Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeieleza Mahakama bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya kusafirisha vinyonga 164, nyoka na mijusi, inayomkabili Eric Ayo na wenzake wawili.
Ayo na wenzake wanakabaliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 23/2021 yenye mashtaka matatu ya yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na safirisha nyara za Serikali.
Mbali na Ayo, washtakiwa wengine ni Ally Ringo na Aziz Ndago, ambao kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh20 milioni bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Jana Jumanne, Februari 18, 2025 Wakili wa Serikali Winiwa Kasala amemweleza Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa kesi hiyo imeitwa kwa kutajwa na upelelezi haujakamilika.
“Kutokana na upelelezi wa kesi hii kutokukamilika, tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine ya kutajwa,” amesema Kasala.
Hakimu Magutu amekubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, 2025 itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kati ya Desemba mosi 2020 na Januari mosi, 2021 katika mikoa ya Morogoro, Tanga na Dar es Salaam, walipanga njama na kuongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Vilevile, wanadaiwa kukutwa na nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda katika kipindi na mikoa ileile.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kukutwa wakikusanya, kusafirisha na kuuza vinyonga 164, Mijusi 20 na nyoka sita, wote wakiwa na thamani ya Sh20 milioni, mali ya Serikali.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na dola za Marekani 9,000 sawa na Sh19.8 milioni.
Shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha linalomkabili Ayo peke yake, kuwa Januari 26, 2021 katika benki ya CRBD iliyopo Msamvu mkoani Morogoro, kwa makusudi alibadilisha dola za Marekani 400 na kupata Sh923,600, wakati akijua, fedha hizo zilikuwa zimetokana na uuzaji wa nyara za Serikali.
Ringo na Ndago wapo nje kwa dhamana huku Ayo akiendelea kusota rumande kutoka na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Machi 16, 2021.