Kigoma. Shahidi wa pili katika shauri la uchaguzi wa viongozi wa Mtaa wa Livingstone, Kata ya Singirima, Manispaa ya Kigoma Ujiji, amesimulia aliyoyashuhudia yakijiri ndani ya kituo cha kupigia kura akiwemo watu kupiga kura zaidi ya mmoja na mtendaji Kata alivyoingiza kura bandia.
Shahidi huyo Zainabu Hamisi alikuwa wakala wa mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, katika uchaguzi huo, Luma Akilimali, wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa mwaka 2024.
Wajibu maombi (walalamikiwa) katika shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Aristida Tarimo ni aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo, Mawazo Kiembe’ msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa Livingstone na Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).
Akilimali anadai mchakato wa uchaguzi na uchaguzi huo wenyewe haukuwa huru na wa haki kwa kuiuka kanuni zilizowekwa na hivyo kuifanya kuwa batili, kutokana na kasoro zilizojitokeza.
Amebainisha kasoro hizo ni pamoja na mchakato wa uandikishaji wapiga kura kutokufanyika kwa mujibu wa kanuni, ongezeko la wapigakura, mtendaji wa kata kuharibu uchaguzi kwa kuingia kituoni na kura alizozichangaya kwenye kura zilizokuwa zinahesabiwa.
Nyingine ni baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya moja huku wakisadiwa na msimamizi msimaidizi, sanduku la kura za mwenyekiti kuwekwa mafichoni ambako mawakala hawakuwa wanaona waliokuwa wanatumbukiza kura, watu wasiokuwa wakazi kupiga kura na kuingizwa kura bandia.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo itamke uchaguzi huo ni batili, imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku 14 na ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo ufanyike.
Kwa mujibu wa ushahidi wake Zainabu akiongozwa na Wakili Eliutha Kivyiro anayemwakilisha mwombaji, siku ya uchaguzi siku ya kura alifika kituoni saa 12 asubuhi.
Akiwa kituoni hapo mara lilifika gari la vifaa vya uchaguzi na wakati inashusha vifaa msimamizi wa uchaguzi anayeitwa Joakim alimuondoa alipokuwa akishuhudia vifaa vikishushwa na alipohoji akamwambia kuwa hatakiwi kuhoji maswali.
Katika kituo cha kupigia kura sanduku la mwenyekiti liliwekwa (mafichoni) katika chumba cha siri kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya kupigia kura mahali ambako mtu akiingiza kura hawakuwa walimuona ila masanduku mawili tu ya kuraza qajumbe ndio yalikuwa yakionekana.
Kutokana na hali hiyo yeye alitoka akamuita mwenyekiti wake Luma (mwombaji) aje aangalie hali ilivyokuwa naye aliangalia akaondoka kisha akarudi na viongozi wengine wawili wa ACT kulalamika sanduku hilo litolewe lakini msimamizi Joakim akakataa.
Baadaye alifika msimamizi wa uchaguzi Mkurugenzi wa Manispaa akaliweka sehemu ya wazi na muda wote huo kura zilikuwa zimeshaanza kupigwa na watu waliendelea kupiga kura.
Katika upigaji kura kuna watu waliopiga kura zaidi ya mmoja kwani alimuona mtu aliyetumbukiza kura zaidi ya moja na alipolalamika msimamizi msaidizi akamshtaki kwa askari kwamba analeta fujo na akamuonya kuwa akiongea tena neno lingine wanamtoa nje.
Baadaye jioni kwenye saa 12 jioni wakiwa wanachambua kura za mwenyekiti na za wajumbe kwa ajili ya kuhesabu alifika mtendaji wa kata akiwa na kura nyingi mkononi akazichanganya na kura zilizokuwa zimeshapigwa.
Mara lilitokea kundi la watu zikatokea vurugu wakapiga mawe kituo na shughuli ya kuhesabu kura ikaishia hapo, hivyo kura hazikuhesabiwa tena.
Akihojiwa na Wakili Ignatus Kaghashe anayemwakilisha Mawazo, mjibu maombi wa kwanza aliyekuwa mgombea wa CCM aliyepitishwa kuwa mwenyekiti, amesisitiza sanduku la mwenyekiti lilikuwa ndani ya chumba kilichokuwa kimetengenezwa kwa ajili ya kupigia kura.
Hata hivyo, hakushuhudia mpigakura aliyepewa karatasi za kura zaidi ya moja, lakini akasema kuwa matokeo hayakutangazwa na hivyo hakumjua mshindi mpaka kesho yake ndio alisikia kuwa alipitishwa Mawazo wa CCM.
Amefafanua alijua mtendaji alizokuja nazo zilikuwa ni kura kwa sababu alifika akazichanganya na zile kura zilizokuwa zimeshapigwa.
Awali, shahidi wa kwanza ambaye ni mwombaji katika shauri hilo, Luma ameieleza Mahakama alivyoitwa na wakala wake huyo kushuhudia sanduku hilo la kura za mwenyekiti lilivyokuwa limewekwa mafichoni.
Pia, ameeleza jinsi walivyozozana na msimamizi msaidizi akataa kuliweka wazi mpaka walipomjulisha Mkurugenzi ambaye alifika kituoni hapo muda wa saa nne asubuhi ndio akalitoa mafichoni akaliweka sehemu ya wazi.
Amedai kuwa alipiga kura majira ya jioni akiwa miongoni mwa watu wa mwishoni kupiga kura baada ya kupiga kura alikuwa amekaa katika nyumba ya tagu kutoka kituoni hapo.
Kwa umbali huo amedai kuwa alikuwa akiona kila kilichokuwa kinaendelea ndani ya kituo ambacho kilijengwa kwa turubai upande mmoja ikiwa wazi.
Shahidi huyo mlalamikaji amedai akiwa hapo mara alipita mtendaji wa kata hiyo akiwa na karatasi za kura alizokuwa amezishikilia mkononi na alipoingia kituoni alizichanganya na kura nyingine zilizokuwa zinaendelea kuhesabiwa.
Kutokana na hali hiyo kuliibuka vurudu wakafika askari wakaondoka na masanduku, hivyo kura hazikuhesabiwa mpaka mwisho na kwamba kituo kilichomwa moto.
Akisoma fomu namba 8A ambayo ni fomu ya matokeo ya mwenyekiti, iliyopokewa na Mahakama na kuwa kielelezo cha ushahidi wake amesema kuwa matokeo kwake si sahihi.
Amesema kuwa walioandikisha walikuwa 403 waliopiga kura 285 na kura halali 285 na zilizoharibika zilikiwa 16, huku ikionesha kwamba mgombea wa CCM alipata kura 187 na yeye kura 89.
Licha ya mkanganyiko kuwa kura zilizopigwa zilikuwa 285 na zilizoharibika 16 bado kura halali zikabakia zilezile 285, kura za wagombea hao wawili pekee pamoja na zilizoharibika zinazidi idadi ya kura zilizopigwa kwa kura 7 bila kujumuisha za wagombea wengine wanne.
Hivyo aliieleza Mahakama kuwa hakuridhika na matokeo hayo kwani uchaguzi haukuwa huru na wa haki na ndio maana anaiomba mahakama itengue uchaguzi wa huo, iamuru urudiwe kwa gharama za wajibu maombi na apewe haki nyingine yoyote anayostahili.
Akihojiwa na Wakili Kaghashe wa mujibu maombi wa kwanza, amesema matokeo hayakutangazwa na kwamba ilivyokuwa wasimamizi walipomaliza tu wakaondoka na alijua mshindi baada ya kupata hizo fomu kuwa aliyeshinda ni mgombea wa CCM kwa kura 187 na yeye alipata kura 89.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa wakala wake wakati wa zoezi la kuandikisha wapigakura waliojiandikisha walikuwa 237 lakini majina yaliyobandikwa yalikuwa 403 jambo ambalo linaonesha kuwa kuna majina yaliongezwa.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Urso Luoga amesema kuwa alimuona mtendaji aliingia kituoni akiwa ameshika kura kwani aliwapita alipokuwa amesimama, lakini akasema hajui zilikuwa za chama gani na wala hawezi kujua zilikuwa ngapi.
Amefafanua kuwa kura bandia ni zile zinazokutwa zaidi ya moja zikiwa zimeshikana pamoja.