Dar es Salaam. Siku 90 zimetolewa kwa vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo zahanati kuhakikisha vinakuwa na sehemu maalumu za kuchomea taka hatarishi, watakaokiuka hilo wanaweza kusitishiwa utoaji huduma.
Wasiokuwa na maeneo hayo wametakiwa kuhakikisha taka zao zinakusanywa na makandarasi waliosajiliwa kufanya kazi hiyo na si wanaozoa taka majumbani.
Agizo hilo limetolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ,baada ya kubainika kuwapo kwa ongezeko la taka hatarishi zinazotupwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufukweni.
Taka hatarishi zinazotokana na huduma za afya ni pamoja na zitokanazo na tiba mbalimbali, zenye mgando wa damu, sehemu za mwili wa binadamu zilizoondolewa kwa sababu za magonjwa, zenye viambukizi vya magonjwa, vitu vyenye ncha kali (sindano, nyembe).
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Mei 16, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC, Hamadu Kissiwa wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Kissiwa amesema taka hatarishi zinazotokana na huduma za afya zinaweza kusababisha milipuko ya magonjwa na vifo iwapo taratibu za ukusanyaji, utunzaji na uteketezaji hautazingatiwa.
Amesema athari hizo hazitaishia kwa binadamu pekee bali utupaji wake holela huweza kuathiri viumbe hai na mazingira.
“Ili kuzuia na kudhibiti athari zitokanazo na taka hizo mfumo mahususi unaofanya kazi kwa ufanisi wa kuzidhibiti unapaswa ufuatwe kama ulivyobainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 na Kanuni za udhibiti wa taka hatarishi za mwaka 2021,” alisema Kissiwa.
Mbali na uwepo wa sheria hiyo, Kissiwa amesema baadhi ya watoa huduma wamekuwa hawafuati mwongozo, utaratibu na sheria zilizowekwa na Wizara ya Afya kwa kuwapa kazi watu wasioidhinishwa kukusanya taka hizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi (Aphta), Dk Egina Makwabe, amesema wakati mwingine mkanganyiko huo unasababishwa na halmashauri ambazo kuna hivyo vituo vya afya.
Amesema ni kweli miongozo inawataka kuwa na sehemu ya kuteketeza taka hatarishi au kuingia mkataba na wakandarasi au hospitali zilizo na maeneo hayo, lakini wakati huo pia halmashauri zinadai jukumu la kukusanya taka liko chini yao na wanapaswa kulipia tozo.
“Nafikiri suluhu ni wao NEMC kuwaambia halmashauri kuacha kukusanya taka hatarishi kwa sababu si wajibu wao, pia siamini kama halmashauri zina sehemu za kuchomea taka hizo,” amesema Makwabe.
Katika hatua nyingine, Kissima amesema Mei mwaka huu, Baraza lilipewa taarifa ya utupaji holela wa taka za aina hiyo katika maeneo ya Kibaha, Mkoa wa Pwani na kweli walikuta zikienda kutupwa, nyingine zikichomwa bila kuteketea jambo linalochochea uchafuaji wa mazingira na kuhatarisha afya za wananchi.
Amesema ongezeko hilo pia linazidi kuonekana kwani hata vijana wanaofanya usafi maeneo ya fukwe wamekuwa wakikusanya taka hizo, hali inayohashiria kuwepo kwa utupaji holela kwenye vyanzo vya maji hasa baharini na kwenye mito.
“Unakutana na taka zinazotokana na huduma za afya, utashangaa hizi sindano zimekujaje ufukweni, wakati huku watu wanaogelea, viwembe vilivyotumika katika utoaji huduma ambavyo vikimkata mtu huweza kusambaza magonjwa ikiwa aliyehudumiwa alikuwa na ugonjwa wa kuambukiza,” alisema Kissiwa.
Kufuatia suala hilo, NEMC imezieleza mamlaka za udhibiti nchini zinazoshughulikia usimamizi wa taka zinazotokana na huduma za afya kuhakikisha watoa huduma za afya kote nchini wanafuata miongozo iliyowekwa.
Miongozo hiyo ni ile ya wizara pamoja na masharti ya Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa taka hatarishi za Mwaka, 2021 ikiwemo kuwa na miundombinu ya usimamizi wa taka zao pamoja na vibali vilivyotolewa na Wizara ya Afya.
“Adhabu kali zitatolewa kwa wote ambao hawataweza kutekeleza agizo hili ikiwemo kufungiwa vituo vyao mpaka watakapoweka miundombinu madhubuti ya uhifadhi, usafirishaji na uteketezaji wa taka zao,” alisema Kissiwa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utu na Mazingira (HUDEFO), Sara Pima amesema katika kipindi cha mwaka jana na mwaka juzi wamekuwa wakishuhudia ongezeko la taka hatarishi zinazotupwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufukweni.
Alisema kupitia kampeni wanazofanya za usafishaji wa mazingira, wamekuwa wakichukua takwimu za taka wanazokusanya na wakati mwingine wanakutana hadi na dripu.
“Tunakutana na dripu, chupa za dawa wakati mwingine tunajaza hadi ndoo tatu, zinaleta hofu, zinaathiri mazingira yetu,” alisema Sarah.
Amesema katika utekelezaji wa kampeni hizo, wamekuwa wakiwashirikisha NEMC jambo ambalo huwafanya kushuhudia kile kinachofanyika.
“Tunashukuru kwa sababu tumechagiza utolewaji wa tamko hili, mbali na NEMC tuliandika barua hata Wizara ya Afya kuwaeleza hali iliyopo ili waone namna gani wanaweza kusaidia katika kutatua tatizo hilo,” amesema Sarah.