Washirika wa ndani wasakwa ujenzi hoteli ya nyota tano Serengeti

Dar es Salaam. Katika juhudi za kubadilisha taswira ya utalii wa Tanzania, Kampuni ya Maendeleo Hospitality Ventures (MHV) inayosimamiwa na kundi la wawekezaji kutoka Marekani, imetangaza mpango wa kujenga hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano katika Kijiji cha Robanda, karibu na Lango la Fort Ikoma, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Lengo kuu la mradi huo inaelezwa ni kuimarisha sifa ya Tanzania kama mojawapo ya maeneo bora ya utalii duniani, kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka eneo hilo, pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwekezaji huyo mapema leo Jumatano Februari 19, 2025, hoteli hiyo itatoa huduma za kimataifa, huku wageni wakipata fursa ya kipekee ya kutazama wanyamapori na kufurahia uzuri wa asili wa Serengeti.

Aidha, mradi huo utazingatia utalii endelevu kwa kuenzi urithi wa utamaduni wa Tanzania na kuhakikisha kuwa jamii za eneo hilo zinanufaika kiuchumi.

Mwenyekiti wa MHV, Rishen Patel ameeleza furaha yake kuhusu mradi huo, akisema: “Maono yetu ni kubadilisha sekta ya hoteli nchini Tanzania kwa kuanzisha hoteli za kifahari zinazoakisi urithi wa utamaduni na mandhari ya kipekee. Serengeti, inayojulikana kwa wanyamapori wake wa ajabu na Uhamaji Mkubwa wa Wanyama, ni eneo sahihi kwa kuanza safari hii.”

Patel amebainisha ukuaji mkubwa wa sekta ya utalii wa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni, akitaja kuwa idadi ya watalii ilifikia milioni 1.8 mwaka 2023, na kuingiza mapato ya Dola bilioni 3.37 za Marekani.

Takwimu za awali za Agosti 2024, zinaonyesha ongezeko la watalii wa kimataifa hadi kufikia zaidi ya milioni 2, huku mapato yakitarajiwa kufikia Dola 3.5 bilioni.

“Mwelekeo huu unaonyesha kuvutia kwa Tanzania kimataifa kama kivutio cha utalii, huku juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na kuendeleza utalii endelevu zikiendelea kuzaa matunda,” amesema Patel.

Katika kufanikisha mpango huo, MHV imeingia makubaliano na kampuni ya CORE Securities Limited, ambayo ni mwanachama wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ili kupata mtaji kupitia Ofa ya Umma ya Kwanza (IPO).

MHV inatarajia kuuza asilimia 31 ya hisa kwa wawekezaji wa Kitanzania, asilimia 3 kwa jamii za eneo husika na asilimia 2 kwa wafanyakazi wa mradi huo, hatua inayolenga kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika uwekezaji huo.

“Tunaamini huu ni wakati mwafaka kwa uzinduzi wa mradi huu wa kimkakati, ambao utaongeza ubora wa huduma za malazi nchini. Hoteli yetu katika Serengeti ni hatua ya kwanza, lakini tunapanga miradi mingine Zanzibar, Ngorongoro na Kilimanjaro, tukilenga kuvutia wageni kutoka duniani kote,” amesema Patel.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, George Fumbuka;

“Tuko katika hatua za mwisho za mazungumzo ili kuunda Timu ya Ushauri itakayosaidia kupata vibali muhimu vya serikali kwa ajili ya uzinduzi wa Ofa ya Umma ifikapo mwezi ujao.”

Fumbuka amesema wana matumaini kuwa hoteli hiyo ya kifahari itazinduliwa rasmi Julai 2025.

“Tunajivunia kushiriki katika mradi huu wa kimkakati unaoungwa mkono na wawekezaji wenye uzoefu wa kimataifa. Hii ni fursa adhimu kwa Watanzania kunufaika kupitia umiliki wa hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam,” amesema.

Related Posts