Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabiliwa washtakiwa 13 wanaokabiliwa mashtaka ya kuhujumu uchumi, likiwemo la kuharibu noti zenye thamani ya Sh4.6 bilioni bado unaendelea.
Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano, likiwemo la kuchanachana noti hizo na kuisababishia Benki Kuu ya Tanzania hasara ya Sh4.6 bilioni.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameeleza hayo leo Alhamisi, Februari 20, 2025 kesi hiyo ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 100/2022 ni Mariagoreth Kunzugala maarufu Bonge, Henry Mbowe maarufu Mzee wa Vichwa, Asha Sekiboko, Cecilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanaheri Omary wote walikuwa wafanyakazi wa BoT na wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa wengine ambao si watumishi wa BoT ni Alistides Genand, Musa Chengula, Zaituni Chihipo na Respicius Rutabilwa.
Kasala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Geoffrey Mhini.
“Kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika, na hakimu anayesikilizaa shauri hii Anna Magutu yupo likizo, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedia Wakili Kasala.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Machi 20, 2025 kwa kutajwa.
Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kuiomba Mahakama Kuu.s
Katika hati ya mashtaka inadaiwa, kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30, 2019, washtakiwa wakiwa Watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Pia inadaiwa, Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga.
Katika shitaka la tatu, washtakiwa wote, waliharibu noti 460,000 za Sh10,000 kila moja, zenye thamani ya Sh4.6 bilioni kwa kuzikatakata.
Katika shitaka la nne, siku na maeneo hayo, washtakiwa wote walijipatia faida ya Sh1.5 bilioni kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.
Katika shitaka la tano washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia BoT hasara ya Sh bilioni 4.6
Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita, lakini Juni 18, 2021, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwafutia shtaka la kutakatisha fedha na hivyo kubaki na mashtaka matano.