Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imesema barua ya malalamiko kuhusu uteuzi wa viongozi watendaji wa juu na wajumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyowasilishwa katika ofisi hiyo na kada wa chama hicho, imewafikia.
Kanda huyo Lembrus Mchome, mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro anapinga uteuzi wa viongozi hao uliofanwa na Mwenyekiti, Tundu Lissu Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.
Kabla ya kuipeleka katika ofisi hiyo ya msajili, Mchome alipeleka barua hiyo katika ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika jana Jumanne, Februari 18, 2025 akibainisha uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha Baraza Kuu kutimia.
Kwa mujibu wa Mchome vigogo waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (naibu katibu mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (naibu katibu mkuu – Zanzibar).
Katika barua hiyo ambayo Mwananchi imeiona, Mchome anadai wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho kuwa ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala ni batili.
Kwenye kikao hicho cha Baraza Kuu kilichofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam Januari 22, 2025, Lissu aliwasilisha majina ya wateule hao kisha wakaidhinishwa na wajumbe wa baraza hilo kwa kunyoosha mikono.
Mchome ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga Mwanga mkoani Kilimanjaro anadai kwa hali hiyo ni uthibitisho viongozi wa kitaifa na wajumbe wa kamati kuu watano waliopendekezwa na mwenyekiti wa Chadema na kuthibitishwa ni batili.
Kutokana na hilo, kada huyo amesema viongozi wote waliothibitishwa kinyume cha utaratibu watangazwe kuwa batili, wasitumikie nafasi zao hadi uthibitishaji halali utakapofanyika.
Mchome ameongeza kuwa uamuzi wote uliofanywa na kamati kuu ambayo wajumbe hao wameshiriki ubatilishwe na Baraza Kuu liitishwe tena kufanya upya mchakato utakaohakikisha akidi inatimia.
Hatua hiyo ya Mchome imeibua mijadala maeneo mbalimbali ndani na nje ya viunga vya Chadema hususan mitandaoni. Wapo wanaoona kuwapo kwa hoja wakiunga kile kilichosemwa na Mnyika kabla ya Kikao cha Baraza Kuu kuanza na wengine waona kama njia ya kutaka kujirudisha nyuma.
Leo Jumatano Februari 19, 2025 Mwananchi limemtafuta Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kujua kinachoendelea ambapo ameanza kwa kusema barua ya Mchome imeshafika katika ofisi hiyo, wanasubiri kwanza ifanyiwe kazi ndani ya Chadema kwanza.
“Kwa sababu barua imeandika kwa katibu mkuu, tunasubiri ifanyiwe kazi kwanza ndani ya chama, lakini tumeiona ina malalamiko ya msingi sana. Kwa utaratibu uliopo wasiporidhika anakuja kwetu kwa sisi tunasimamia katiba na sheria za vyama,” amesema Nyahoza.
Nyahoza amesisitiza: “Malalamiko yake yana mantiki, kwa hiyo tunasubiri majibu kwa chama ili tuone hili suala lipoje, kwa sababu huwezi kujua ukweli wa jambo hadi usikilize pande zote mbili. Tunasubiri, lakini ukiyasoma unaona mantiki yake, ila huo ni upande mmoja, lazima tusikilize na upande wa pili.”
Kwa mujibu wa Nyahoza, kama mlalamikaji (Mchome) hataridhika na majibu atakayopewa atawasilisha katika ofisi ya msajili kwa sababu mambo ya katiba hayaishii ndani ya chama.
Saa 5:41 asubuhi ya leo Jumatano, Mnyika ametumia akaunti yake ya X, kuelezea barua hiyo ya Mchome akisema: “Kuna mkakati wa kuhamisha mwelekeo kutoka NoReforms NoElection. Uamuzi ya Baraza Kuu Januari 22 2025 ni halali kwa kuwa mkutano ulikuwa na wajumbe halali 234 kati ya 412 sawa na asilimia 56.8.

“Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 6.2.2. kikao hicho kilifanya uthibitishaji kwa mujibu wa Katiba ibara ya 7.7.12 (c) na (e) na hakukuwa na agenda ya uchaguzi. Nakala ya barua tajwa kupelekwa kwa Msajili kunaashiria nia ovu iliyoko nyuma ya pazia,” ameandika Mnyika.
Hata hivyo, Januari 22, 2025, kabla ya kuanza kwa Kikao cha Baraza kuu kilichofanyikia ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema walikodi ukumbi wa Mlimani City ambao kwa siku hiyo walitakiwa wasizidishe zaidi ya saa nne usiku.
“Kwa muda tuliona nao hatupaswi kuongeza ajenda zingine zitakazosababisha kuingia kwenye shida kuhusu ukumbi wa mkutano. Kwa sababu ajenda ya uchaguzi haipo tena kwa pendekezo hilo kama litakubalika akidi ya mkutano huu, haitakuwa tena akidi ya asilimia 75 inayohitajika kama kikao kinahusu ajenda ya uchaguzi.
“Kwa vile hakuna ajenda ya uchaguzi ya kikao hiki ni simple majority nitakayoitangaza katika hatua ya baadaye kidogo, baada ya sekretarieti kukamilika idadi ya mwisho ya wajumbe, lakini kwa wingi wajumbe waliopo hivi kwa vyovyote tuna simple majority mkutano unaweza kuendelea,” alisema Mnyika.
Baada ya maelezo hayo ya Mnyika, Mchome naye amejitokeza kwenye hoja hiyo akiweka kipande cha sekundi 21 cha Mnyika akizungumza siku ya Kikao cha Baraza kuu akizungumzia suala la akidi kutokutimia.
Mchome ameambatanisha kipande hicho cha video, ameandika: “Mhe Katibu Mkuu, Mosi, naomba ujibu barua yangu. Hakuna mkakati wowote wa kuhamisha NoReformsNoElection. Wala nia ovu dhidi ya taasisi yangu.”
“Uzuri mkutano huo ulikuwa live, dunia inaona na wote wameshuhudia. Hakukuwa na akidi hiyo unayosema. Natamani tusimamie katiba yetu.”
Namna ya kumaliza mvutano
Mwananchi limezungumza na wanasheria, John Mallya ambaye kupata mtazamo wake wa kutoa kwenye suala hili ambapo amesema namna pekee ya Chadema kutoka katika tatizo hilo ni kutoa ufafanuzi wa wajumbe walioshiriki baraza kuu lililoketi Januari 22, 2025.
“Nataka kuamini kwamba zile rekodi za wajumbe waliokuwepo zilirekodiwa, naamini watakuwa nazo wakishazitoa hizo basi jibu la Mchome litakuwa limepatikana. Siyo lazima Chadema iweke kwenye vyombo vya habari wamjibu tu Mchome,” amesema.
“Kama ni kweli baraza kuu halikuwa na akidi inayotakiwa, basi inatakiwa taratibu zingine zifautwe za kuitisha baraza kuu jingine, kwa mazingira haya viongozi wataendelea kuwepo vitu watakavyovifanya vitakuwa batili,” amesema Mallya.
Mallya ametolea mfano kwamba katibu mkuu ana wajibu wa kuongoza vikao vya sekretarieti, kamati kuu kupitisha wagombea, sasa kama viongozi hao hawajapita kihalali huenda wagombea wasioteuliwa watawawekea mapingamizi.
“Kama malalamiko ya Mchome yana ukweli, Chadema irudi katika utaratibu unaotakiwa kwa kuitisha upya baraza kuu na wagombea wawe walewale,” amesema Mallya.
Mchome kwenye barua hiyo iliyonakiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, amesema ili akidi ya kikao kilichowaidhinisha vigogo hao kamilike, kilipaswa kuwa na wajumbe 309, badala ya 85 waliokuwepo ambao ni sawa asilimia 20.6.
Mchome, mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, amesema kwa mujibu wa katiba ya Chadema tolea la mwaka 2019 jumla ya wajumbe wa Baraza Kuu ni 412 na ili kikao kiwe halali na kufanya uamuzi kinatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua 309.
“Kikao cha Januari 22, 2025 kilikuwa na wajumbe 85, sawa na asilimia 20.6 ambao ndiyo wajumbe halali na ndio waliofanya uamuzi wa kuthibitishwa kwa wateuliwe hao kinyume cha katiba na kanuni za chama ibara 6.2.2 (a) na (b) ya katiba ya chama mwaka 2006 toleo la 2019.
“Ukumbini kulikuwa na jumla ya watu 236, wakiwemo wajumbe halali 85 na wasio halali 151, ambapo baadhi yao wameonekana katika picha za video jongefu wakipiga kura za kufanya uamuzi wa kuwathibitisha viongozi wa chama na wajumbe wa sekretarieti,” amedai Mchome.
Mchome ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga Mwanga mkoani Kilimanjaro na Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa, anadai kwa hali hiyo ni uthibitisho kwamba viongozi wa kitaifa na wajumbe wa kamati kuu watano waliopendekezwa na mwenyekiti wa Chadema na kuthibitishwa ni batili.
Kutokana na hilo, kada huyo ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu amesema viongozi wote waliothibitishwa kinyume cha utaratibu watangazwe kuwa batili, wasitumikie nafasi zao hadi uthibitishaji halali utakapofanyika.
Mchome ameongeza kuwa uamuzi wote uliofanywa na kamati kuu ambayo wajumbe hao wameshiriki ubatilishwe na Baraza Kuu liitishwe tena kufanya upya mchakato utakaohakikisha akidi inatimia.
“Hatuna malalamiko na walioteuliwa, ni watu sahihi, wengine tumeshawahi kufanya nao kazi kwa ukaribu, lakini tunahitaji wapite katika njia sahihi. Tunataka Baraza Kuu lijalo liwe na akidi ya asilimia 75 au zaidi ili kuwathibitisha kuwa wajumbe halali.
“Narudia, hatuna mashaka na walioteuliwa ni watu wazuri, lakini kwa sababu Chadema inasimamia katika misingi ya katiba, basi tuisimamie na kuilinda katiba yetu, ili kupata wajumbe halali. Naamini demokrasia itafuatwa katika hili,” amesema Mchome.