Same. Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, kwa kushirikiana na Shirika la Six Rivers Africa, imeanzisha mpango maalum wa kukabiliana na changamoto za uhifadhi zinazowakabili wanyamapori. Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kulinda afya za wanyamapori na kuhifadhi mazingira yao dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Tiba kwa Wanyamapori (Veterinary Support Project) leo, Februari 19, 2025, Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Steria Ndaga amesema mradi huu utaongeza uwezo wa kuhifadhi na kulinda afya za wanyamapori katika hifadhi hiyo.
Kwa niaba ya Kamishna Ndaga, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi (Tanapa), Sonia Lyimo amesema mradi huo utatoa msaada wa haraka kwa wanyamapori wanaohitaji huduma za afya, ikiwa ni pamoja na matibabu kwa walioumia na udhibiti wa magonjwa yanayoweza kuenea.
“Wanyamapori wanakumbana na changamoto nyingi, zikiwemo magonjwa, migogoro na binadamu, ujangili na mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu utachangia kulinda afya zao na kuwawezesha kuendelea kuishi katika mazingira bora,” amesema Kamishna Lyimo.
Aidha, amebainisha kuwa mradi huo pia utasaidia kufanya tafiti kuhusu magonjwa yanayoweza kuwa hatari kwa wanyamapori na kuweka mikakati ya kuzuia milipuko ya magonjwa.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amesema mradi huo utachangia mafanikio endelevu katika hifadhi hiyo, akisisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kulinda urithi wa asili kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
“Tuna matumaini kuwa ushirikiano kati ya Six Rivers Africa, Shirika la Elephant Conservation Organization (ECO), na Tanapa utaleta mabadiliko makubwa na kuimarisha huduma za wanyamapori hapa Mkomazi,” amesema Mgeni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Six Rivers Africa, Brandon Kemp kwa upande wake amesema msaada wa gari na vifaa tiba waliotoa ni sehemu ya juhudi za kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kulinda rasilimali za uhifadhi.
“Huu ni mchango wetu katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya hifadhi za taifa na kuboresha huduma kwa wanyamapori,” amesema Kemp.
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Frank Sangarufu amesema mradi huo umegharimu zaidi ya Sh140 milioni na unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanapa, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na Shirika la Six Rivers Africa