CHAMA cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kimezindua rasmi Maonesho na Tuzo kwa Wanawake Wajasiriamali kwa msimu wa tano, pamoja na kutangaza mfululizo wa matukio yatakayosherehekea Siku ya Wanawake Duniani 2025. Matukio haya yatafanyika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, yakilenga kuonyesha mafanikio ya wanawake katika sekta ya biashara na kukuza usawa wa kijinsia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza, ameeleza kuwa maadhimisho haya yanaenda sambamba na kutimiza miaka 30 ya Mpango wa Beijing, hatua muhimu katika harakati za kuwawezesha wanawake duniani kote.
“TWCC ni chama kinachoongoza katika kuwezesha wanawake kiuchumi nchini, kikiwa na wanachama wa moja kwa moja wapatao 20,000. Pia, mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 20 tangu chama chetu kilipoanzishwa, hivyo tunajivunia mafanikio makubwa tuliyopata.” Amesema Mwajuma .
TWCC pia imetangaza kuanzisha idara maalum inayoshughulikia masuala ya vijana wa kike na wa kiume, kuhakikisha wanapata fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi kwa usawa.
Mfululizo wa Matukio Muhimu
1. Kongamano la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi litafanyika Pemba (Februari 22, 2025)
Kongamano hili linalenga kuwapa wanawake maarifa na fursa za kukuza biashara zao kwa kuimarisha ushirikiano na wawekezaji.
2. Usiku wa Mwanamke Mfanyabiashara Utafanyika Unguja, Zanzibar (Februari 26, 2025)
Tukio hili litahusisha utoaji wa tuzo maalum kwa wanawake waliofanikiwa katika sekta ya ujasiriamali, uongozi na uvumbuzi.
3. Maonesho ya Wanawake na Vijana yatafanyika Mlimani City, Dar es Salaam (Machi 1-5, 2025)
Maonesho haya yatawaleta pamoja wanawake na vijana wajasiriamali kutoka sekta mbalimbali kuonyesha bidhaa na huduma zao.
Taasisi kama BRELA, TRA, GCLA, na UTT Amis zitashiriki kutoa huduma na mwongozo wa biashara. Mwisho wa kujisajili kushiriki ni Februari 26, 2025.
4. Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani yatafanyika jijini Arusha (Machi 8, 2025)
TWCC itashiriki maadhimisho haya ambapo wanawake watajumuika kusherehekea mafanikio yao na kujadili changamoto wanazokabiliana nazo.
5. Tuzo za Viwanda na Biashara kwa Wanawake Wajasiriamali zitafanyika The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam (Machi 22, 2025)
Tuzo hizi zitatolewa kwa wanawake waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya viwanda na biashara. Maombi ya kushiriki yamefunguliwa kuanzia leo Februari 19 na yanatarajiwa kufungwa Machi 10, 2025.
“Maombi ya Kushiriki Tuzo:
Wanawake wanaotaka kushiriki katika Tuzo hizi wanahimizwa kujaza fomu za maombi au kupendekezwa na watu wanaowafahamu na kuwasilisha majina yao kupitia mifumo ambayo tumeweka.”
Kamati maalum itachuja majina kulingana na vigezo vya tuzo. Mwisho wa kutuma maombi ni Machi 10, 2025.” Amesema Mkurugenzi Mtendaji, TWCC.
TWCC inatoa wito kwa wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika matukio haya ili kupata fursa za mtandao wa kibiashara, ushauri, na uwezeshaji wa kifedha.
“Wanawake ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania. Ni wakati wa kuwekeza katika ubunifu wao na kuhakikisha wanapata nafasi sawa katika biashara na viwanda,” ameongeza Mercy Sila ambaye ni rais wa TWCC
TWCC inatoa wito kwa wanawake, vijana, viongozi wa biashara, na wanajamii wote kushiriki katika sherehe hizi na kutumia sauti zao kuhamasisha ujumbe wa uwezeshaji, usawa na ushirikishwaji wa kijinsia. Ili kushiriki katika matukio haya, washiriki wanahimizwa kutufuatilia mitandao ya kijamii ya TWCC na kutumia hashtag rasmi za kampeni: #30YearsOfBeijing, #IWD2025, #WomenEmpowermentTanzania, na #Beijing30.