Mikusanyiko yapigwa marufuku Musoma | Mwananchi

Musoma. Serikali wilayani Musoma mkoani Mara imepiga marufuku mikusanyiko ikiwepo shughuli za matanga na maombolezo katika maeneo yenye mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ikiwa ni mkakati wa kudhibiti ugonjwa huo wilayani humo.

Hadi sasa jumla ya watu 63 wameugua ugonjwa huo huku mtu mmoja akifariki tangu ugonjwa huo ulipuke wilayani humo Januari 23, 2025 huku chanzo kikielezwa kuwa ni matumizi hafifu ya vyoo bora na safi katika maeneo yaliyoathirika.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema leo Alhamisi Februari 20, 2025 kuwa kwa sasa kuna wagonjwa wanne katika kambi iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu wilayani humo.

“Kwa muda wa siku tatu sasa hatuna wagonjwa wapya na hawa bado wapo hospitalini kwasababu walifika wakiwa na hali mbaya lakini jitihada za madaktari zimesaidia kuwaondoa katika hali mbaya na sasa angalau wanaendelea vizuri,” amesema

Amesema ili kuhakikisha hakuna maambukizi mapya zipo hatua kadhaa zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa ya lazima kama matanga ambapo waombolezaji hawaruhusiwi kula misibani wala kufanya matanga.

Amesema pia wameanza kugawa dawa za kutibu maji kwa kila kaya katika maeneo hayo baada ya vipimo kuonyesha kuwa vyanzo vya maji vingi vina vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.

Amesema hadi sasa ugonjwa huo umebainika katika vijiji viwili katika halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini ambavyo ni Bwaikwitururu na Bwaikumsoma katika Kata ya Kiriba na kwamba jitihada zinafanyika ili kuhakikisha hakuna mlipuko katika maeneo mengine zaidi.

Chikoka amesema timu ya wataalamu na viongozi wa halamshauri hiyo wanatembelea vijiji vyote kutoa elimu inayokwenda sambamba na oparesheni ya kuzibaini kaya ambazo hazina vyoo.

“Kama utakumbuka Mkuu wa Mkoa aliagiza tutoke ofisini twende vijijini kupambana na hili tatizo, hivi ninavyoongea na wewe niko njiani naelekea vijijini tunachofanya ni kutoa elimu juu ya matumizi ya maji yaliyochemshwa bila kusahau vyoo bora na safi pamoja na kugawa dawa za kutibu maji,” amesema.

Februari 17, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi aliwaagiza wakuu wa Wilaya za Rorya na Musoma kupiga kambi katika maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo ili kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kuenea na kusababisha madhara zaidi.

 “Ni aibu karne hii wilaya kukumbwa na ugonjwa kama huu ambao tunajua unasababishwa na nini, wakuu wa wilaya nawaagiza tokeni ofisini nendeni kwa wananchi fanyeni operesheni elimsheni wananchi wanatakiwa kufanya nini ili kuepuka maambukizi zaidi,” amesema.

Mtambi alisema amebaini uwepo wa ufuatiliaji hafifu kwa kwa wakuu hao wa wilaya baada ya kutolewa kwa maagizo jambo ambalo kwa namna moja ama nyingine linasababisha wananchi kutokufuata maagizo wanayopewa.

 Alisema wananchi wanapaswa kuongozwa kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya kwa maelezo kuwa ugonjwa huo unaweza ukaepukika endapo wananchi watafiata maelekezo hayo.

“Hili jambo halipendezi ni bahati mbaya kwamba pamoja na kujua njia za kukabiliana na ugonjwa huu lakini watu bado wazito kubadilisha mfumo wa maisha na hii inasababishwa na kutokufanyika kwa ufuatiliaji wa maagizo yanayotolewa,” amesema.

Amesema uwepo wa ugonjwa huo katika wilaya hizo pamoja na mambo mengine kunasababisha kusimama kwa shughuli za maendeleo katika maeneo husika.

Baadhi ya wakazi wa Musoma, wamesema ni vyema hatua zikachukuliwa kwa wale wote ambao wanakiuka maelekezo ya wataalamu wa afya juu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara.

“Nakumbuka kulikuwa na kampeni ya nyumba ni choo sijui iliishia wapi,kama inawezekana basi kampeni hiyo ifufufuliwe kwakweli ni aibu kwa watu kutokutumia vyoo,” amesema Grace Joachim.

Annastazia Mabere amesema matumizi hafifu ya vyoo katika baadhi ya maeneo ni matokeo ya kutokuwajibika kwa viongozi wa maeneo husika kwani zipo sheria na kanuni zinazotakiwa kufuatwa dhidi ya kaya ambazo hazina vyoo.

“Sikumbuki vizuri lakini nadhani endapo kaya itakutwa haina choo basi inatakiwa kutozwa faini ya Sh50, 000 na hizi kaya zinajulikana kwasbabu kuna viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kata sasa cha kujiuliza wanashindwa nini kusimamia sheria,” amesema.

Related Posts