WAKATI hali ikiwa si shwari kwa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra kutokana na kufungwa mabao mepesi hivi karibuni yanayoonekana yanatokana na makosa binafsi, kocha aliyekuwa akimnoa ndani ya timu hiyo ameomba kuondoka na taarifa zinasema tayari ametoa FAR Rabat ya Morocco.
Kocha huyo anayemnoa Diarra na makipa wengine katika kikosi cha Yanga, alikuwa ni Alaa Meskini raia wa Morocco ambaye ameuomba uongozi kumvunja mkataba wa kuendelea kuinoa kutokana na sababu za kifamilia na tayari jamaa ameshatimka Jangwani na kuibukia FAR Rabat iliyopo nchi anayotokea.
Kabla ya Diarra kuyumba hivi karibuni, kipa huyo wa kimataifa kutoka Mali alikuwa na mitatu mfululizo iliyopita ya mafanikio ikiwamo kutwaa tuzo mbili za Kipa Bora wa Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho.
Makali ya Diarra yameonekana kupungua makali tofautio na alivyoanza msimu wa 2021-2022 alipotua Yanga, akitokea Stade Malien ya Mali ambapo msimu huo alitwaa tuzo ya Kipa Bora na kurudia tena na 2022-2023 alibeba tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu Bara na msimu uliopita alinyakua Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, wakati kipa huyo akijitafuta, huku akiacha maswali mengi kwa mashabiki waliofikia hatua ya kumbatiza jina la ‘Screen Protector’, taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinabainisha kocha Meskini tayari ameandika barua ya kuvunja mkataba huku uongozi ukiridhia.
Mtoa taarifa huyo ameenda mbali zaidi na kutaja sababu ya kocha huyo kufikia uamuzi huo ni kuwa, anataka kuwa karibu na familia yake iliyopo Rabat, Morocco na Mwanaspoti limepenyezewa kuwa amejiunga na FAR Rabat inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco, Batola Pro.
“Kocha Alaa Meskini ameomba kuvunja mkataba na uongozi umeridhia kutokana na sababu alizozitaja, ambazo ni kuhitaji kuwa karibu na familia yake huko kwao Morocco.
“Amesema kwa sasa mama yake anaumwa na hakuna wa kumuuguza, anataka awe karibu naye ukizingatia kwamba hivi karibuni alifiwa na baba yake mzazi,” kilisema chanzo hicho.
Kocha Meskini aliyejiunga na Yanga Agosti 2023 wakati wa kocha Miguel Gamondi na hadi anaondoka Yanga tayari amefanya kazi na makocha watatu.
Mbali na Gamondi, kocha Meskini amefanya kazi na Sead Ramovic na Miloud Hamdi na hadi anaondoka alikuwa amebakiza mkataba wa miezi minne kabla ya kumalizika Juni 2025, huku Yanga ikiwa imecheza mechi 20 za Ligi Kuu Bara msimu huu ikifungwa mabao tisa na kimataifa iliruhusu sita katikia mechi nane zikiwamo za raundi ya awali na zile za makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.