Mwalimu Yufresh apatiwa mguu wa bandia

Dar es Salaam. Siku kadhaa baada ya gazeti la Mwananchi na majukwaa yake ya kidijitali kuchapisha taarifa kuhusu Yusuph Ibrahim, mwalimu mwenye ulemavu anayeomba msaada wa kupatiwa mguu bandia, wadau waanza kujitokeza kumshika mkono mwalimu huyo.

Yusuph anayefahamika mitandaoni kama Yufresh amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na aina yake ya ufundishaji inayohusisha nyimbo na michezo ya watoto anayofanya akiwa na mguu mmoja.

Mwalimu huyu wa shule ya msingi Kisuma iliyopo kata ya Nyaminyusi halmshauri ya Kasulu vijijini mkoani Kigoma alieleza Mwananchi kuwa anapitia maumivu makali kwa shughuli anavyofanya akitegemea mguu mmoja.

Mei 14, 2024 Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ilitoa Sh700,000 ikiwa ni sehemu ya kuchangia upatikani wa mguu wa bandia kwa mwalimu huyo.

Akizungumzia msaada huo, Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Evarlasting Lyaro amesema wameguswa kutokana na moyo wa kujitoa anaoonekana kuwa nayo mwalimu huyo.

“Anaonekana ni jinsi gani anaipenda kazi yake, changamoto aliyonayo haitakiwi kuwa kikwazo ndiyo maana tukaona na sisi tuwe sehemu ya kuchangia ili hitaji lake la mguu bandia liweze kufanyiwa kazi.

“Ni imani yetu kwamba akifanikiwa kupata huo mguu atawafikia wanafunzi wengi na itampunguzia maumivu ambayo anayapata sasa kwa sababu analazimika kuzunguka huku na kule akiwa na mguu mmoja. Tunahitaji kuwa na watu wanajitotea na kupenda kazi zao kama huyu,” amesema Evarlasting.

Kwa upande wake, Yufresh ameishukuru mamlaka hiyo kwa kuguswa na tatizo lake na kuomba wadau wengine kuwa sehemu ya kuwezesha kupata mguu bandia ili kumuwezesha kufanya kazi yake kwa ufanisi.

“Kiukweli napitia maumivu makali wakati wa kutekeleza majukumu yangu, naonekana nina furaha nikiwa nacheza na wanafunzi wangu ni kweli nafurahia lakini pia napata maumivu makali.

“Kusimama ubaoni ukiwa na mguu mmoja sio kitu rahisi, hivyo kuwepo kwa watu wanaoguswa na kufanikisha mimi kupata mguu bandia ni jambo la kumshukuru Mungu niwaombe na wadau wengine waguswe,” amesema Yufresh.

Mwalimu huyo ameeleza kuwa gharama ya mguu bandia ni Sh4.5 hadi sasa amefanikiwa kupata Sh2.1 milioni kiasi kinachopungua ni Sh2.4 milioni.

Related Posts