Rekodi ya ugenini Prisons yamtesa Josiah

KOCHA wa Tanzania Prisons, Amani Josiah amesema ana kazi ya kufanya katika kikosi hicho ili kukifanya kilete ushindani msimu huu, huku akidai rekodi ya michezo ya ugenini inamtesa, jambo analotaka kulifanyia marekebisho haraka.

Kauli ya Amani inajiri baada ya timu hiyo kuchapwa juzi mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, na kufikisha michezo yake 10 ya ugenini msimu huu bila kuonja ladha ya ushindi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Amani amesema changamoto kubwa ni maeneo yote mawili kuanzia beki na la ushambuliaji ambalo kwa michezo ya hivi karibuni imekuwa shida kwao, ingawa anaendelea kupambana ili kurekebisha hali iliyopo.

“Mchezo na Dodoma Jiji tungeweza kuimaliza mechi kipindi cha kwanza ila tulishindwa kutumia nafasi tulizopata, pia eneo la ulinzi tulifanya makosa ambayo kiukomavu tusingeyafanya, inauma kama kocha ila tunaendelea kurekebisha hali iliyopo,” amesema.

Josiah alijiunga na Prisons Januari 2, mwaka huu akichukua nafasi ya Mbwana Makata aliyetimuliwa Desemba 28, mwaka jana, ambapo tangu achukue timu hiyo ameiongoza michezo minne ya Ligi Kuu na kati yake ameshinda mmoja tu na kuchapwa mitatu.

Makata alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu, sare mitano na kupoteza saba, ambapo alikiacha kikiwa nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi 11.

Baada ya hapo akaiongoza kocha msaidizi wa timu hiyo, Shaaban Mtupa na katika michezo miwili alianza na kichapo cha mabao 4-0, dhidi ya Yanga ugenini Desemba 22, 2024 na ushindi finyu wa bao 1-0, mbele ya Pamba Jiji nyumbani Desemba 26, 2024.

Josiah alijiunga na kikosi hicho akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship na hadi sasa timu hiyo imecheza michezo 10 ya ugenini bila kuonja ladha ya ushindi, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao matatu tu na kuruhusu 14.

Kiujumla kikosi hicho kimecheza michezo 20 ya Ligi Kuu hadi sasa ambapo kati ya hiyo kimeshinda minne tu, sare mitano na kupoteza 11, ambapo safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 11 na kuruhusu 25, ikishika nafasi ya 14 na pointi zake 17.

Pamba Jiji 0-0 TZ Prisons

Mashujaa FC 0-0 TZ Prisons

Tabora United 0-0 TZ Prisons

Namungo FC 1-0 TZ Prisons

Coastal Union 2-1 TZ Prisons

Kagera Sugar 0-0 TZ Prisons

Dodoma Jiji 3-2 TZ Prisons

Related Posts