KITAUMANA katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa wakati mastaa wa Coatal Union na Azam watakapovuja jasho kwenye msako wa pointi tatu ndani ya dakika 90.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ambao utapigwa kesho utakuwa wa 20 kwa timu hizo msimu huu, kila moja ikihitaji ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri kwenye msimamo.
Azam FC inahitaji kupunguza pengo baina ya timu zilizo juu yake kwenye msimamo, Yanga ikiwa kinara kwa pointi 52 tofauti ya pointi 10 na Azam, lakini pia Simba inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 47 tofauti ya pointi tano na Azam ambayo inashika nafasi ya tatu kwa pointi 42, hivyo kama itashinda itarejesha matumaini makubwa kuwania ubingwa.
Coastal Union inahitaji kujitengenezea mazingira mazuri ya kumaliza nafasi ya juu ikiwa inashika nafasi ya sita kwa pointi 22 sawa na Fountain Gate pamoja na KMC.
Timu hiyo imeziacha pointi moja Pamba Jiji na Namungo zenye 21, mbili Mashujaa, JKT tanzania na Dodoma Jiji FC zenye 20 na pointi tano Tanzania Prisons yenye 15.
Mara ya mwisho Coastal na Azam kukutana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa ni Mei 29,2022 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA, ambapo Coastal ilishinda kwa mikwaju ya penalti 6-5.
Lakini, mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa ni Septemba 22, 2024 pale Azam Complex baada ya dakika 90 ubao kusomeka Azam 1-0. Ndani ya dakika 90 wababe hao walivuja jasho huku makipa wakifanya kazi kuokoa hatari za washambuliaji, hivyo mchezo wa kesho unatazamiwa kuwa mgumu kwa timu zote.
Katika mechi tano za mwisho za ligi ambazo timu hizo zimekutana Azam imeshinda nne, sare moja na mchezo ambao ulitoa mabao mengi ni ule wa Novemba 27, 2023 Azam ikishinda 3-2 na baada ya hapo matokeo yamekuwa chini ya mabao matatu.
Azam sio kinyonge inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi nne kati ya tano za mwisho ilizocheza ikifunga jumla ya mabao tisa ndani ya dakika 450.
Mechi hizo ni ushindi dhidi ya Mashujaa (2-0), KMC (2-0), JKT Tanzania (3-1), Fountain Gate (2-0) na kichapo cha 1-0 dhidi ya Pamba Jiji FC.
Kiungo wa Azam, Feisal Salum amehusika kwenye mabao 14 katika mechi zote za timu yake msimu huu akifunga manne na kutoa asisti 10, hivyo huenda akawa moto katika mchezo huo.
TAOUSSI, CHILAMBO WATOA NENO
Akizungumzia mchezo huo, kocha mkuu wa Azam, Rashid Taoussi alisema: “Siufahamu uwanja ambao tunakwenda kucheza, lakini wachezaji wangu wako tayari kwa sababu tumefanyia kazi makosa ya mchezo uliopita. Tumejiandaa vya kutosha kwa sababu tunakwenda kucheza na timu ngumu.
“Lengo kuwa ni kutwaa ubingwa na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa na naamini hilo litafanikiwa kwa sababu nina wachezaji wazuri na katika mchezo wa kesho kuna nyota kadhaa ambao tuliwakosa wamerejea ndani ya kikosi.”
Nyota wa timu hiyo, Nathaniel Chilambo alisema licha ya mchezo huo kuwa mgumu watahakikisha wanapata matokeo mazuri ambayo yatazidi kuwaweka kwenye ramani ya kuwania ubingwa.
Kocha wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema kuwa wanahitaji pointi tatu wakikumbuka mchezo uliopita walipoteza dhidi ya Pamba Jiji kwa mabao 2-0.
“Tumetoka kupoteza, isingekuwa vyema tena tukapoteza katika uwanja wetu wa nyumbani. Kwa hiyo nimeandaa wachezaji vyema kisaikolojia kwamba angalau tuweze kupata matokeo,” alisema Mwambusi.
Straika wa timu hiyo, Ally Mgaya aliwataadharisha Azam kuwa wasitegemee mchezo mwepesi kutoka kwao.
Katika mechi tano za mwisho za Coastal Union imeshinda mmoja sawa na iliopoteza na kutoka sare tatu ambapo imefunga mabao matatu na kufungwa matano. Mechi hizo ni ushindi dhidi ya JKT Tanzania 2-1, kupoteza kwa Pamba Jiji 2-0 na sare Tabora United 1-1, KMC 1-1 na Mashujaa iliyotoka nayo suluhu.