Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, hakuna kisingizio cha kuifanya Afrika iendelee kuwa haina uwakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Guterres alikuwa katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, alikohudhuria Kikao cha 38 cha Kawaida cha Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), ambacho kilianza Jumamosi iliyopita na kuendelea hadi Jumapili.
Katibu Mkuu huyo wa UN amesisitiza kuwa, ataendelea kufanya kazi na Umoja wa Afrika na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha Afrika inapata uwakilishi inaouhitaji, ikiwa ni pamoja na kuwa na wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakuu wengi wa nchi za Afrika wanahisi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa halina ufanisi kikazi na haliko jumuishi kwa nchi zote wanachama na wamekuwa wakifanya kampeni za kuwania kupata viti viwili vya baraza hilo kwa takribani miaka 80 tangu umoja huo ulipoanzishwa.