Kigoma. Shahidi wa pili wa upande wa mwombaji katika shauri la uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi, Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kuwa askari polisi alitumbukiza kura bandia kwenye sanduku la kura.
Shahidi huyo, Rajabu Zuberi alitoa maelezo hayo hayo alipokuwa akitoa ushahidi wake katika shauri hilo lililofunguliwa na mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Didas Baoleche.
Baoleche, ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa huo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024, alifungua shauri hilo dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mrisho Mwamba, aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
Wajibu maombi wengine katika shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Mfawidhi Ana Kahungu, ni msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).

Aliyekuwa mgombea mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Didas Baoleche baada ya kutoka katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma.
Baoleche anadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na ukiukwaji wa kanuni, sheria na taratibu, ikiwemo matokeo kutochapishwa wala kubandikwa kama kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza, pamoja na kuingizwa kwa kura bandia, baadhi yake zikidaiwa kukamatwa.
Kwa mujibu wa madai yake, kasoro hizo zilimnyima haki yake ya kikatiba na wananchi wa mtaa huo walishindwa kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Hivyo, ameiomba mahakama kutamka kuwa uchaguzi huo ni batili na kuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo kutangaza uchaguzi mpya ndani ya siku saba na uchaguzi huo kufanyika ndani ya siku 60.
Katika ushahidi wake wa msingi, akiongozwa na Wakili wa ACT-Wazalendo, Prosper Maghaibuni, na wakati wa kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi Jumanne, Februari 18, 2025, shahidi huyo, mkazi wa Kibirizi, alieleza kuwa alishiriki katika uchaguzi huo kama mpigakura.
Akiwa katika foleni kwenye kituo cha kupiga kura katika Shule ya Kibirizi Novemba 27, 2024, vurugu zilitokea baada ya mtu aitwaye Rama Kagongo kukamatwa na mmoja wa mawakala akiwa na kura bandia.
Kagongo alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na kura hizo zilichukuliwa na polisi aliyekuwepo kituoni hapo.
Baada ya muda, polisi huyo alimruhusu Kagongo kukimbia, jambo lililosababisha wananchi kuanza kumfukuza.
Wakati huohuo, askari huyo alizichukua kura hizo na kuzitumbukiza kwenye sanduku la kura. shahidi alipolalamikia kitendo hicho, aliamriwa kuondoka, ndipo akaenda kuripoti tukio hilo kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
Kutokana na hali hiyo, shahidi anadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki na ameiomba Mahakama kutamka kuwa ni batili.
Katika majibu yake kwa maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili Hamis Kimilomilo, anayemwakilisha Mrisho Mwamba wa CCM, shahidi alieleza kuwa kura bandia zilizokamatwa zilifanana na kura halali zilizotumika katika uchaguzi huo.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Mkama Musalama, shahidi alisema Rama Kagongo aliyekamatwa na kura bandia, alikuwa mbele yake kwenye foleni, lakini hakumbuki aliyekuwa nyuma yake kama alikuwa Baoleche.
Aidha, alipoulizwa na Wakili wa Serikali Res Majara, shahidi alisema hakuripoti tukio hilo polisi kwa kuwa polisi alikuwepo eneo hilo na ndiye aliyekuwa na wajibu wa kumkamata mhalifu.
Pia, alisema hakwenda kituo cha polisi kumshtaki askari aliyedai alitumbukiza kura bandia kwenye sanduku, kwa sababu alitoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi ambaye kwa ufahamu wake, ndiye mwenye mamlaka ya kushughulikia masuala hayo.
Awali, shahidi wa kwanza ambaye ni mwombaji (mlalamikaji) katika shauri hilo, Baoleche akiongozwa na Wakili Maghaibuni, ameieleza mahakama kuwa aliteuliwa na chama chake na msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Kibirizi kugombea nafasi hiyo.
Katika maelezo ya ushahidi wake, Baoleche alieleza kuwa siku ya uchaguzi alipiga kura katika kituo cha Kibirizi Shuleni, chumba E. Akiwa kwenye foleni karibu na mlango Ramadhani Kagonga, mkazi wa Kibirizi na mwanachama wa CCM, alikamatwa akiwa na kura bandia.
Baada ya kupiga kura, Kagonga alitumia muda mrefu karibu na masanduku ya kura, jambo lililoibua wasiwasi. Wakala wa Baoleche, Hussein Kiba, alimfuatilia na alipomchungulia, alimuona akiwa na furushi la kura akizitumbukiza kwenye sanduku la kura. Kiba alimvamia Kagonga na kumtoa nje, huku kura nyingine zikiwa tayari zimetumbukizwa na nyingine zikiwa bado mkononi mwake.
Wasimamizi wa uchaguzi waliokuwamo ndani pamoja na askari polisi walifika haraka na kumnasua wakala kutoka kwa Kagonga. Polisi alibaki akiwa ameshikilia kura hizo mkononi.
Baoleche, aliyedai alikuwa umbali wa takribani mita tano kutoka mlango, alisema kuwa madirisha yalikuwa wazi kiasi kwamba aliweza kuona kilichokuwa kikitokea ndani.
Alipoingia ndani na kumuuliza askari kwa nini alimwachia Kagonga huku akibaki na kura mkononi, polisi alijibu kuwa suala hilo linapaswa kuachwa kwao (polisi) walishughulikie.
Amedai baada ya muda, Kagonga alipotoka nje, wananchi walimvamia na kuanza kumpiga, lakini polisi walifika na kumtoa, kisha akakimbilia msikitini.
Baada ya uchaguzi, Baoleche alirejea nyumbani na baadaye akaenda katika ofisi ya Kata kutaka kujua matokeo. Alipomkuta msimamizi wa uchaguzi na kumuuliza, alijibiwa kuwa hayo ndiyo matokeo.

Hata hivyo, matokeo hayo yalikuwa chini na yamelowana kiasi cha kufanya namba zisiweze kuonekana vizuri. Kwa msingi huo, Baoleche alidai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki kwa kuwa uliathiriwa na ongezeko la kura bandia. Ameliomba mahakama itamke kuwa uchaguzi huo ni batili.
Akihojiwa na Wakili Hamis Kimilomilo wa CCM, Baoleche alijibu kuwa hamjui aliyeshinda na kwamba alimshtaki mtu asiyemjua.
Hata hivyo, baadaye alidai kuwa aliyemshtaki alitangazwa mshindi katika ofisi ya kata, ingawa matokeo hayakubandikwa kama inavyotakiwa na kanuni za uchaguzi.
Kuhusu ushiriki wake katika uchaguzi, Baoleche alisema kuwa aliteuliwa na msimamizi kwa nyaraka, lakini hakuwasilisha nyaraka hiyo mahakamani kuthibitisha uteuzi wake.
Aidha, alikiri kuwa hana idadi kamili ya kura zilizokamatwa na alipoulizwa kuhusu idadi ya kura alizopata katika uchaguzi huo, alijibu kuwa hawezi kukumbuka.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Fortunatus Mwandu, Baoleche aliieleza Mahakama kuwa kielelezo alichokitoa kuthibitisha kuwa alikuwa mgombea ni nakala ya matokeo ya uchaguzi. Hata hivyo, alikiri kuwa hajawasilisha mahakamani fomu yake ya uteuzi kuwa mgombea.
Kuhusu kura bandia na jinsi zilivyofanana na halali, alidai zilikuwa nyingi zaidi ya inavyotarajiwa.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Mkama Musalama, alikiri kuwa katika hati yake ya madai hajaandika kuwa Ramadhani Kagonga alitumbukiza kura bandia kwenye sanduku la kura.
Ameiambai Mahakama kuwa katika maelezo yake ya ufafanuzi alipokuwa akiongozwa na Wakili wake Prosper Maghaibuni, Baoleche alifafanua kuwa alipotaja kura bandia, alimaanisha zile zilizokamatwa kwa Kagonga.
Kuhusu hoja ya kutowasilisha mahakamani kura zinazodaiwa kuwa bandia, alieleza kuwa hazikuwasilishwa kwa sababu zilishikiliwa na polisi, huku nyingine zikiwa tayari zimetumbukizwa kwenye sanduku la kura.