Tanzania inaweza kujifunza haya kwa watoto wa Finland

Fikiria watoto wenye umri wa miaka 13 tayari wanafunzwa kuhusu masuala ya fedha, kuweka akiba, bajeti, au hata jinsi ya kuendesha biashara ndogo. Nchi ya Finland imebuni programu maalumu kwa vitendo, kwa Kifini Yrityskylä (Mji wa Biashara) kwa ajili ya kujifunza masuala ya kifedha kwa watoto mashuleni na imeleta matokeo mazuri.

Programu ya Yrityskylä, inahusisha wanafunzi wenye umri wa miaka 13 hadi 15, ambao wanashiriki kwa pamoja kujifunza masuala ya kifedha. Inaanza kwa kujifunza dhana za kifedha darasani kulingana na ratiba iliyopangwa, na kisha kushiriki katika zoezi la mfano linalofanana na maisha halisi, ambalo ni kama igizo la maisha ya kila siku katika mji au kijiji, wanafunzi wanaonesha ubunifu kwa wanachokipenda, mfano kubuni biashara, kuandaa bajeti, kuuza bidhaa, kufanya manunuzi, kupatana bei, na kufanya maamuzi mengine ya kifedha.

Wanacheza nafasi za wafanyakazi, wamiliki wa biashara, maofisa wa umma, na wakaazi wa mji, wakifanya maamuzi ya kifedha katika mazingira yanayofanana na maisha halisi. Zoezi lote hilo linasimamiwa na walimu wenye mafunzo maalumu ya ufundishaji elimu ya fedha.

Vilevile, wanafunzi pia wanajifunza changamoto za kifedha zinazoweza kutokea ikiwa mtu hatakuwa na utaratibu mzuri wa kujiongoza, matumizi ya israfu, kutokuwa na bajeti inaweza kumweka mtu katika hali ngumu kifedha, na mengine.

Mfumo huu wa mafunzo unakuza uelewa mpana wa uwajibikaji wa kifedha na kiuchumi tangu wakiwa na umri mdogo. Programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya halmashauri za miji, sekta binafsi, na taasisi za elimu. Kwa mujibu wa tovuti ya programu hiyo, asilimia 75 ya watoto wa Kifini katika umri huu wanashiriki programu hiyo.

Tathmini ya ripoti ya ufuatiliaji kuhusu elimu ya fedha kwa nchi za OECD, inaonyesha vijana wa Kifini wa miaka 15 kuwa miongoni mwa walio na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya kifedha duniani.

Kuna mambo kadhaa tunaweza kung’amua kutoka kwenye programu hiyo.

Kwanza, mbinu ya kujifunza kwa vitendo hufanya somo la fedha kuwa la kuvutia na rahisi, hasa kwa watoto. Elimu ya fedha inageuka kuwa zoezi la kusisimua ambapo watoto hujifunza kwa kushirikiana na kufanya majaribio, kama michezo yao ya kawaida. Hii inaongeza tija kubwa kuliko mtindo wa darasani pekee, ambapo mifano kuhusu dhana za kifedha inaweza kuonekana kuwa ya kufikirika zaidi.

Pili, mfumo huu unawajengea watoto misingi ya uwajibikaji, ushirikiano na kufanya maamuzi kwa kuzingatia maadili mazuri, ikiwa ni pamoja na kutathmini athari za kijamii na kimazingira za biashara zao. Wanajifunza kuwa mafanikio ya kifedha hayawezi kutenganishwa na maadili mema. Katika dunia inayotawaliwa na mvuto wa maisha ya kifahari, na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa wa kiuchumi, mafunzo haya ni muhimu kwa kizazi kinachokua.

Tatu, ili maarifa ya kifedha yawe na maana zaidi, ni lazima yajengewe picha ya uhalisia. Mfano, nchini Finland, dhana mbalimbali za kifedha zimejumuishwa katika mtalaa kupitia masomo kama hisabati na maarifa ya jamii, jambo linalowasaidia wanafunzi kuhusianisha dhana za kifedha na maisha halisi.

Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa Finland kwa kuingiza elimu ya fedha katika masomo ya shule za msingi. Kutumia mifano rahisi na inayohusiana na maisha halisi katika kufundisha watoto kuhusu kuweka akiba, matumizi sahihi ya fedha, na mengineyo kunaweza kusaidia kuwajenga kwa misingi bora ya kifedha.

Vilevile, walimu wanapaswa kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo maalumu ya namna ya kufundisha elimu ya fedha kwa watoto, ili kuwapatia nyenzo na maarifa yatakayowawezesha kufundisha elimu ya fedha kwa mbinu bunifu na zenye ufanisi.

Hali kadhalika, ushirikiano kati ya wadau, mashule, benki na taasisi za kifedha unaweza kusaidia juhudi hizo, kwa kuleta elimu ya fedha katika mazingira ya kujifunzia, na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata ujuzi wa moja kwa moja kuhusu mazingira halisi ya kifedha.

Related Posts