Morogoro. Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), ambayo ni taasisi chini ya Wizara ya Nishati, imepanga kuendesha mnada wa vitalu 26 vya utafutaji mafuta na gesi asilia, kati ya hivyo 23 vipo katika Bahari ya Hindi na vitatu vikiwa katika Ziwa Tanganyika.
Lengo kuu ni kuvutia wawekezaji na kuimarisha juhudi za utafutaji wa nishati hii muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa mnada huo utafanyika Machi 5, 2025, sambamba na kongamano la mafuta na gesi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, litakalofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema minada iliyofanyika katika miaka ya 2000, 2004, 2008, na 2013 ilisababisha kugundulika kwa gesi asilia inayotumika maeneo mbalimbali nchini na kwamba hadi sasa, Tanzania ina gesi asilia yenye futi za ujazo trilioni 57.54.
“Temejipa muda wa miezi tisa mpaka mwisho wa mwaka 2025 tutakuwa tumepata wale ambao wamevutiwa kuja kuwekeza, na ugunduzi wa gesi unakwenda sambamba na kampeni ya Mkuu wa nchi Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia Afrika,” amesema Mhandisi Sangweni.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesisitiza kuwa mnada huu utahamasisha uwekezaji zaidi na kuongeza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, jambo litakaloongeza nafasi za ajira na mapato kwa taifa.
Ameongeza kuwa sekta ya nishati ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Kapinga pia ameeleza kuwa, kupitia kuvutia wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, Tanzania itaongeza uzalishaji wa rasilimali hii muhimu, hivyo kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.
“Tukifanikiwa kuvutia wawekezaji kwenye vitaru hivyo shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zitaongezeka pia kuongeza uwezekano wa uzalishaji kwa muda mrefu tulikuwa tunazungumzia ugunduzi wa gesi asilia yenye futi za ujazo trilioni 57.54, ni wakati sasa wa kwenda zaidi ili kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Kapinga.