TAMASHA LA KUMBUKUMBU YA VITA VYA MAJIMAJI KUFANYIKA RUVUMA, WANANCHI KUELIMISHWA KUHUSU HISTORIA NA UTAMADUNI

 NA BELINDA JOSEPH, RUVUMA.

Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi 27 Februari 2025, na litahusisha shughuli mbalimbali za kiutamaduni na kihistoria zinazolenga kuenzi mashujaa waliopigana vita hivyo,  Tamasha hilo litafanyika mkoani Ruvuma, ambapo wananchi watapata fursa ya kujifunza kuhusu historia ya vita vya Majimaji na umuhimu wa utamaduni wa Makabila mbalimbali ya Mkoa huo.

Kaimu Muhifadhi wa Makumbusho ya Majimaji, Bi. Rose Kangu, amesema kuwa uzinduzi wa Tamasha hilo unatarajiwa kufanyika tarehe 23 Februari, Uzinduzi huu utakuwa na biashara, maonyesho ya bidhaa mbalimbali kutoka kwa wadau wa utamaduni, maliasili na utalii, Wananchi na wageni wanakaribishwa kushiriki ili kujionea bidhaa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika siku hiyo.

Pia litatoa fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu tamaduni za watu wa Mkoa wa Ruvuma, ikiwemo nyimbo za asili na ngoma za kabila la watu wa Mkoa huo ambapo tarehe 24 Februari, kutakuwa na mashindano ya ngoma za asili, kutoka  kila kabila katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma, ambalo litaonyesha ngoma zake za kitamaduni, na Washindi watatu wa mashindano hayo watapata nafasi ya kutumbuiza kwenye kilele cha tamasha. Aidha kutakuwa na mashindano ya vyakula vya asili na dawa za asili, vitakavyowakutanisha wananchi na utamaduni wa kiasili.

Amesema Siku ya Tarehe 25 Februari, kutakuwa na mdahalo mkubwa utakaofanyika katika Ukumbi wa shule ya Dkt. Samia SuluhubHassan Wilayani Namtumbo, Mdahalo utakaohusisha masuala ya utamaduni wa makabila yanayopatikana Namtumbo na wananchi wote wanahamasishwa kuhudhuria ili kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu tamaduni za makabila hayo.

Tarehe 26 Februari itakuwa ni siku maalumu kwa ajili ya Wangoni maarufu kama “Ngoni Day.” Katika siku hii, Wangoni watakusanyika katika eneo la Maposeni, ambako ilikuwa Ikulu ya Chifu wa Wangoni Mputa Gama, na mwenyeji wao siku hiyo atakuwa ni Inkosi Emmanuel Gama atakuwa mgeni rasmi, imeelezwa kuwa watu watajifunza masuala mbalimbali yanayohusu Wangoni, ikiwemo chakula cha asili na desturi zao.

Kilele cha Tamasha  kitatimia tarehe 27 Februari, ambapo wananchi wote wanakaribishwa kushiriki katika hafla ya kumuwaenzi mashujaa wa Vita vya Majimaji, Hii itakuwa ni siku ya kuadhimisha kwa pamoja na kuenzi michango ya mashujaa waliopigania uhuru wa nchi yetu na waliouawa na wakoloni wakati wakipigana vita hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea James Mgego, ametoa rai kwa Chama hicho kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kumbukizi hizi muhimu na kupitia tamasha hilo, wananchi watapata fursa ya kujifunza na kujivunia historia ya taifa lao, huku wakizingatia umuhimu wa kuenzi utamaduni na mashujaa waliopigania uhuru. 

Mgego amesisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi kimejipanga vizuri kushirikiana na wananchi katika sherehe hizo ambazo zitajumuisha shughuli mbalimbali za kuvutia, na hivyo, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuadhimisha kumbukizi hii kwa pamoja.

Related Posts