Dar es Salaam. Wakati wateja 7,000 nchini wakinufaika na mikopo ya nyumba, Watanzania wametakiwa kutumia fursa hiyo kuweza kumiliki nyumba zinazotolewa kwa mkopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkopo wa nyumba unatolewa na taasisi ya fedha ya Tanzania Mortgage Refinance Company Limited (TMRC) kupitia wanahisa wake 20 ikiwamo Benki ya KCB.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya amesema mikopo ya nyumba sasa inapatikana kote nchini, inatoa fursa ya Watanzania kumiliki nyumba kwa riba nafuu na malipo kidogo kidogo kama ambavyo angelipa kodi ya pango.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati taasisi hiyo ikimkaribisha mwanahisa mpya, Benki ya KCB (T) Ltd iliyowekeza Sh500 milioni, Mgaya amesema ni rahisi sasa Watanzania wengi kumiliki nyumba kupitia mkopo.
Amesema tangu kuanzishwa kwa TMRC miaka 10 iliyopita, wanahisa wameongeza na sasa kuna wanahisa 20 wanaotoa mikopo ya nyumba ambao ni wa muda mrefu kati ya miaka 15 hadi 20.
“Wanahisa wanapoongezeka ndipo fursa zaidi zinaongezeka, hivyo hivi sasa rahisi Watanzania kuweza kumiliki nyumba kupitia wanahisa wetu 20,” amesema Mgaya na kubainisha kwamba tangu mikopo ya nyumba imeanza wateja 7,000 wamenufaika nao.
Mbali na KCB, miongoni mwa wanahisa wengine 20 wa TMRC ni benki za CRDB, NMB, NBC, TIB Development Ltd, Azania, Exim na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), pamoja na mashirika ya kimataifa ya kifedha kama Shelter Afrique na International Finance Corporation (IFC).
Kwa mujibu wa Mgaya, mtandao wa mikopo ya nyumba umetanuka kwa kutolewa kote nchini, ambapo mteja anaweza kununuliwa nyumba au kujenga nyumba kupitia mkopo huo wa muda mrefu hadi miaka 20.
Mkurugenzi wa Biashara za Kanda wa KCB Group na Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank Tanzania, Cosmas Kimario, amesema milango ipo wazi kwa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo.
“Wengi tunafahamu ambavyo ni mchakato kujenga nyumba, kuna watu anaanza kujenga kidogo kidogo hadi anafikia hatua ya kumaliza naye anakuwa anastaafu, kupitia mkopo wa nyumba atamiliki nyumba kwa muda mfupi,” amesema.
Amesema mikopo ya taasisi nyingi za benki huwa ni ya miaka mitatu hadi saba, lakini katika mikopo ya nyumba ni miaka 15 hadi 20, hivyo kumpa fursa mteja kulipa kidogo kidogo bila kuhisi maumivu ya makato..
“Unapolipa mkopo wa nyumba, pesa ambayo ungeitumia kulipa kodi ndiyo unaitumia kuinunulia nyumba na kulipa kidogo kidogo hivyo inakurahisishia,” amesema.
Amesema KCB kuwa mwanahisa wa TMRC ni uwekezaji wa kimkakati ambao unawapa uwezo wa kutoa mikopo zaidi ya nyumba na kuchangia maendeleo ya makazi.