Mfumo waja kusajili watumishi kada ya ununuzi

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekiri kuwepo kwa changamoto nyingi zinazowakabili watumishi wa kada ya ununuzi katika kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kukosekana kwa kanzidata yao.

Changamoto nyingine ni uzingatiwaji wa ithibati ya taaluma ya ununuzi, uwezo mdogo wa baadhi ya wataalamu wa kada hiyo wanoendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na uadilifu wenye shaka wa baadhi yao.

Hayo, yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman leo Jumatano, Februari 19, 2025 katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi.

Dk Mohammed alitaka kufahamu mkakati wa Serikali juu ya kutathmini upya masilahi ya watumishi wa fani ya ununuzi ili kuwaongezea motisha ya kufanya kazi na kwa mujibu wa kanzi data ni watumishi wangapi wa fani ya ununuzi wameajiriwa Zanzibar na katika madaraja gani.

Akijenga hoja yake, amesema kada ya ununuzi ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi, lakini bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa kanzidata ya wataalamu wa manunuzi na upungufu wa masilahi kwa kada hiyo.

Akijibu swali hilo, Dk Mkuya amesema katika kutatua changamoto hizo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha mfumo wa usajili wa watumishi wa kada ya ununuzi, utakaowezesha watumishi wa kada ya hiyo kujisajili na kuhifadhi taarifa zao.

“Pia, Serikali ipo katika hatua za kufanya marekebisho ya Sheria ya taasisi ya wakaguzi, wahasibu na washauri elekezi wa kodi kwa lengo la kusimamia taaluma ya ununuzi kwa kuzingatia weledi wa kitaaluma na ithibati, kama zilivyo taaluma nyingine,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema tayari Serikali imeandaa rasimu ya sheria ya ununuzi na inakusudia kufuta sheria ya ununuzi na uondoaji wa mali za umma kwa lengo la kupunguza changamoto zinazowakabili watendaji wa kada ya ununuzi.

Amesema, Serikali kupitia ofisi hiyo ilifanya jitihada ya kukusanya taarifa za watumishi hao katika taasisi zote za Serikali ambapo hadi kufikia Desemba, mwaka jana ilibainika kuwa jumla ya watumishi 727 wa kada ya ununuzi wameajiriwa na Serikali.

Amesema kati ya watumishi hao, watumishi 571 wameajiriwa Unguja na watumishi 156 wameajiriwa kwa upande wa Pemba.

Hivyo, amesisitiza kuwa Serikali kupitia ofisi hiyo inakusudia kuandaa muundo wa utumishi wa kada ya ununuzi ambao utawezesha kuangalia majukumu, madaraja na masilahi ya watumishi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Related Posts