Dar es Salaam. Kama ulidhani kusitishwa kwa misaada ya maendeleo nje ya Marekani, kunawagusa wafanyakazi na walio mstari wa mbele pekee, umekosea.
Kukosekana kwa misaada hiyo, kunawaamsha wadau wakisema itarajiwe ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, magonjwa ya ngono, mimba za utotoni, vifo vitokanavyo na uzazi.
Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) lilikuwa na mnyororo mpana katika kushughulikia afya, hasa afya ya uzazi ambapo vijana na vijana balehe zaidi ya milioni 21.3 walinufaika kwa namna moja ama nyingine nchini.
Elimu kuhusu afya ya uzazi iliwafikia vijana moja kwa moja kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Dreams iliyosaidia vijana zaidi 70,000 nchini, Sharp Project ambayo iliwafikia maelfu ya vijana katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Manyara.
Kwa kiasi kikubwa miradi hii ilisaidia kupunguza maambukizi mapya ya VVU, mimba za utotoni, uzazi salama na kusaidia upatikanaji na mahitaji ya bidhaa na huduma za afya ya uzazi, huku ikiweka mkazo maalum kwa wasichana balehe wenye umri wa kati ya miaka 10-19.
Miongoni mwa vijana kinara na mwelimisha rika, Hadija Maganga amesema upatikanaji wa huduma na bidhaa za afya ya uzazi kwa vijana na wanawake wadogo nchini, ni muhimu kwa ustawi wa jamii hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya sera za misaada ya kigeni.
Amesema wasichana wadogo balehe wanaathirika sana na kukosekana kwa taarifa, hasa zihusuzo afya ya uzazi.
“Kipindi hiki tunaposikia taarifa misaada inakwenda kukoma, kama wadau tunabaki tunajiuliza hali itakuwaje? Unapoongea na vijana balehe wanaonyesha wazi kuna usiri miongoni mwa familia, hawazungumzi nao wazi kuhusu masuala ya afya ya uzazi.
“Wengi wanatafuta taarifa wenyewe, waelimisha rika walisaidia kwa kiasi kikubwa, hatuna hakika iwapo serikali itaweza kufanya yale yaliyofanywa na USAID,” amesema.
Ameongeza, Serikali inapaswa kutafuta utatuzi wa afya ya uzazi hasa kwa vijana balehe, “Serikali haiwezi msisitizo kama ambavyo miradi ya Sharp inafanya kuhakikisha vijana wanahusishwa.”
Mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi nchini, Denis Bwana amesema kupatikana kwa hizi huduma, ni jibu sahihi la kukabiliana na mimba za utotoni kwa mikoa yenye namba kubwa ikiwemo Manyara na morogoro hasa upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.
“Huduma za afya ya uzazi ni pamoja na masuala ya uzazi wa mpango, matumizi ya kondomu na vifaa tiba vya aina hiyo, vinachangia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni,” amesema.
Bwana amesema mimba za utotoni zina uhusiano wa moja kwa moja na ndoa za utotoni, sababu huduma za afya ya uzazi ni pamoja na taarifa sahihi kufika, inayosaidia mabinti kufanya maamuzi yao.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, taarifa hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kushusha maambukizi ya VVU kwa sababu huduma za uzazi huambatana na masuala ya uzazi wa mpango, ambayo ni pamoja na matumizi ya kondomu.
“Ndani yake kulikuwa na uchechemuzi mbalimbali wa masuala ya afya, kuna watoa huduma ngazi ya jamii walikuwa wanapita kutoa elimu kwa makundi rika, kupitia program zilizokuwa chini ya ufadhili wa USAID waliokuwa wanasaidia kukabiliana na changamoto hizi.
“Kusimama kwa hii miradi hawa vijana, taarifa nyingi hawawezi kupata. Programu zilizobaki hazitoshi na hata zilipokuwepo za USAID, bado hazikutosheleza tafsiri yake ni kwamba vijana watakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi, mimba za utotoni zitaongezeka, ndoa za utotoni,” amesema Bwana.
Amesema mimba nyingi za utotoni zinachangia vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, kwakuwa mtoto atazaliwa na mama ambaye hayupo tayari kiuchumi, kibaolojia, kisaikolojia na kiakili.
Bwana amesema madhara yatakayokuwepo sasa, yanaweza kuathiri vizazi vijavyo.
Mratibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Modest Pesha amesema bado ni mapema kutathmini athari ndani ya kipindi kifupi cha mabadiliko ya sera za misaada ya kigeni kwa makundi ya vijana.
Mchungaji Pesha amesema upatikanaji wa huduma na bidhaa za afya ya uzazi kwa makundi hayo ni muhimu katika kulenga maambukizi ya VVU, mimba za utotoni, mimba zisizotarajiwa, ndoa za kulazimishwa kama matokeo ya mimba za utotoni.
Pia amesema zitasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto hasa kwa wanaojifungua katika umri mdogo ili kufikia malengo ya SDG, migogoro katika kaya na jamii nzima kwa ujumla pamoja na kusambaratika kwa familia.
“Huduma juu ya afya ya uzazi ni pamoja na utoaji wa elimu kuanzia ngazi ya familia kwa wazazi kuvunja ukimya, pamoja na taasisi za dini kuhusisha elimu ya afya ya uzazi katika mafundisho yao,” amesema.
Mchungaji Pesha amesisitiza upatikanaji wa bidhaa uzingatie maadili, misingi na mafundisho ya kiimani, umri na matumizi sahihi ili kuepusha madhara zaidi.
Hata hivyo wadau wametoa wito kwa serikali, kuhakikisha inatimiza mikataba mbalimbali ukiwemo ule wa Abuja unaozitaka nchi kuhakikisha zinatenga asilimia 15 ya bajeti yake kushughulikia afya.
“Tumefanya kitu kizuri katika huduma ya mama na mtoto, lakini mifumo yetu ya afya tukitegemea misaada zaidi tutakwama. Kwakuwa hatukuwekeza kushughulikia afya, misaada yote ya nje kutoka Marekani ni fedha ndogo lakini angalia athari yake kwetu.
“Hapa ndiyo tuone umuhimu wa kodi zetu, uwekezaji wakwanza iwe kwenye afya, pili elimu na miundombinu. Afya ya uzazi imetetereka zaidi kwa sasa. Lazima tuwe na mifumo ya afya ambayo ni endelevu.”
Bwana anasema nchi inatakiwa kujitathmini misaada kupitia USAID iliitumiaje, ni wataalamu wangapi walitengenezwa na wanaweza kuifanyia nini nchi kwa sasa na kwamba lazima tuwe wawajibikaji.
“Ili kuweza kurejesha hizi huduma, lazima tulegeze masharti kuwe na mazingira rafiki, kodi, sera zetu zisipokuwa rafiki watu wataacha lazima tuangalie sera zetu upya ili sekta binafsi ziweze kuwekeza kwenye afya,” amesema.
Bwana amesisitiza kuwa ni muhimu kuwa wabunifu katika kuwekeza katika sekta ya afya.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema suala hilo linashughulikiwa na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambao wanaangalia hizo huduma zote na baada ya kuzifanyia uchambuzi taarifa itatolewa.
Hata hivyo amesema hakuna huduma iliyosimama, zinaendelea zikiwa zimeunganishwa kwa pamoja, pia dawa za ARV na nyinginezo wanapata.
Hata hivyo Dk Magembe amesema kundi la asasi za kiraia ambao walikuwa wanatoa elimu kwa vijana kuhusu mimba za utotoni na elimu ya afya ya uzazi zinasimama.
“Tunaangalia lazima ziendelee. Kwa sasa watoa huduma ngazi ya jamii wapo wanalipwa na serikali na wanatoa huduma jumuishi zote kuanzia elimu kwa umma, huduma za kifua kikuu, malaria, uzazi wa mpango, mimba za utotoni.
“Tumetengeneza mpango jumuishi mtoa huduma ngazi ya jamii amewezeshwa kwa mafunzo maalum, ni kati ya mikakati ambayo itatupa uendelevu wa zile huduma, wanatoa pia elimu. Hili linafanyiwa kazi na timu ndani ya serikali si Wizara ya Afya pekee,” amesema.
Dk Magembe amesisitiza kuwa huduma zote za msingi hasa zinazohusu matibabu na tiba zinaendelea kama kawaida.