Dar es Salaam. Bei ya dhahabu imepanda na kufikia rekodi ya Sh7.5 milioni kwa wakia moja (troy ounce) mnamo Februari 15, 2025, ikiwa ndio kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa, kwa mujibu wa viwango vya ubadilishaji wa fedha vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ongezeko hilo la Sh1.3 milioni kutoka wastani wa Sh6.2 milioni mnamo Januari 2, 2025, linaakisi ongezeko la mahitaji ya wawekezaji katikati ya hali ya sintofahamu ya uchumi wa dunia, ikiwa ni pamoja na shinikizo la mfumuko wa bei na kuyumba kwa sarafu.
Licha ya kufikia viwango vya juu kihistoria, soko la dhahabu bado linakabiliwa na kuyumba kwa bei. Baada ya kufikia wastani wa Sh7.46 milioni mnamo Oktoba 31, 2024, bei hiyo ilishuka kidogo na kufikia Sh7.42 milioni kufikia Jumanne, Februari 18, 2025.
Hata hivyo, ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana, ambapo bei ya dhahabu ilikuwa Sh5.02 milioni, thamani ya sasa inaonyesha ongezeko la asilimia 49, jambo linalothibitisha dhahabu kuendelea kuwa kivutio kwa wawekezaji wanaotafuta njia salama za kuhifadhi thamani ya mali zao.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, alisema kuwa ongezeko la bei ya dhahabu ni matokeo ya mienendo ya kiuchumi kwa ujumla, hususan athari za mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya sarafu, hali inayowasukuma watu wengi kuwekeza kwenye dhahabu.
“Hali ya sitofahamu duniani imeongeza mahitaji ya dhahabu kama rasilimali thabiti. Shinikizo la mfumuko wa bei na kuyumba kwa sarafu ni sababu kuu zinazowafanya watu kuelekea kwenye dhahabu kama uwekezaji salama,” alisema.
Takwimu za hivi karibuni kutoka soko la kimataifa la London zinaonyesha kuwa mnamo Februari 15, 2025, bei ya dhahabu ilipanda hadi $2,908 kwa wakia moja, kutoka $2,812 mwishoni mwa Januari, ikionesha ongezeko kubwa ndani ya mwezi mmoja pekee.
Tutuba alihusisha ongezeko hili na mabadiliko ya uwiano wa mahitaji na upatikanaji wa dhahabu kwenye sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa madini hayo kutoka migodi.
“Changamoto za kimataifa kama vile hali ya kutokuwepo kwa utulivu wa kisiasa, migogoro ya kiuchumi, na vita vinavyoendelea, zimesababisha wasiwasi kwenye masoko ya fedha, hali inayowasukuma wawekezaji kuelekea kwenye rasilimali salama kama dhahabu,” aliongeza.
Mchambuzi wa masuala ya fedha, Oscar Mkude, alibainisha kuwa matukio fulani ya kimataifa, hususan nchini Marekani, yanaweza kuwa yanachangia mwenendo huu wa soko.
“Kushuka kwa thamani ya soko la hisa (la Marekani), sambamba na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Rais Donald Trump, kumesababisha wawekezaji wengi kuelekeza mitaji yao kwenye dhahabu kwa ajili ya utulivu wa kifedha,” alisema.
Mkude pia alitaja vita inayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na uamuzi wa Afrika Kusini wa kutopeleka dhahabu nchini Marekani kama sababu zinazochangia mabadiliko haya ya soko.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini Tanzania wanafuatilia kwa karibu mabadiliko ya bei na kuhisi athari za kupanda kwa thamani ya madini hayo.
Euphrosina Mtundu, mchimbaji wa dhahabu kutoka Kahama, alisema kuwa amekuwa akipata faida kubwa zaidi kutokana na mauzo ya dhahabu yake, hasa ile yenye ubora wa juu.
“Ninapouza dhahabu yenye ubora wa asilimia 96 hadi 99, napata faida kubwa sana, hasa sasa ambapo bei imepanda,” alisema.
Mchimbaji mwingine kutoka eneo hilo, Zacharia Soko, alieleza kuwa bei ya dhahabu yenye ubora wa asilimia 98 imeongezeka kwa kiwango kikubwa.
“Gramu moja sasa inauzwa Sh218,000 ikilinganishwa na Sh185,000 mnamo Januari,” alisema.
“Ongezeko hili ni faida kwa wachimbaji kama mimi, hasa kwa juhudi za serikali za kuanzisha masoko ya madini yanayohakikisha bei thabiti na kuwezesha ukusanyaji wa mrabaha na kodi”
Wakati bei ya dhahabu ikiendelea kuyumba katikati ya hali ya sitofahamu duniani, wadau wa sekta ya madini wanatarajia kuona ikiwa dhahabu itaendelea kupanda au itatulia katika viwango vilivyopo kwa sasa.