Sh260 za Benki ya Dunia kuboresha sekta ya afya

Unguja. Benki ya Dunia (WB) imeipatia Zanzibar Dola za Marekani 100 milioni (Sh260 bilioni) kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya kisiwani hapa.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo Kanda ya Kusini Mwa Afrika, Milena Stefanova ametoa kauli hiyo leo Februari 18, 2025 alipozungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, Ikulu Zanzibar.

Amesema benki hiyo inaridhika na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya  Zanzibar kuimarisha huduma za Afya na kuahidi kuendelea na misaada kwa ustawi wa watu wake.

Katika mazungumzo hayo, Dk Mwinyi ameishukuru Benki ya Dunia kwa msaada huo aliosema ni kichocheo cha mabadiliko makubwa na kuimarika kwa miundombinu ya matibabu.

Hata hivyo, amesema licha ya Serikali kufanikiwa kujenga Hospitali za Wilaya na vituo vya Afya, bado zipo changamoto zinazohitaji utatuzi wa haraka na kuiagiza Wizara ya Afya kutumia fedha hizo vizuri kwa kuimarisha miundombinu ya afya, mafunzo kwa watendaji na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu.

“Serikali ina malengo mahususi ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo bora cha matibabu kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, naipongeza Benki ya Dunia kuendelee kutuunga mkono,” amesema.

Rais Mwinyi ameishauri Wizara ya Afya kufanya kazi kwa ukaribu na mtaalamu wa Benki ya Dunia kutafuta wakandarasi wazuri na weledi kusimamia ujenzi wa miundombinu ya matibabu ili msaada huo wa fedha utumike kwa kwa ufanisi na kuleta mabadiliko yanayostahiki katika sekta ya afya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui ameeleza kuwa wizara hiyo inajipanga vema kuhakikisha fedha hizo zinaenda kutumika kufanikisha lengo la kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha pekee cha utalii wa tiba na matibabu na mafunzo ya afya, kama zilivyo nchi za India na Thailand.

Related Posts