Ile mishuti ya Ulomi sio ya bahati mbaya

HIVI unayafuatilia mabao anayofunga mshambuliaji wa Mashujaa, David Ulomi? Hadi sasa nyota huyo ana mabao manne na yote yanafanana, licha ya kuyafunga kwa timu mbili tofauti na mwenyewe akifichua mabao hayo hayafungi kwa kubahatisha ila anayafanyia kazi mazoezini.

Ulomi alifunga bao la pili kali katika ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Mashujaa dhidi ya Pamba Jiji katika pambano la Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma ukiwa ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo hiyo tangu iliposhinda mara ya mwisho Novemba 23, mwaka jana.

Mashujaa ilikuwa imecheza mechi nane mfululizo bila kupata ushindi  tangu ilipoinyoosha Namungo kwa bao 1-0, lakini juzi ikiwa nyumbani ilishinda 2-0 bao la kwanza likiwekwa kimiani na Hassan Hadji ‘Cheda’, aliyewahi mpira wa penalti uliopigwa na Danny Lyanga na kuokolewa dakika ya 35.

Ndipo dakika ya 83, Ulomi alipopiga shuti kali nje ya eneo la 18 akipokea pasi ya Jaffary Kibaya na kumshinda kipa wa Pamba, Yona Amos na kuuzamisha mpira wavuni.

Sasa kama ulidhani Ulomi anabahatisha kumtungua Yona, utakuwa umekosea kwani alishamfunga tena katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyoisha kwa sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza pale alipofunga mabao mawili yaliyoiokoa Mashujaa kufa ugenini.

Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao yote mawili ya kusawazisha baada ya Mashujaa kutanguliwa, bao la pili la dakika ya 83 ndilo lililoonekana bora zaidi, baada ya kupiga shuti la mbali lililomshinda kipa wa Pamba, Yona Amos na kuzama wavuni.

Kama haitoshi, nyota huyo alifunga pia bao la mbali wakati kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-2, dhidi ya Yanga Desemba 19, 2024, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC na kushuhudia Prince Dube akifunga ‘hat-trick’ ya kwanza ya msimu huu.

Ulomi alifunga bao hilo dakika ya 45, akiwa nje ya eneo la 18 na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga, Khomeiny Abubakar na kuzama wavuni, huku lingine la kikosi hicho cha ‘Mapigo na Mwendo’, likifungwa na Idrisa Stambuli dakika ya 62.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ulomi alisema siri ya mabao yake ni kutokana na kufanyia mazoezi kwa kiasi kikubwa, huku moja ya jambo lingine ni kupewa uhuru na benchi la ufundi, la kujaribu mara kwa mara pindi anapoona kuna nafasi ya kupiga.

“Muhimu ni ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu kwa sababu bila ya wao siwezi kufanya lolote,” alisema nyota huyo wa zamani wa timu za Ruvu Shooting, Dodoma Jiji, Al Hilal ya Sudan na Moroka Swallows ya Afrika ya Kusini.

Matokeo ya juzi yaliifanya Mashujaa kuchupa hadi nafasi ya  sita ikifikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 20, lakini likimfanya Ulomi kufikisha mabao manne hadi sasa katika Ligi Kuu inayoendelea tena leo kwa michezo miwili, mapema saa 8 mchana Tanzani Prisons iliyotoka kupoteza 3-2 ugenini mbele ya Dodoma Jij itaialika Tabora Unitedi. Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kabla ya saa 10 jioni, maafande wa JKT Tanzania wataikaribisha Kagera Sugar inayoshika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo wenye klabu 16. Mchezo huo wa JKT na Kagera utapigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo, jijini Dar es Salaam.

Related Posts