkuu wa Majeshi wa Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni, alitoa onyo mwishoni mwa juma kuwa jeshi hilo lingeshambulia eneo la Bunia, iwapo vikosi vya wapiganaji wa ADF vitakaidi kujisalimisha ndani ya saa 24.