Twiga Stars yaimaliza Guinea, bado 90 ugenini

Twiga Stars imeanza vyema kampeni za michuano ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco, baada ya ikiitandika Equatorial Guinea kwa mabao 3-1 katika mchezo mkali uliopigwa jana, Uwanja wa Azam Complex.

Twiga ambayo imekuwa na kikosi bora kwa miaka ya hivi karibuni, ilionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huo uliokuwa umehudhuriwa na wanafunzi wengi kutoka shule mbalimbali.

Stars ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0, liliwekwa kimiani na Getruede Engueme katika dakika ya  42 kwa shuti la mbali ambalo lilimshinda kipa Naijat Abas.

Twiga ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo pamoja na rekodi nzuri ya Guienea ya kutwaa ubingwa huu mara mbili, ilirejea kipindi cha pili na nguvu kubwa na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 49 kupitia kwa Stumai Abdallah aliyepokea pasi kutoka kwa Clara Luvanga dakika sita baadaye Enekia Lunyamila aliifungia Twiga bao la pili kwa kichwa akimalizika krosi ya Lydia Kabambo.

Pamoja na Guinea, kupambana ikitaka kusawazisha bao hilo, mambo yalikuwa magumu zaidi kwao baada ya kuruhusu bao la tatu lilowekwa kimiani na Diana Msewa katika dakika ya 90, likiwa ndiyo bao lilishangiliwa zaidi kutoka na ubora wa mfungaji baada ya kuwapiga chenga wachezaji watatu na kipa wao na kufunga kiufundi.

Ushindi huu umeiweka Twiga kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya pili kwenye mchezo wa pili utakaopigwa Guinea wikiendi ijayo. Endapo timu hiyo chini ya kocha Bakari Shime itavuka kwenye hatua hii itakutana na mshindi kati ya Uganda na Ethiopia, ambao mechi yao ilikuwa ikipigwa jana jioni.

Related Posts