Mahakama yatupa maombi ya watumishi wa zamani wa Takukuru

Dodoma. Wafanyakazi wa zamani wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waliokuwa wamefungua shauri kuomba mapitio ya mahakama, wakipinga kufutwa kwao kazi, wamekwaa kisiki baada ya maombi yao kutupwa.

Watumishi hao wa zamani wa Takukuru, Hassan Chamshama, Hamis Mkao na Ibrahim Liban, walifungua maombi namba 27443/2024 dhidi ya mwenyekiti wa kamati ya usimamizi Takukuru, Takukuru na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hata hivyo, katika uamuzi wake alioutoa jana Jumanne, Februari 18, 2025 na kuwekwa katika mtandao wa mahakama wa TanzLii leo, Februari 19, 2025 Jaji Evaristo Longopa wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, aliyatupa maombi hayo akisema hayakuwa na mashiko.

Kulingana na maombi yao, walieleza wao walikuwa waajiriwa wa mjibu maombi wa pili (Takukuru) kama maofisa wachunguzi kati ya Agosti 7, 2014, Julai 30,2014 na Februari 28,2001 mtawalia, hadi walipoachishwa kazi na mwajiri wao mwaka 2023.

Walieleza katika utumishi wao, Takukuru iliwachagua kuhudumu katika kampuni ya Akiba na Mikopo inayojulikana kama PCCB Saccos Limited ambapo Chamshama na Liban walikuwa wajumbe wa bodi na muombaji wa pili, Mkao akawa mhasibu wa Saccos hiyo.

Muda wao wa uongozi katika Saccos hiyo kwa Chamshama na Liban ulimalizika Oktoba 10, 2022 na kurudishwa katika ofisi ya Takukuru ambapo Aprili 2023, mwajiri aliwaita na kuwajulisha anaendesha uchunguzi wa kijinai wa matumizi mabaya ya fedha za Saccos.

Wote wakaandika maelezo ya onyo kuhusiana na tuhuma hizo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wakaendelea na majukumu yao kama kawaida hadi baadaye 2023 wakapokea barua hawatapandishwa vyeo kutokana na uchunguzi unaoendelea.

Oktoba 2023, waombaji hao wakapokea mashtaka ya kinidhamu na kutakiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu na baada ya kamati kukamilisha usikilizwaji, waombaji wote hao watatu walifutwa kazi katika nafasi walizokuwa wanahudumu.

Kulingana na waombaji hao, waliomba wapewe mwenendo wa shauri hilo la kinidhamu na nyaraka zote zinazohusiana na kuachishwa kwao kazi lakini hawakupewa kwa wakati na hivyo wakaamua kukata rufaa kwa mjibu maombi wa kwanza.

Hata hivyo, mjibu maombi wa kwanza ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Usimamizi Takukuru, alizikataa rufaa zao kwa maelezo ziliwasilishwa nje ya muda na ni kutokana na uamuzi huo, ndio wakaamua kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.

Nini walichokuwa wanaomba

Katika maombi hayo, wakaomba mambo manne, moja ni mahakama itoe amri ya kubatilisha, kufuta na kuuondoa uamuzi wa mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa Februari 20 na Machi 27, 2024 wa kukataa rufaa zao kwa kamati.

Ombi la pili ni kuiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha, kufuta na kuondoa katika kumbukumbu, uamuzi wa Takukuru uliotolewa kupitia kwa mkurugenzi mkuu ambao ulihusu kuwafuta kazi waombaji wote watatu katika shauri hili.

Halikadhalika waliiomba mahakama itoe amri ya kuwalazimisha mjibu maombi kwa kwanza (mwenyekiti wa kamati) na wa Pili (Takukuru) kutekeleza majukumu yao kulingana na sheria, misingi ya haki ya asili na Haki za Kikatiba.

Katika ombi la nne, kupitia mapitio hayo ya mahakama, waliiomba mahakama itoe amri ya kuwataka mjibu maombi wa kwanza na wa pili katika shauri hilo, kutoingilia ajira zao bila kufuata kanuni na sheria lakini tano, wakaomba walipe gharama za kesi.

Desemba 6, 2024 wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo ambayo yaliambatanishwa na viapo vya waombaji, wajibu maombi kupitia kiapo kinzani kutoka kwa Ayub Akida, ambaye ni mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu, waliponga maombi hayo.

Kupitia kwa wakili wao, Issack Tasinga, waombaji hao walisema mjibu maombi wa kwanza na wa pili ni mamlaka mbili tofauti, moja ikiwa ni mamlaka ya rufaa na nyingine ikiwa ni mamlaka ya kinidhamu kwa waombaji hao.

Kupitia kiapo cha Akida, wajibu maombi walipinga vikali madai ya watumishi hao wa zamani wa Takukuru, akisema maombi hayo yanakiuka sheria kwa kuwa waombaji hao sio watumishi wa mjibu maombi wa kwanza hivyo kiapo chao ni batili.

Alieleza njia pekee ambayo ingeweza kufanyika ni kuwa na kiapo cha pili kutoka kwa ofisa kutoka ofisi ya mwenyekiti wa kamati ya usimamizi ambayo ilishiriki katika mchakato uliohusiana na rufaa ya wajibu maombi hao hivyo akaomba kiondolewe.

Kuhusu maombi ya msingi, wakili Tasinga alijenga hoja kuwa waombaji hao watatu waliazimwa na PCCB Saccos Limited, wakifanya kazi kwa uhuru kwa kuzingatia sheria ya vyama vya ushirika kwa vyama vya akiba na mikopo ya mwaka 2020.

Walieleza katika utendaji wao wa kazi, walibanwa na sheria na kanuni za ushirika na si vinginevyo, lakini ni baada ya miezi sita kupita tangu wamalize utumishi wao kwenye Saccos, ndipo walipopata wito juu ya matumizi mabaya ya fedha.

Waombaji hao walipinga muundo wa kamati ya nidhamu iliyosikiliza shauri lao kwa madai kuwa haina wajumbe isipokuwa mwenyekiti na katibu na haikuwa na uwiano wa kijinsia, lakini hoja zao hizo hazikusikilizwa wakati wa shauri hilo.

Ni jambo lililo katika kumbukumbu za mahakama kuwa, shauri hilo la kinidhamu lilikamilika na wao kuachishwa kazi, hawakuridhika wamjulisha mjibu maombi wa pili nia yao ya kukata rufaa na wakaomba mwenendo ili uwasaidie kuandaa sababu za rufaa.

Baadaye wakaitwa kwenda kuchukua mwenendo na kumbukumbu za shauri ya kinidhamu walizoomba, lakini badala yake wakakamatwa, kuwekwa mahabusu na baadae kushitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa uhujumu uchumi.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 51 ya 2023 bado inaendelea kusikilizwa na wako nje kwa dhamana na sasa wako mbele ya mahakama hiyo kuomba mapitio ya mahakama (judicial review) kupinga kufukuzwa kazi na rufaa yao kukataliwa.

Walidai Takukuru haikuwa na mamlaka ya kuwafuta kazi kwa kutumia sheria za utumishi za PCCB, hawakuzingatia haki ya asili (natural justice) na kamati ya nidhamu haikuwa na mwendesha mashitaka, walalamikaji ni Takukuru na ndio walioendesha shauri.

Wajibu maombi kwa upande wao, kupitia kwa wakili wa Serikali, Ngatanda, walisema kanuni za Takukuru kupitia GN namba 300 ya 2009, imeanzisha uwepo wa kamati ya usimamizi na vyombo vingine vya kusimamia mashauri ya nidhamu.

Alisema mjibu maombi wa kwanza na wa pili sio mamlaka mbili tofauti bali ni vyombo vya kinidhamu vinavyopatikana katika taasisi moja ya Takukuru na kanuni ya 4 imetoa muundo wa kamati ya kinidhamu itaundwa na watu gani.

Kuhusu maombi ya msingi, wakili huyo alisema hayana msingi na maombi yao hayastahili kushughulikiwa na mahakama bali kuyatupilia mbali na kusisitiza kupinga vikali yote ambayo yalielezwa na waombaji kupitia kiapo chao.

Uamuzi wa Jaji ulivyokuwa

Katika uamuzi wake, alisema maombi matano ya waombaji hao hayakubaliki katika mamlaka ya mahakama hiyo kwa sababu, moja inahusu amri dhidi ya uamuzi wa kuwafuta kazi na pili, kuitaka Takukuru itende wajibu kwa mujibu wa sheria.

Hoja ya tatu wanayoomba kwa mujibu wa Jaji ni kuwazuia wajibu maombi kuingilia ajira za waombaji na nne, wakaomba wajibu maombi wabebe gharama za kesi.

Jaji alisema kanuni zinazosimamia mapitio ya mahakama (judicial review) zinataka uamuzi unaolalamikiwa unatakiwa uwe ndio wa mwisho kufanywa na mamlaka ya kiutawala na kwamba hakuna nafuu nyingine waombaji wanaweza kuipata.

Kulingana na Jaji, amri kuhusiana na uamuzi wa Takukuru kuwafuta kazi haiwezi kupatikana kwa sababu uamuzi wa Takukuru sio wa mwisho kiasi kwamba upingwe kupitia mapitio ya mahakama na wana njia nyingine ya kuupinga.

“Uamuzi unaweza kupingwa kwa njia ya rufaa ndani ya siku 14 baada ya kupewa taarifa za kuachishwa kazi,”alisema Jaji Longopa na kutoa mifano ya shauri kama hilo.

Jaji alisema waombaji walishindwa kuishawishi mahakama ni wajibu gani wa kisheria ambao waombaji waliomba kwa wajibu maombi na wakakataa kuufanya na kusema wajibu wa mahakama katika mapitio ya mahakama sio sawa na wa rufaa.

Kulingana na Jaji, ombi mojawapo ni kama linataka mahakama ibatilishe uamuzi wa wajibu maombi na kuagiza kusikilizwa upya kwa shauri lao la kinidhamu kwa kuzingatia sheria wakati uamuzi wake ulitegemea kile wajibu maombi walichokiona.

Kulingana na sababu hizo na nyingine, Jaji alisema kwa ujumla wake, maombi hayo dhidi ya wajibu maombi yanastahili kutupwa na kila upande utabeba gharama zake za kesi.

Related Posts